WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali itazifutia usajili Taasisi zote zisizokuwa za
Kiserikali (NGO’s) zilizoko kwenye Tarafa ya Loliondo zinazofanyakazi
kinyume na katiba zake na sheria ya nchi ambapo ametoa miezi sita
zijitathimini kama zinafanya kazi ya kuhudumia jamii au la.
Pia ameahidi kumpeleka Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Taraha hiyo ya Loliondo
kwa lengo la kuzifanyia ukaguzi NGO hizo ili kubaini kiasi cha fedha
wanazopata kama zinalingana na matokeo ya kazi za kijamii inazofanya
katika Tarafa hiyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo
(Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati akizungumza na Wakurugenzi wa NGO na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwenye ukumbi wa
Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Amesema NGO nyingi zimekuwa
zikipata bajeti kubwa ya fedha lakini masuala ya maendeleo wanayoyafanya
katika eneo hilo hayalingani na bajeti halisi wanazopata.”Loliondo
pekee kuna NGO zaidi ya 30 ila zilizokuwa ‘active’ ni 15 tu kuna nini
Loliondo? Na baadhi yake zinafanya kazi ya kuchochea eneo hili lisiwe na
amani,”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “watu
wote wanaoshirikiana na NGO hizo zinazochafua taswira ya nchi
tutawashughulikia. Mnawavalisha watoto kandambili zilizotobona na miguu
michafu kisha mnawapiga picha mnazituma kwenye mitandao na kusema
umasikini wa Tanzania ndio huo. Hatutawavumilia watu wa namna hii,”
amesisitiza.
Amesema NGO nyingi zimekuwa
zikilalamikiwa kutokana na kufanya kazi kinyume na mikataba yake ya
usajili na miongoni mwa NGO hizo ni pamoja na PWC inayopata sh. bilioni
2.5 kwa mwaka, UCRT inayopata sh. bilioni 1.5 kwa mwaka, Oxfarm Tanzania
inayopata sh. bilioni 1.7 kwa mwaka.
“Nitafuatilia kwa karibu kuona
kazi wanazozifanya kwani zinapata fedha nyingi kwa mwaka. Lazima tujenge
nidhamu kwa wote wanaopata fedha kwa lengo la kuisaidia jamii. Wote
wanaojihusisha na shughuli nje ya mikataba yao wabadilike ndani ya miezi
sita. Wafuate kanuni, sheria na taratibu za nchi,” amesema.
Amesema Serikali haiwezi kufanya
kazi bila ya wadau ila haiitaji wadau wanaofanya mambo kinyume cha
taratibu, ambapo amezitaka NGO hizo kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa
Kampuni (BRELA) ili ziweze kutambulika kisheria na ofisi zake kujulikana
badala ya hivi sasa kuwa na ofisi za mifukoni.
Awali, Waziri Mkuu alizungumzia na
wananchi wa kijiji cha Ololosokwan ambapo alisema mgogoro wa ardhi
kati ya wananchi wa Tarafa la Loliondo na wawekezaji unaolikabili eneo
hilo Waziri Mkuu mesema Serikali itahakikisha mgogoro huo uliodumu kwa
muda mrefu unamalizika haraka.
Aidha, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Bw. Mrisho Gambo kukutana na uongozi wa wilaya ya Ngorongoro na
kamati ya wananchi iliyoundwa kwa ajili ya kuboresha uhifadhi ili
kumaliza mgogoro huo na kisha kumpelekea taarifa.
“Haiwezekani Waziri Mkuu aje
kumaliza mgogoro wa ardhi Loliondo wakati kuna viongozi hapa. Mimi
nimemuagiza Mkuu wa mkoa aje akutane na wawekezaji na wananchi ili
kuzungumza na kuupatia ufumbuzi mgogoro huu na atakayeshindwa ndiye
nitakayemshughulikia,” amesema.
Amesema Serikali itahakikisha
migogoro ya ardhi inamalizika nchini ili kuwawezesha wananchi kufanya
shughuli zao kwa amani na utulivu. “Naomba tushirikiane katika kutatua
changamoto hii ya migogoro ya ardhi kwani suala hili limeahidiwa katika
ilani ya uchaguzi ya CCM,”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wananchi kuingiza ng’ombe kiholela
kutoka nje ya nchi kwa kuwa kitendo hicho kinachangia kuwepo kwa
migogoro ya ardhi.
Katika kuhakikisha suala hilo
linadhibitiwa Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Rashid Taka
kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo
kuimarisha ulinzi katika mipaka kwa kuongeza doria ili kudhibiti
uingiaji holela wa mifugo.
Naye Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema eneo la Loliondo ni muhimu
sana kwa ajili ya ikolojia ya wanyama pamoja na maji kwani hifadhi ya
Serengeti inategemea zaidi eneo hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 15, 2016.
No comments :
Post a Comment