Thursday, November 19, 2015

SBC yapunguza bei ya vinywaji vyake kutoka shillingi mia sita (600) hadi mia tano (500)


Na Beatrice Lyimo-Maelezo
index                                                                            Dar es Salaam.
Kampuni ya SBC Tanzania Limited, watengenezaji na wasambazaji wa vinywaji baridi imepunguza bei ya vinywaji vyake kutoka shillingi mia sita (600) hadi mia tano (500) kwa chupa yenye ujazo wa Mililita 350 na 300.
Hayo yamesemwa na Meneja Mafunzo na Uwezeshaji Bw.Rashid Chenja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa lengo la kupunguza bei ni kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyopo.
“Imekuwa vigumu kwa mnywaji kuweza kudumu bei ya kinywaji akipendacho cha pepsi , gharama za maisha zinapanda kila mwaka na soda imekuwa ghali kiasi cha wananchi wa kawaida kushindwa kumudu kununua soda hivyo kampuni imeamua kupunguza bei” alifafanua Meneja huyo.
Pia amesema kuwa kampuni ya SBC Tanzania imefanya punguzo hilo  kuanzia tarehe 16/11/2015 kwa vinywaji vya Pepsi, Mirinda,7up, Mountain Dew na Evervess na maeneo yatakayo husika na punguzo hilo la bei ni Dar es salaam,Morogoro, Dodoma, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara na Zanzibar.
“Ni matumaini yetu mtaendelea kutuunga mkono katika biashara yetu kwa kununua soda zetu kwa bei iliyopendekezwa ya shilingi Mia Tano kwa chupa, shilingi elfu tisa mia nne (9,400) kwa kreti moja na faida kwa wauzaji wa rejareja itakuwa ni shilingi 2500 kwa kila kreti” aliongeza Bw. Chenja. 
Mbali na hayo Kampuni ya SBC Tanzania Limited inawashukuru wateja wake kwa kuwaunga mkono katika biashara yao kwa kipindi cha miaka 14 hapa nchini.

CHAMA CHA ADC CHAFUTA VIKOSI VYAKE VYA ULINZI NA USALAMA

index
Na Magreth Kinabo- MAELEZO
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imeviasa vyama vingine vya siasa kuiga mfano wa Chama  cha Alliance  For Democratic Change(ADC- Dira  ya Mabadiliko) kutokana na juhudi zake za kutii sheria bila shuruti kutokana na  kuvunja vikosi vya ulinzi na usalama.
 Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Sisty Nyahonza wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dares Salaam jinsi chama hicho kilivyotekeleza Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258  kifungu cha 9(C) ambayo hairuhusu chama chochote cha siasa kutumia nguvu ili kufikia malengo yake, kwa kutumia vikosi hivyo.
 Naibu Msajili huyo alisema  chama hicho kimefuta Idara ya  Ulinzi na Usalama kijulikanacho  kwa jina la Star Guards kwa mujibu wa barua yao iliyowasilishwa katika ofisi hiyo.
Alisema kwa mujibu wa barua ya chama hicho, iliyosainiwa na  Katibu Mkuu Taifa, Lydia Bendera, Novemba 13, mwaka 2015,  yenye kumbukumbu namba ADC /HQ/GEN/VO1.1/81/15,ambayo ilieleza kwamba kutokana na kikao cha Baraza la Vyama Vya Siasa kilichofanyika Aprili 22,mwaka huu ambacho agenda kuu ilikuwa ni kujadili suala la vyama vya siasa kuwa na vikundi hivyo ni ukiukwaji wa sheria za nchi, na kufikiwa maamuzi yake kuwa;
1.     Vyama vya siasa havina budi kuheshimu sheria za nchi, na kutakiwa kuvunja vikundi vya ulinzi na usalama vilivyoko katika vyama vya siasa.
2.     Vyama vya siasa  vinatakiwa kuondoa  katika Katiba za vyama vifungu,ibara zinazoruhusu kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama.
Alisema barua hiyo ambayo iliendelea kufafanua kwamba  “kwa kuzingatia maazimio yaliyofikiwa kati ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini yaliyofikiwa na vyama, chama chetu kimekwisha chukua hatua ya utekelezaji wa maazimio ya baraza la vyama, na yale yote uliyoyaelekeza kupitia barua yako yenye kumb. namba HA.322/362/20/22  ya tarehe 16/06/2015.
“ Kupitia barua hii ninakujulisha rasmi kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa mamlaka aliyopewa na kanuni za chama chetu , ametengua uteuzi wa Mhe. Omari Albert Constantino kuwa mkuu wa idara ya STAR GUARDs,” ilieleza barua hiyo.
Naibu Msajili huyo alisema chama hicho “kimetii sheria ya nchi na  hii iwe chachu kwa vyama vingine kwa kuwa kutuii sheria ni kipaumbele cha demokrasia,” alisema Nyahonza.
 Aliongeza kwamba demokrasia ina vitu vitatu ambavyo ni utii wa sheria, amani na utulivu, hivyo ili demokrasia ifanye kazi lazima kuwe na vitu hivyo.
Aidha Nyahonza alisema Ibara ya 107 ya Katiba ya Nchi inaruhusu Serikali pekee kuanzisha vikosi hivyo.
Akizungumzia kuhusu kwa chama kitakachokiuka agizo hilo, kitachukulia hatua gani alisema kufanya hivyo ni kosa la jinai.
“Sisi tunafanya kazi na jeshi la polisi, ukikataa kufanya hivyo  utakamatwa na utalazimishwa kutii sheria,” alisisitiza.

