Thursday, December 15, 2016

PROF. MBARAWA: SERIKALI KUJENGA DARAJA KUBWA MKOANI MWANZA


mwanzo
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), na Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mwanza Eng. Fredinand Mishamo (kushoto), wakiingia katika Kivuko cha MV TEMESA wakati alipokagua kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Kijiji cha Luchelele na Irunda, mkoani Mwanza.
mwanzo-1
Muonekano wa Kivuko cha MV TEMESA kinachotoa huduma zake katika Kijiji cha Luchelele na Irunda, mkoani Mwanza. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 80, magari 5 kwa wakati mmoja.
mwanzo-2
Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mwanza Eng. Fredinand Mishamo (kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu hali ya utendaji wa kivuko cha MV TEMESA wakati alipokagua kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Kijiji cha Luchelele na Irunda, mkoani Mwanza.
mwanzo-3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akielekezwa na Nahodha Mkuu wa kivuko cha MV TEMESA (kulia), wakati alipokagua kivuko hicho, mkoani Mwanza.
mwanzo-4
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Luchelele, mara baada ya kukagua kivuko cha MV TEMESA kinachotoa huduma kati ya Kijiji hicho na Irunda, mkoani Mwanza
mwanzo-5
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza Road Works inayojenga kwa kiwango cha lami barabara ya Usagara-Kisesa yenye urefu wa KM 16, mkoani Mwanza.
mwanzo-6
Mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza Road Works (wa pili kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuhusu hatua ya ujenzi iliyofikiwa ya barabara ya Usagara-Kisesa yenye urefu wa KM 16 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mwanza. Wa pili kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya.
mwanzo-8
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Usagara-Kisesa yenye urefu wa KM 16 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mwanza. Barabara hiyo inatarajiwa kukamilika Mwezi Februari mwakani.
mwanzo-7
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wafanyakazi wa taasisi za wizara hiyo alipokutana nao mkoani Mwanza.
………………….
Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 litakalounganisha eneo la Kigongo na Busisi, wilayani Misungwi Mkoani Mwanza ...

Kauli hiyo imetolewa mkoani Mwanza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akizungumza na watumishi wa Taasisi za Wizara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesema  tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutekekeleza kazi hiyo.
“Serikali ina nia ya dhati kwa wananchi wake katika kuhakikisha wanapata miundombinu iliyobora kwa maendeleo yao, hivyo basi wananchi wa mkoa huu mtarajie kupata daraja jingine kubwa la Kigongo-Busisi”, amesema Waziri Mbarawa.
Ameongeza kuwa kuhusu suala la ununuzi wa meli mpya ya kisasa itakayotoa huduma mkoani Mwanza na Bukoba, tayari Serikali imeshatenga fedha na majadiliano kwa ajili ya ununuzi wa meli hiyo yataanza wiki ijayo.
Prof. Mbarawa amewataka watumishi hao kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa haraka, uadilifu na uwazi  ili kuboresha utendaji na kwenda sambasamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea Kivuko cha
Mv Temesa kinachotoa huduma kati ya Kijiji cha Irunda na Luchelele mkoani  Mwanza na kumtaka Meneja wa kivuko hicho kuhakikisha anasimamia wananchi katika kuilinda na kuitunza miundombinu ya kivuko hicho.
Pia amemtaka Meneja huyo kufunga mifumo ya kielektroniki ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), mkoani Mwanza, Eng. Fredinand Mishamo, amemhakikishia Waziri huyo kuboresha hali ya miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ili kivuko hicho kijiendeshe chenyewe bila kutegemea ruzuku kutoka TEMESA Makao Makuu.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea barabara ya Usagara – Kisesa (km 16), na kutoridhishwa kwa hatua ya ujenzi wake, hivyo kumtaka Mkandarasi wa Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Roads Works anayejenga barabara hiyo kumaliza ujenzi wake ifikapo mwezi Februari mwakani.
Waziri Prof. Mbarawa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Mwanza ambapo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments :

Post a Comment