Na Lydia Churi-Mahakama, Mbeya
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania
wametakiwa kufuata maadili ya kazi, kwa kuongeza nidhamu na kutoa huduma
bora kwa wananchi wanaofika kutafuta haki katika mahakama mbalimbali
nchini ili kuongeza imani ya juu ya utendaji wa mahakama.
Akizungumza na watumishi wa ngazi zote wa
Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman amesema Mahakama ni chombo kinachotoa huduma hivyo watumishi hao
hawana budi kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndiyo wateja wao.
Aliwataka watumishi hao kushughulikia
malalamiko ya wananchi yanayoletwa mahakamani na kuyapatia ufumbuzi ili
kuzimaliza kero na hoja mbalimbali zinazoelekezwa kwenye taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa pamoja na watumishi kutoa huduma bora, mahakama itahakikisha inaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi hao.
Alisema Mahakama ya Tanzania inafanya
maboresho ya huduma zake ambapo tayari imeanza kukarabati majengo yaliyo
katika hali mbaya na kujenga majengo mapya hasa ya mahakama za Mwanzo
na wilaya ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wa kada
mbalimbali.
Kwa mujibu wa Sheria, kila wilaya inapaswa
kuwa na mahakama ya wilaya. Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, zipo 960
tu wakati mahitaji ni kuwa na mahakama za mwanzo katika kila kata ambapo
kuna kata zaidi ya 3000 nchi nzima.
Jaji alisema mahakama ya Tanzania tayari
imeanza ujenzi wa mahakama za mfano kumi za wilaya zinazojengwa kwa
kutumia teknolojia rahisi, ya muda mfupi na yenye gharama nafuu.
Mahakama hizo ziko mbioni kukamilika.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda
ya Mbeya Mhe. Noel Chocha alisema kasi ya upunguzaji wa mlundikano wa
mashauri katika Mahakama za Mwanzo zilizoko kanda ya Mbeya ni nzuri kwa
kuwa mashauri yaliyobaki mahakamani ni 670 tu yenye umri wa siku moja
mpaka miezi sita mahakamani. Jumla ya mashauri 12,448 yamemalizika
katika mahakama za Mwanzo.
Alisema changamoto katika kanda yake
ni ufinyu wa fedha inayotengwa kwa ajili ya kuendesha mashauri hali
inayoweza kudumaza mfumo wa wa utoaji haki katika kanda yake.
Alisema hadi sasa, Mahakama Kuu kanda
ya Mbeya inayo mashauri 177 ya madai, 398 yanayohusu migogoro ya Ardhi
na 394 ni mashauri ya jinai.
Jaji Mkuu wa Tanzania leo amehitimisha
ziara ya siku mbili kwa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga pamoja na kanda
ya Mbeya ambapo alikagua shughuli za Mahakama kwenye kanda hizo.
No comments :
Post a Comment