Tuesday, November 15, 2016

PSPF na utekelezaji wa ahadi za Rais Magufuli



Dkt John Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Na Christian Gaya

Katika kipindi cha mwaka mmoja cha utawala wa Rais Magufuli nchini, Mfuko wa Pensheni PSPF kwa upande wake umesaidia Watanzania wanaopata huduma za hifadhi ya jamii kupitia PSPF kuongezeka kutoka 394,494 hadi kufikia 444,679 ikiwa ni sehemu ya utekeleza wa agizo la Rais.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSPF meneja uhusiano na masoko  wa mfuko huo, Costantina Martin anasema hatua hii ya PSPF imelenga kutekeza agizo na kutimiza ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyokuwa akitoa ya kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanufaika na huduma za hifadhi za jamii ikiwemo huduma za bima za afya wakati wa kampeni na baada ya kuingia madarakani.
Akitoa taarifa ya mwaka mmoja kwa upande wa Mfuko wa PSPF Costantina Martin  anasema idadi hii inajumuisha Watanzania walio katika sekta rasmi na isiyo rasmi nchini.
“Kundi hili kubwa lilikuwa limesaulika kujumuishwa katika hifadhi ya jamii, lakini baada ya Mhe. Rais Magufuli kulizungumzia katika kampeni zake hivi sasa mwamko wa kujiunga na hifadhi ya jamii umeongezeka na PSPF tumeanza kulitekeleza agizo hili kwa kuwahamasisha wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi na sekta rasmi kuchangia na kujiunga katika Bima ya Afya”anasema  Martin.
Anafafanua ya kuwa katika kuhakikisha kuwa azma hiyo inatimizwa tayari PSPF imeingia makubaliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kufikisha huduma za afya kwa watanzania wengi ambao wapo katika sekta isyo rasmi na hivyo kujenga jamii yenye afya bora inayochangia katika ujenzi wa nchi.
“Chini ya makubaliano yanawasaidia wanachama wa PSPF walio katika Mpango wa Uchangiaji wa Hiari kuweza kupata tiba kupitia NHIF kwa gharama ya shilingi 76,800/- kwa mwaka katika hospitali mbalimbali ziliingia makubaliano na Mfuko huo wa Bima ya Afya” Costantina anatamka.
Anasema ya kuwa mpango huo wa PSPF unaounga mkono juhudi za Rais Magufuli  za kutaka kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata huduma na matibabu nchi nzima kwenye vituo vyote vilivyosajiliwa na NHIF kuanzia Zahanati hadi Hospitali ya Taifa kwa gharama nafuu.
Hivi sasa huduma hiyo ya PSPF kuwadhamini wananchama wake kwa ajili ya kupata matibabu imesaidia watanzania wengi sana kunufaika na huduma hii husasan katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Magufuli.
Akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Magufuli alisema kuwa dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umaskini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora.
Rais alitamka ya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kuhamasisha wananchi wengi wanajiunga na Bima ya Afya.
“Katika kutekeleza hilo PSPF kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imeshawafikia Watanzania 2,710 walio katika sekta isiyo rasmi kuanza kunufaika na huduma za Afya kupitia PSPF” anataja Costantina.
Anafafanua zaidi kwa kusema ya kuwa mbali na sekta ya afya, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Magufuli PSPF kwa upande wake imesaidia kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa Nchi ya Viwanda kwa lengo la kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi.
Anasema viwanda hivyo ambavyo PSPF imewekeza ni pamoja na 21st Century cha Morogoro, Saruji Tanga. Na anaongeza ya kuwa hivi sasa PSPF imejipanga kuwekeza katika Kituo cha Biashara cha Kurasini (Kurasini Logistic Center) kwa lengo la kuchochea uwekezaji wa viwanda na kutoa ajira kwa wananchi.
“Viwanda vingine ambavyo PSPF imejipanga kuwekeza ni kile cha Nguo cha Urafiki, Morogoro Canvas Mill na Kiwanda cha Viatu Karanga kilichopo Moshi”, anaendelea kutaja.
Anasema ya kuwa hatua hiyo iliyoanza kutekelezwa na PSPF ni sehemu utekelezaji hotuba ya Mhe. Rais Magufuli wakati anafungua rasmi Bunge 11 mjini Dodoma mwishoni mwa mwaka jana ambapo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo katika ujenzi wa viwanda ili mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40 ya ajira zote hapa nchini.
Anaongeza ya kuwa wajasiliamali wadogo wadogo ambao kwa kuwekeza katika afya kutawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla
“Kwa kutoa kinga ya huduma ya bima ya afya kwa wanachama wetu na familia zao sisi kama PSPF tunatambua kwamba wananchi walio na afya bora ni nguvukazi na raslimali kubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini” Costantina anafafanua.
Kwa kutoa mafao ya huduma ya bima ya afya PSPF itaisaidia serikali katika kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko na wanaofanya kazi kwenye sehemu hatari zaidi, kwa kutoa mafao ya huduma za afya PSPF itachangia serikali katika kukidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.
Anasema huduma hii ya bima ya afya kwa wateja wetu  itakuwa na fursa nyingine kwetu ya kutekeleza lengo letu la kuwafikia Watanzania wengi zaidi walioko kwenye sekta isiyo rasmi na kufungua milango kwa kundi kubwa la Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa na uhakika wa matibabu kwa kuwa hawakuwa wanachama wa PSPF.
“Lengo kubwa ni kumjengea uwezo mjasiliamali mdogo awekeze kwa ajili ya afya yake huku akiendelea na shughuli nyingine za kujitafutia kipato” Costantina anaongeza.

PSPF ilianzishwa kwa sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 199 . Sura ya 371 na inatoa huduma za Hifadhi ya Jamii katika Mapngo wa lazima na wa hiyari. Costantina Martin anasema, wakati PSPF wamebobea katika suala la pensheni, NHIF wao wamebobea katika kutoa huduma za afya, hivyo ushirikiano wa Taasisi hizi mbili zenye uzoefu wa kuhudumia maisha ya Watanzania, umeanza kuwapa unafuu mkubwa wa maisha.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment