Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza kabla ya kuzindua Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme
jijini Dar es salaam kwenye Kituo cha TANESCO cha Mikocheni jijini Dar
es salaam Novemba16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo akizungumza katika Uzindunduzi wa Mradi wa
Uboreshaji Miundombinu ya umeme katika jiji la Dar es salaam uliofanywa
na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kwenye Kituo cha TANESCO cha Mikocheni
jijini Dar es salaam Novemba 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto kwake)
wakitazama mfumo wa usambazaji umeme kabla ya Waziri Mkuu kuzindua
Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme jijini Dar es salaam kwenye
Kituo cha TANESCO cha Mikocheni jijini Dar es salaam Novemba 16,
2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam watumie fursa ya uwepo wa
umeme wa uhakika kwa kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili waweze
kujiongzea kipato.
Ametoa wito huo leo (Jumatano,
Novemba 16, 2016) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali
waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme
jijini Dar es Salaam uliofanyika kwenye Ofisi za TANESCO zilizoko
Mikocheni jijini humo.
Akizungumza kabla ya kubonyeza
kitufe kuashiria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema: “Umeme ni
mhimili mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile. Tumepata umeme wa
uhakika, tumieni fursa hii ya uwepo wa umeme wa uhakika kujiongezea
kipato.”
“Hivi sasa tumepata umeme wa
uhakika, fanyeni kazi kwa bidii ili mfaidi matunda ya kuwepo kwa umeme
huo. Serikali inategemea kwamba sasa wananchi mtaanzisha na kukuza
viwanda vidogo vidogo na vikubwa, biashara zitapanuka na kilimo bora
huko vijijini kitaongezeka,” amesema.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda na moja ya nyenzo kuu ya
kuendesha uchumi wa viwanda kwa tija na ufanisi ni upatikanaji wa
nishati ya umeme ya uhakika, na ndiyo maana kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha miundombinu
ya umeme inaboreshwa ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme.
“Wataalam wamenieleza kuwa mradi
huu ulihusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha kupozea umeme cha MVA 100,
ujenzi wa njia za usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 132 katika
maeneo mbalimbali ya Jiji kupitia chini ya ardhi, ujenzi wa njia za
usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 33, pamoja na ujenzi wa ujenzi
kituo cha udhibiti mifumo ya usambazaji umeme (Distribution SCADA
System) katika msongo wa kilovoti 33 na 11.”
“Kukamilika kwa mradi huu
kunaondoa adha zilizokuwepo awali kutokana na kukatika umeme mara kwa
mara. Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli za biashara katika
kuleta maendeleo ya Taifa ambapo upatikanaji wa umeme wa uhakika ni wa
lazima,” ameongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof.
Sospeter Muhongo amesema Wakala wa Jiolojia Tanzania kwa kushirikiana na
Wakala wa Jiolojia wa Finland wanaunda mpango wa pamoja wa kuibua
madini ya kisasa ambayo yanatafutwa zaidi duniani kukidhi mahitaji ya
kiteknolojia.
“Hivi sasa madini kama graphite
na lithium yanahitajika zaidi kwenye teknolojia za kisasa kama za
utengenezaji wa simu, tuachane na madini yaliyozoeleka kama vile dhahabu
na Tanzanite,” alisisitiza.
Alitumia fursa kuuagiza uongozi
wa TANESCO uhakikishe kuwa hakuna mgao wa umeme nchi nzima kwani
Watanzania wamechoshwa na tabia ya kukatiwa umeme mara kwa mara. “Ili
tujenge nchi ya viwanda, tunahitaji umeme wa uhakika, umeme unaotabirika
na zaidi ya yote umeme wa bei nafuu,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Waziri wa Biashara za Nje na
Maendeleo wa Finland, Bw. Kai Mykkanen alisema Serikali yake imedhamini
ujenzi wa mradi huo kwa vile inaamini kuwa umeme wa uhakika ni
suluhisho la kuondoa umaskini kwa hiyo kukamilika kwa mradi huo
kutaondoa adha ya kukatika umeme kila mara.
Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika eneo la nishati ya umeme na nishati mbadala.
Katika hatua nyingine,
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Eng. Felchesmi Mramba alisema ujenzi wa
mradi huo umegahirimu sh. bilioni 74.6 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni
63.56 zimetolewa na Serikali ya Finland na sh. bilioni 11.03 zimetolewa
na Serikali ya Tanzania.
Alisema kukamilika kwa mradi huo
kumewezesha sehemu kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na njia za
mzunguko (ring circuit) zinaoingizaa umeme. “Teknolojia hii iliyotumika
itawezesha vituo vya kupozea umeme kuwa na njia mbadala ya kupata umeme
endapo njia mojawapo inayopeleka umeme itapata hitilafu,” alisema.
Naye Meneja wa Kituo cha
Kudhibiti Mifumo ya Usambazaji, Eng. Alex Kalanje alimweleza Waziri Mkuu
kwamba kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kompyta, (distribution SCADA
SYSTEM) kituo hicho cha udhibiti wa mifumo ya usambazaji umeme katika
jiji la Dar es Salaam kitawasaidia watoa huduma wao waweze kufuatilia
kwa haraka zaidi pale matatizo yanapotokea.
“Baada ya kukamilika kwa kituo
hiki, lengo letu ni kujenga kituo kama hiki kwenye mjai ya Arusha,
Mbeya, Dodoma na Mwanza,” alisema.
No comments :
Post a Comment