Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi amelishukuru Shirika la Nyumba Taifa (NHC) kwa msaada wa
mifuko ya saruji 10, kofia za bati 20, mabati 90 ya geji 28 vyote
vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 2.6 milioni ukiwa ni msaada kwa
ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la sekondari Mwanzi iliyoko
Wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Dkt. Nchimbi ametoa shukrani hizo
juzi wakati akipokea masaada huo kutoka kwa Meneja wa NHC Mkoa wa
Singida Ladislaus Bamanyisa na kutoa wito kwa mashirika, watu binafsi na
taasisi zikiwemo mabenki, kuiga mfano mzuri wa NHC kusaidia serikali
katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.
“Mimi nitumie nafasi hii kuwaita
au kuwaalika mabenki na taasisi zingine kuja mkoani Singida kutuunga
mkono katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi,
pamoja na uboreshaji wa miundo mbinu ya shule za msingi na
sekondari”,amesema.
Ameongeza kuwa benki, shirika au
watu binafsi watakaojitokeza kuunga mkono kuuendeleza Mkoa wa Singida
kwa kujenga jengo lo lote pamoja na majengo ya shule, huduma za afya na
mengine yanayolenga kuwanufaisha wananchi, wataruhusiwa kupaka rangi na
kuweka nembo zao ili kutangaza shughuli au huduma wanazotoa.
Amesema kwa njia hiyo benki,
taasisi au watu binafsi watakuwa wamejitangaza na tangazo hilo litadumu
kwa muda mrefu ikilinganishwa na matangazo mengine.
“Kwa upande wa wadau binafsi na
wao wataruhusiwa kuweka picha za familia zao kwenye majengo au miradi
husika. Kama ni mfugaji na ameuza sehemu ya mifugo yake kugharamia
miradi wa umma, ataruhusiwa kuweka picha ya familia na ng’ombe zao”,
amesema Dkt. Nchimbi.
Naye Meneja wa NHC Mkoa wa Singida
Ladislaus Bamanyisa, amesema wataendelea kuiunga mkono serikali katika
kuboresha sekta mbalimbali na huo mchango ni sehemu ndogo ambapo shirika
bado linaendele ana jitihada za kukusanya michango mingine.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Nchimbi amezungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya
ya Manyoni na kuwaeleza kuwa halmashauri za wilaya na manispaa zimekuwa
ni chanzo au viwanda vya kuzalisha mabango na kelele nyingi kwa wananchi
kutokana na huduma zisizokidhi mahitaji na ubadhirifu wa fedha za umma.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa
ataelekeza nguvu zake kuanzisha na kufufua kilimo cha umwangiliaji na
ufugaji wa samaki ili Mkoa uweze kunufaika kiuchumi na ujio wa makao
makuu kuhamia mkoa jirani wa Dodoma.
“Sisi wakazi wa mkoa wa Singida
sote ni lazima tujiandae kikamilifu kulisha makao makuu ya nchi
yatakapokuwa Dodoma. Tuitumie fursa hiyo kumtokomeza adui umaskini”,
amesisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni
Geofrey Mwambe amesema wakati wanaendelea na ujenzi wa bweni halmashauri
ya Manyoni imejipanga pia kujenga uzio katika shule hiyo ya sekondari
ya Mwanzi ili kuboresha ulinzi katika shule hiyo.
Mwambe amesema kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wanamalizia ujenzi wa bweni moja na kuanza ujenzi wa
bweni lingine huku akiwashukuru wafanyabiashara wa Wilaya ya Manyoni kwa
kujitoa katika kusaidia maendeleo ya Wilaya hiyo.
No comments :
Post a Comment