Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya
Mipango Bibi Florence Mwanri anayeongoza timu ya ukaguzi wa miradi
kutoka Tume ya Mipango akielekea kukagua mradi wa ufugaji ngo’ombe na
uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa katika eneo la Narunyu
wilayani Lindi. Kulia ni Bi, Yasinta Mrose (Mtawa) ambaye anasimamia
upande wa mifugo.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri akitoa ushauri kwa uongozi wa mradi
ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa (ambao ni watawa) katika moja
ya mabanda ya ng’ombe wa maziwa. Wengine ni maofisa wa Serikali
walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji huyo.
Baadhi ya ng’ombe wa maziwa wa
mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa
eneo la Narunyu wakiwa katika banda.
Bi Yasinta Mrose (Mtawa)
akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri
hatua za awali za kutengeneza gesi kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya
Mipango, Florence Mwanri akiwa ndani ya chumba ambapo gesi inazalishwa
(gesi ipo ndani ya turubai lililojaa ndani ya chumba hicho linaloonekana
chini).
Mwonekano wa Kiwanda cha kuzalisha nishati inayotokana na kinyesi cha ng’ombe.
Ndama
wanaofugwa katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa
unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wakiwa katika banda.
PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO
……………………………………………………………….
Na Adili Mhina, Lindi
Tume ya Mipango imefanya ziara
katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na
watawa eneo la Narunyu wilayani Lindi na kushauri uongozi wa mradi huo
kutumia fursa za mikopo ya kilimo ili kupanua wigo wa uzalishaji wa
mazao ya mifugo pamoja na kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme kwa
kutumia kinyesi cha wanyama.
Mradi huo umekuwa ukizalisha
maziwa na nyama kwa ajili ya biashara huku nishati ya umeme kwa ajili
kuendesha shughuli za kiwanda hicho ikiwa inazalishwa kutokana na
kinyesi cha wanayama hao.
Kwa sasa uzalishaji umepungua
baada ya kiwanda kushindwa kuzalisha nishati ya umeme ya kutosha na
kuanza kutegemea umeme wa tanesco ambao kwa mujibu wa mmoja wa
wasimamizi wa mradi huo, Bi Yasinta Mrose umesababisha gharama za
uzalishaji kuongezeka.
Changamoto nyingine ni
kuharibika kwa baadhi mashine zinazotumika kuandaa malisho ya ngo’ombe,
ukosefu wa soko la karibu kwa mazao ya nyama na maziwa, pamoja na uhaba
wa maeneo kwa ajili ya malisho ambapo kwa sasa mradi una zaidi ya
ng’ombe 400.
Kutokana na changamoto hizo,
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri aliueleza
uongozi huo kuwa ni vyema wafanye taratibu za kuomba mkopo hususani
katika benki ya kilimo ili waweze kuongeza mtaji, uzalishaji na kupanua
soko.
“Huu ni mradi mzuri na msirudi
nyuma katika uzalishaji wenu, nawashauri mkae mjadiliane muone namna ya
kupata mkopo ili muweze kununua mashine za kisasa na muongeze
uzalishaji. Bila kuchukua hatua hizo mnaweza mkashangaa mradi unakufa
wakati unafaida kwenu na hata kwa wananchi wanaowazunguka,” alieleza.
Kuhusu changamoto ya soko la
karibu, Mwanri alieleza kuwa uongozi unapaswa kufikiria kuzalisha maziwa
na kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa na kusafirisha nje ya
wilaya ya Lindi kwani soko bado ni kubwa.
Aliongeza kuwa hatua iliyofikiwa
ya kuzalisha umeme wa kutosha kuhudumia shughuli zote za uzalishaji
kiwandani hapo ni nzuri na Serikali inaiunga mkono jitihada za sekta
binafsi katika kukuza maendeleo ya uchumi ikiwa ni njia ya kutekeleza
malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2016/17-2020/21).
“Nimefarijika sana kusikia
mlikuwa mnazalisha umeme wa kuwatosheleza, mmejitahidi kutekeleza mpango
wa Taifa wa Maendeleo kwa vitendo. Tume ya Mipango inatambua na kuunga
mkono jitihada zenu hivyo nawasihi shirikianeni na Halmashauri kufanya
kila linalowezekana ili shughuli zenu ziendelee zaidi ya mlivyokuwa
mnazalisha huko nyuma,” aliongeza.
No comments :
Post a Comment