Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Kampuni moja ya Ujerumani ya
Ferrostaal, inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika wilaya
ya Kilwa mkoani Lindi, kitakacho gharimu zaidi ya Euro Bilioni 1 nukta 2
(1.2bln) ambacho kinatajwa kuwa kitakuwa moja ya viwanda vikubwa vya
mbolea Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Balozi wa
Ujerumani hapa nchini, EGON KOCHANKE, wakati alipomtembelea na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Jijini Dar
es salaam, ambapo wawili hao wamezungumzia masuala kadha wa kadha
yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani uliodumu kwa muda
mrefu.
Balozi Kochanke amesema kuwa
kiwanda hicho kitakachojengwa kwa ubia kati ya kampuni hiyo ya Ujerumani
na wawekezaji wazawa na wengine kutoka Bara la Asia, inatokana na
hamasa kubwa ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John
Pombe Magufuli katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda.
“Kiwanda hiki kitakuwa kikubwa
zaidi ya mara mbili ya kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mtwara
na kitagharimu Euro Bilioni 1.2, kitasisimua uchumi wa nchi pamoja na
kukuza ajira” alisema balozi huyo aliyeambatana na naibu Balozi wa
Ujerumani hapa nchini, John Reyels na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa nchi
hiyo Julia Hannig.
“Mbali ya Kampuni hiyo ya
Ferrostaal, wawekezaji wengine ni kampuni ya Mbolea ya Minjingu, na
kampuni nyingine kutoka Pakistan ambayo kwa pamoja wameingia ubia wa
kujenga kiwanda hicho cha mbolea kitakachokuwa uwekezaji mkubwa”
Aliongeza Balozi Egon Kochanke.
Egon Kochanke, ameiomba serikali
kutatua changamoto ya gharama za gesi ili kiwanda hicho kiweze kuanza
ujenzi wake mapema iwezekanavyo na kuchochea maendeleo ya kilimo hapa
nchini.
Ameyataja maeneo mengine ambayo
nchi yake itaelekeza rasilimali zake kuwa ni kuendeleza sekta ya afya,
wajasiriamali wadogowadogo, sekta ya ufundi mchundo pamoja na
kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja kuwekeza viwanda na
biashara mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Balozi huyo wa Ujerumani
ameahidi kuwa nchi yake iko tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili
kuifanyia ukarabati meli ya MV Liemba, inayofanya zafari zake katika
ziwa Tanganyika, ambayo ni meli ya kihistoria kwa kuwa na umri wa zaidi
ya miaka 100, ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa watanzania na nchi
jirani za Zambia, Burundi na DRC Kongo.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Ujerumani kwa ushirikiano
mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na kwamba Tanzania iko tayari
kuendeleza ushirikiano huo.
Amesema kuwa uwekezaji wa kiwanda
kikubwa na cha mfano cha mbolea huko mkoani Lindi, utachochea sekta ya
kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watanzania, kwa kuongeza
tija ya uzalishaji wa mazao ya wakulima na mbolea ya ziada itauzwa nchi
za nje.
Dkt. Mpango, amemshukuru Balozi
huyo wa Ujerumani kwa ahadi yake ya kusaidia kukarabati meli ya MV
Liemba, na kiomba nchi hiyo kusaidia ununuzi wa meli mpya ili kuimarisha
usafiri na usafirisha wa watu na mizigo katika eneo la maziwa makuu.
Vilevile ameiomba nchi hiyo
kuendeleza misaada yake katika sekta ya ufundi kupitia mamlaka ya Ufundi
Stadi (Veta) pamoja na kuendelea kutoa ufadhili wa masomo ya juu kwa
wanafunzi wa kitanzania kwenda kusoma nchini humo kama ambavyo imekuwa
ikifanya miaka mingi iliyopita kupitia Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Balozi Kochanke amekubali kufanya
hivyo na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania
katika mambo hayo na masuala mengine, ikiwemo kuishauri namna bora ya
kuhamishia Serikali mkoani Dodoma, wakitumia uzoefu wa nchi hiyo
ilipohamisha makao makuu yake kutoka Berlin kwenda Born.
No comments :
Post a Comment