Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi kutoka TRA Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu semina kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa china
itakayofanyika tarehe 25 Novemba 2016, leo jijini Dar es Salaam.Katikati
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jiteng Consultancy Limited Bw.
Andrew Huong na Meneja Msaidizi wa Kampuni hiyo Bw. Wesley Huung
(kushoto).
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi kutoka TRA Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu semina kwa jumuiya ya
wafanyabiashara wa Kichina itakayofanyika tarehe 25 Novemba 2016.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakifuatilia mkutano uliowakutanisha wadau kutoka TRA na Jumuiya ya
wafanyabiashara wa China leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
ya Jiteng Consultancy Limited Bw. Andrew Huong (katikati) akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu semina kuhusu elimu ya mlipa kodi na
uwekezaji ikatakyofanyika tarehe 25 Novemba 2016 katika ukumbi wa BOT
jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa
Kodi kutoka TRA Richard Kayombo na Meneja Msaidizi wa kampuni hiyo
Wesley Huung.Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO.
…………………………………………………………………
Na. Lilian Lundo – MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kwa kushirikiana na Ubalozi wa China hapa nchini imeandaa warsha kwa
Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China kuhusu mambo ya kodi na uwekezaji.
Hayo yamesemwa leo, Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi kutoka TRA Bw.
Richard Kayombo alipokuwa akiongea na vyombo vya habari juu ya warsha ya
kutoa elimu ya mambo ya kodi na uwekezaji kwa wafanyabiashara hao wa
Kichina.
Kayombo amesema kuwa warsha hiyo
itafanyika Ijumaa Novemba 25, 2016 katika ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) Jijini Dar es Salaam ambapo lengo kuu la warsha hiyo ni
kuwawezesha wafanyabiashara hao wa Kichina kuzingatia na kuzitumia
sheria za kutoza kodi sahihi pamoja na kukokotoa kodi ya zuio katika
bidhaa na huduma na hivyo kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari miongoni
mwao.
“Mada zitakazowasilishwa ni
pamoja na mabadiliko ya bajeti 2016/17, masuala ya forodha na uondoshaji
wa bidhaa, kodi ya zuio hususani katika sekta ya ujenzi pamoja na kodi
ya ajira,” alifafanua Bw. Kayombo.
Aliendelea kwa kusema kuwa,
wafanyabiashara hao watapata fursa ya kuuliza maswali na kupata
ufafanuzi wa masuuala mbalimbali ili kuwawezesha kufanya shughuli zao
kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Aidha mada hizo zimeandaliwa kwa
kuzingatia umuhimu wa kuongeza uelewa miongoni mwa Jumuiya ya
Wafanyabiashara wa China na kuzingatia matakwa ya sheria.
Kwa upande wake, Mratibu wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kichina Tanzania, Andrew Huang amesema
kuwa warsha hiyo itawasaidia wafanyabiashara wa Kichina kufanya biashara
kwa kufuata sheria za kodi za Tanzania kutokana na wengi wao kutokuwa
na elimu hiyo.
Waziri wa Biashara na Viwanda
Charles Mwijage anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa warsha hiyo ambayo pia
itahudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini.
No comments :
Post a Comment