BALOZI WA UINGEREZA NCHINI AONGOZA UZINDUZI WA FILAMU YA KUPINGA UKEKETAJI YA SIMULIZI HALISI YA GHATI NA RHOBI

 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE, wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Filamu ya Simulizi halisi ya Ghati na Rhobi ulifanyika nyumbani kwa balozi huyo, Oysterbay Dar es Salaam jana.
 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose (kulia), akizungumza kabla ya uzinduzi wa filamu hiyo.
 Mwakilishi kutoka taasisi ya DFID, Jane Miller OBE (kushoto), akizungumza katika uzinduzi huo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi (kulia), akizungumza katika uzinduzi huo.
 Wadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Sehemu ya filamu hiyo inavyoonekana.
 Sehemu ya filamu hiyo inavyoonekana.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE (katikati), akichangia jambo katika uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti (kulia), akielezea kuhusu filamu hiyo na changamoto mbalimbali za ukeketaji nchini.
……………………………………………………………………………………
Na Dotto Mwaibale
 
LICHA ya MKOA wa Dar es Salaam kuwa na watu wenye uelewa mkubwa lakini unaongoza kwa asilimia 38 ya ukeketaji imeelezwa.
 
Hayo yalibanishwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Wizara ya Wanawake na Watoto, Margaret Mussai Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Filamu ya Simulizi halisi ya Ghati na Rhobi uliofanyika nyumbani kwa Balozi wa Uingereza hapa nchini.
 
“Hali ya ukeketaji hapa nchini bado ni changamoto kubwa kutokana na jamii kutokuwa na uelewa mkubwa ikiwa ni pamoja na mila za baadhi ya makabila” alisema Mussai.
 
Alisema suala la ukeketaji limekuwa na changamoto kubwa kwa sababu ya wahusika wanaofanya ukeketaji wanatengeneza fedha na kwa msichana anayefanyiwa kitendo hicho anaonekana kuwa na thamani kuliko yule ambaye hajakeketwa.
 
Alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam kuna maeneo ambayo yanaongoza kwa ukeketaji na wasichana hupenda kufanyiwa hivyo ili waonekane wenye heshima.
 
Alisema mkoa wa Dar es Salaam una asilimia 38 ya ukeketaji, Mara asilimia 58, Shinyanga asilimia 55 huku ikifuatia mikoa mingine.
 
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose filamu hiyo inawahusu wasichana wawili ambao wanapinga ukeketaji katika jamii yao.
 
Alisema wasichana hao waqnaonesha ujasiri wa kukataa kitendo hicho chenye maumivu makali na kwa msaada wanafanikiwa kubadisha jinsi jamii yao inavyomchukulia msichana katika kipindi chake cha mpito kutoka usichana hadi kwenda kufikia utu uzima.
 
“Filamu hii inaonesha kwamba si jamii zote ndani ya Tanzania zinazojihusisha na ukeketaji na kwamba maeneo mengi wameamua kuachana na ukeketaji na kuamini kwamba ukeketaji unawezwa kutokomezwa” alisema Melrose.
 
Alisema mtoto wa kike ana haki ya kusomeshwa na kuendelezwa badala ya kuachwa nyumbani na kufanyiwa vitendo hivyo vinavyodumaza jamii kimaendeleo.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti alisema changamoto kubwa ni sheria ya makosa ya ukeketaji kuto kuwa na meno kwani ni mtu mmoja tu aliyehukumiwa kati ya watu 43 waliobainika na makosa hayo.  
 
Filamu hiyo imeandaliwa na ubalozi huo kwa kushirikiana na Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward)
 




Stanslaus Mabula alitaka Tamasha la Kushukuru

1 (4)
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE  wa Nyamagana Stanslaus Mabula ameiomba Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Kushukuru linalotarajia kufanyika Desemba 25 kwewnye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, lihamie jijini Mwanza kwa lengo la kufikisha shukrani kwa Mungu baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, Alex Msama wanayafanyia kazi mapendekezo ya Mabula ili kufanikisha tamasha hilo adhimu lenye nia ya kushukuru Mungu baada ya uchaguzi Mkuu.
Msama alisema tamasha hilo litashirikisha waimbaji mbalimbali wa muziki wa Injili ambao watawasilisha ujumbe wa neno la Mungu kwa jamii baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika kwa amani na utulivu.
Msama alisema Kamati yake inajipanga kufikisha ujumbe wa Shukrani kwa Mungu kupitia viongozi wa dini wakiwemo maaskofu na wachungaji wa makanisa mbalimbali hapa nchini.
“Tamasha la Kushukuru Mungu lina mtazamo wa kufikisha asante kwa Mungu baada ya kuendelea kudumisha tunu ya amani ambayo ndio sifa ya Tanzania nje ya mipaka,” alisema Msama.
Aidha Msama alitoa wito kwa Wadhamini na wafadhili kujitokeza kwa lengo la kusaidia tamasha hilo.

