Kamanda wa Polisi Ilala, Salum Hamdun |
Na Dotto Mwaibale
MTOTO
mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivule
Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam jina lake linahifadhiwa ameelezea
jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka wazazi wake ili asikeketwe.
Mtoto
huyo hivi sasa analelewa na msamaria mwema baada kufungua kesi Kituo
cha Polisi cha Stakishari Ukonga kufuatia kufikishwa kituoni hapo kwa
ajili ya kujisalimisha na kuelezea madhila aliyotaka kufanyiwa.
Wakati
mtoto huyo akijisalimisha katika kituo hicho kuna taarifa za ndani kuwa
kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85 wenye umri kuanzia miaka 12 hadi
15 katika manispaa hiyo ambapo watoto zaidi ya 30 wanadaiwa kukeketwa.
Akizungumza
jijini Dar es salaam mtoto huyo alisema hawezi kurudi tena nyumbani
kwao kwa kuhofia kupigwa na kukeketwa ambapo ameomba msaada wa hifadhi
kutoka kwa watanzania.
“Baada
ya baba yangu kufariki nyumbani kwetu Tarime tulikuja na mama hapa Dar
es Salaam kwa kaka yake Chacha Nyanchiri anayeishi Kitunda Kivule karibu
na Shule ya Msingi Misitu” alisema mtoto huyo.
Alisema
katikati ya wiki iliyopita alifika bibi yake mzaa baba yake aliyemtaja
kwa jina la Boke na kuwaambia yeye na wenzake wajiandaa kwenda
kukeketwa.
Mtoto
huyo alisema kwamba siku ya alhamisi majira ya saa mbili usiku wakiwa
nyumbani kwa mjomba wao anakoishi na mama yake alifika bibi mzaa mama
yake aliyemtaja kwa jina moja la Debora huku akiwa ameongozana na mama
yake Happyness na kuwaambia yeye na watoto wengine wawili wa mama yake
mkubwa wakaoge ili waende kukeketwa.
Alisema
ili kukwepa kukeketwa alipokwenda bafuni alifanikiwa kutoka na kupita
njia nyingine na kufanikiwa kuwatoroka wazazi wake na kwenda kujificha
kwenye pagala na ilipofika saa tatu usiku alifika eneo la kwa Mpemba
akielekea darajani ambapo alikutana na dada mmoja aliyemsimulia mkasa
huo.
Alisema
dada huyo alimchukua hadi nyumbani kwake ambako alilala na siku
iliyofuata alimpeleka kituo cha Polisi cha Stakishari kwa ajili ya
usalama wake.
Mmoja
wa wakazi wa eneo hilo ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kuna
mpango wa kuwakeketa watoto 85 kabla ya kuisha kwa mwaka huu wa 2016 na
kuwa karibu watoto 30 wamekwisha keketwa.
Alisema
shughuli hiyo inasimamiwa na wazee wa kimila wa kabila la kikurya na
kuwa ngariba mkuu wa kazi hiyo ya kukeketa watoto hao yupo eneo la
Nyamuhanga na kuwa baada ya kukeketwa ufanyiwa sherehe kwa siri katika
baadhi ya nyumba zilizopo jirani na ngariba huyo.
Mwenyekiti wa Serikali wa mtaa anaoishi mtoto huyo, Dominick Mlimi alisema hana taarifa ya mtoto huyo kutoweka nyumbani kwao.
“Jana
niliwaona baadhi ya watoto wa kike wa familia ya Nyanchiri wakiwa hapo
barabarani lakini kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo kwa kuhifia kukeketwa
sijazipata” alisema Mlimi.
Mke wa
Chacha Nyanchiri ambaye anaishi na mtoto huyo Regina Wilison alikiri
mtoto huyo kuondoka usiku baada ya kufika nyumbani hapo bibi yake na
mama yake ingawa alisema hawakutoa taarifa kwa mtu yeyote ya kutoweka
kwake.
“Mwenye
mamlaka ya mtoto huyo ni mama yake ambaye ametoka asubuhi kwenda
kumtafuta mtaani mimi sihusiki naye na wala sijui walichomuambia ingawa
siku zote tulipokuwa tukizungumzia kuhusu kukeketwa mtoto huyo alikuwa
akionesha hofu” alisema Wilison.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamdun alisema hakuwa na
taarifa kuhusu tukio hilo ingawa aliahidi kuwasiliana na wasaidizi wake
ili kulifuatilia na kutoa taarifa kamili.
Mtoto
huo alisema watoto wenzake waliofanyiwa vitendo hivyo bado wapo
majumbani mwao wakijiuguza majeraha na kama vyombo vya usalama
vitahitaji kwenda kuwaonyesha walipo yupo tayari.
Taarifa
ambazo tumezipata jana kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaoishi jirani
na nyumba aliyokuwa akiishi mtoto huyo na mama yake zimeeleza kuwa
polisi walifika katika nyumba hiyo na kumkamata Regina Wilson, mama ya
mtoto huyo Happyness na watu wengine wawili na kupelekwa kituo cha
polisi Stakishari Ukonga jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
No comments :
Post a Comment