Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed
Chande Othman amewataka Mawakili nchini kuzingatia Maadili na kufuata
misingi ya haki katika kutekeleza majukumu yao ili kesi
ziendeshwe kwa
haki, haraka na kwa wakati ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.
Akizungumza wakati wa sherehe za
kuwapokea na kuwaapisha Mawakili leo katika viwanja vya Karimjee jijini
Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema endapo Mawakili watatekeleza wajibu wao
kwa kutenda haki watasaidia kupunguza mlundikano wa kesi zilizopo
kwenye Mahakama mbalimbali nchini kuanzisha zile za Wilaya mpaka
mahakama ya Rufani.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka
Mawakili kushirikiana Mahakama pamoja na wadau wengine katika
kuutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambao
pamoja na mambo mengine pia unalenga kupunguza mlundikano wa kesi
kwenye mahakama mbalimbali nchini.
Mhe. Othman pia amewashauri
Mawakili walioapishwa leo kujiendeleza kielimu ili waweze kuongeza ujuzi
utakaowasaidia kupambana na changamoto mbalimbali za kitaaluma na
kwenda na wakati.
Amewataka Mawakili hao kusambaa na
kufanya kazi mikoani ili na raia walioko huko nao wapate haki badala ya
wengi wao kung’ang’ania kwenye miji mikubwa pekee kama vile Dar es
salaam, Arusha, na Mwanza.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Mhe. Fednand Wambali amesema suala la ushiriki wa dhati
katika utoaji wa haki nchini limesisitizwa kwa Mawakili walioapishwa
leo.
Mhe. Wambali pia amewataka
Mawakili hao kuwa waaminifu kwa Mahakama ya Tanzania na kwa wateja wao
ambao n iwananchi wanaotafuta haki zao.Aliongeza kuwa bila ya Mawakili
hao kuwa na maadili hawataweza kufanya kazi.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. George Masaju amewataka Mawakili hao wapya kufanya kazi zao kwa
kufuata maadili ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Alisema kupitia kamati ya
malalamiko, amepokea malalamiko 71 kati ya mwaka 2015 na 2016
yaliyowahusu Mawakili kukiuka taratibu na misingi ya kazi yao.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, baadhi ya malalamiko yalihusu Mawakili kutokuwatetea wateja
wao ipasavyo, kufanya kazi ya uwakili bila ya kulipia kibali, na kutoa
siri za wateja wao.
Jaji Mkuu wa Tanzania amewakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 285 na kuifanya Tanzania kuwa na Mawakili zaidi ya 6080.
Sherehe za kuwakubali na
kuwaapisha Mawakili hao zimefanyika kwa mara ya 55 tangu kuanzishwa kwa
sherehe hizo mwaka 1986 hapa nchini.
No comments :
Post a Comment