MH. KASSIM MAJALIWA NDIYE WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

3-kassim majaliwa
Hatimaye kitendawili kimeteguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli baada ya kumteua Mh. Kassim Majaliwa Mbunge wa Ruangwa mkoa wa Lindi  na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi anayeshughulia elimu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitangaza jina hilo Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai amewaeleza wabunge kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa rais kuteua jina la Waziri Mkuu na kuliwasilisha bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na wabunge
Hivyo bunge litamthibitisha rasmi na kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Fullshangwe na kikosi chake chote kimatakia Mh. Waziri Mkuu Mteule  Kassim Majaliwa afya njema na mafanikio katika majukumu yake mapya.

GAPCO KUDHAMINI KILIMANJARO MARATHON KILOMITA 10 KWA WALEMAVU 2016

Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi (Wa pili kutoka kushoto) akishiriki katika uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2016 ambapo GAPCO ilitangaza kudhamini mbio za kilomita 10 kwa walemavu. Wengine kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania Oscar Shelukindo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Pamela Kikuli, Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, Alex Nkenyenge na Meneja Mawasiliano wa Tigo John Wanyancha.
Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi (Wa tatu kutoka kushoto) akishiriki katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2016 ambapo GAPCO ilitangaza kudhamini mbio za kilomita 10 kwa walemavu.
—————————————————
GAPCO, kampuni ya mafuta inayoongoza Tanzania imetangaza udhamini wake wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 kilomita 10 kwa walemavu.
Akitangaza udhamini huo jana wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo ya Kilimanjaro Marathon, Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi alisema GAPCO inaona fahari kudhamini mbio hizo za kilomita 10 kwa walemavu.
“Tumeshuhudia mbio hizi za Kilimanjaro Marathon zikikua tangu tuanze kudhamini mwaka 2011 na pia kufurahia faida wanayopata washiriki na jamii inayozunguka maeneo ambayo mbio hizi hufanyika kila mwaka. Tunayo furaha kufanya kazi na Wild Frontiers ambao ndio waandaaji wa mashindano haya,” alisema Kakwezi.
“Kama sehemu ya kusaidia jamii ambayo tunafanya biashara, GAPCO Tanzania imeamua kusaidia wanariadha ambao ni walemavu kwa kudhamini mbio ambazo wanashiriki walemavu pekee,” alisema.
Alisema udhamini wa GAPCO pia utahusisha usafiri, malazi na chakula kwa washiriki kutoka Dar es Salaam na pia zawadi za pesa kwa washindi wa mbio hizo za kilomita 10 ambazo zinafanyika pamoja na mbio nyingine za Kilimanjaro Marathon.
Kakwezi aliendelea kusema kuwa Kilimanjaro Marathon limekua tukio kubwa linalovutia washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania na hivyo limesaidia sana kutangaza vivutio vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro na pia kuwaongezea kipato wafanyabiashara wa Moshi.”.

WAZIRI MKUU KUJULIKANA LEO

nd10 
Na Tiganya Vincent – MAELEZO
……………………………………….
Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea na kikao chake  mjini Dodoma kwa Spika wa Bunge hilo Mheshimiwa Job Ndugai kuendelea kuwaapisha Wabunge waliosalia.
Wakati zoezi hilo likiendelea ,shauku kubwa ya Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kusubiri jina la atakayekuwa Waziri Mkuu.
Jina la Waziri Mkuu ajae linatarajiwa kujulikana leo na hatimaye kupigiwa kura na wabunge mara baada ya Spika kumtangaza rasmi kama mteule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.
Mara baada ya zoezi la kupitishwa kwa jina la Waziri Mkuu kupitishwa na Bunge Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atamwapisha mjini Dodoma.
Waziri Mkuu atakaye teuliwa na Mheshimiwa Rais atakuwa ni wa 11 kushika wadhifa huo tangu mwaka 1961.
Mawaziri Wakuu waliowahi kushika nafasi hiyo ni pamoja na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere( 1961-1962), Mzee Rashid Mfaume Kawawa(1962,1972-1977),Edward Moringe Sokoine(1977-1980,1983-1984), Cleopa David Msuya 1980-1983,1994-1995), Dk. Salim Ahmed Salim 1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Fredrick Sumaye(1995-2005),Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015)

No comments :

Post a Comment