Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Ujenzi wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC)
Fredy Msemwa (katikati), akitoa taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki (kushoto), kuhusu mradi
wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Umma zinazojengwa Gezaulole
Kigamboni jijini Dar es Salaam. Waziri Kairuki alikuwa katika ziara ya
siku moja kutembelea miradi ya ujenzi ya Taasisi hiyo iliyopo Dar es
Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud Msangi.
Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud Msangi akitoa taarifa kwa
Waziri Kairuki.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki
(kushoto), akizungumza na watendaji wa mradi huo. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Ujenzi wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC)
Fredy Msemwa (kushoto), akimuelekeza Waziri Kairuki jinsi ujenzi wa
magorofa unavyoendelea katika mradi huo wa Gezaulole. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud
Msangi na Kaimu Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Robert Wambura.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki
(katikati), akikagua nyumba zinazojengwa na Taasisi ya Ujenzi wa Nyumba
za Watumishi wa Umma (WHC) katika mradi ya Gezaulole Kigamboni Dar es
Salaam leo asubuhi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa WHC, Fredy Msemwa na
kulia kwake ni Mjumbe wa Bodi ya WHC, Agnes Meena.
Waziri Kairuki (kushoto), akimuelekeza jambo Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Robert Wambura wakati wa ziara hiyo.
Wafanyakazi wa WHC, wakijadiliana jambo kwenye ziara hiyo.
Ukaguzi wa mradi huo ukiendelea.
Msanifu
Majengo kutoka Onspace Consult. Co.Ltd, Edmund Kahabuka (kulia), akitoa
taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa Magomeni kwa Waziri Kairuki.
Mwonekano wa ujenzi wa magorofa yanayo jengwa katika mradi huo wa Gezaulole Kigamboni.
Mwonekano wa nyumba za chini zinazojengwa katika mradi huo.
Mwonekano wa jengo la ghorofa la mradi huo baada ya kukamilika ujenzi wake.
Na Dotto Mwaibale
WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki
amewataka watumishi wa Umma kuchangamkia nyumba za bei nafuu
zinazojengwa na Serikali ili kuondokana na changamoto ya makazi.
Katika
hatua nyingine Kairuki ameiagiza Taasisi ya Ujenzi wa Nyumba za
Watumishi wa Umma (WHC), kuzingatia ujenzi utakaokidhi mahitaji ya
watumishi wenye mishahara ya kima cha chini wakiwemo walinzi, wahudumu,
madereva na makatibu muhtasi.
Kairuki
aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipofanya ziara kwenye mradi wa
nyumba za WHC, zilizopo Kigamboni, Magomeni na Bunju jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kuangalia ujenzi unavyoendelea.
Alisema
asilimia 80 ya watumishi wa serikali wana mishahara midogo hivyo endapo
nyumba hizo zitauzwa kwa gharama kubwa hawataweza kuzinunua, na azma ya
serikali ni kuwa na nyumba bora zenye gharama nafuu kwa watumishi wake.
“Kwa
asilimia 80 ya watumishi wa umma kiwango watakachoweza kumudu kununua
nyumba hizo hakiwezi kuzidi sh. milioni 20 kwa miaka 18, Tujitahidi
kupunguza gharama kwa kadiri inavyowezekana ili kutoa fursa kwa
watumishi wa umma wa kipato cha chini kuweza kupata nyumba za bei nafuu
za kuishi” alisema.
Waziri
huyo alisema azma ya serikali ni kuhakikisha wanaboresha na kujenga
nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma ambazo zinatakiwa ziwe sio chini
ya nyumba 10,000.
Aliwataka
WHC, kuwa na mpango mkakati wa kuweza kujenga nyumba zaidi ya 10,000
kwa mwaka ili kuwafikia watumishi wengi zaidi hasa waliopo vijijini.
Alisema
katika manunuzi ya nyumba hizo serikali inaangalia jinsi ya kupunguza
kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ili kumpunguzia mtumishi gharama.
Nyumba
hizo zinazojengwa kwa mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na
Pensheni zitauzwa kulingana na ukubwa wa nyumba husika kwani ile ya
chumba kimoja itauzwa kwa sh.milioni 35, vyumba viwili milioni 75 na
vyumba vitatu itauzwa sh.milioni 91.
Mkurugenzi
Mtendaji wa WHC, Fredy Msemwa alisema katika eneo la Kigamboni lenye
ekari 24 wanatarajia kujenga nyumba 790, mradi unaotekelezwa kwa awamu
mbili.
Alisema
katika nyumba za awamu ya kwanza wapo katika hatua ya umaliziaji ambapo
nyumba hizo zinatarajia kukamilia Februari mwakani.
Nyumba
hizo pia zinajengwa katika maeneo mbalimbali nchini, ambazo gharama
zake ni kati ya sh. milioni 33 mpaka sh. milioni 190 pamoja na VAT.
Mwenyekiti
wa Bodi ya WHC, Daud Msangi alielezea changamoto za mradi huo kuwa
waliomba nyumba hizo zisiwe na vat, kupata viwanja bure na vya bei
rahisi pamoja na serikali kuangalia huduma za maji, umeme na barabara.
Nyumba
nyingine zimeanza kujengwa katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Dodoma,
Mtwara, Lindi, Mbeya, Shinyanga, Singida na Arusha huku katika baadhi ya
mikoa hiyo kukiwa na viwanja vya ujenzi huo.
No comments :
Post a Comment