Kwa ufupi
Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta
alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria
(L LB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971.
Historia yake
Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko
wilayani Urambo Mkoa wa Tabora. Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo
kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 -
1957 na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge
Middle School”. Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari
Shule ya Wavulana Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V –
VI.
Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari,
Sitta alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya
Sheria (L LB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971.
Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu
mwaka 1966, wakati yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi
UDSM, wanafunzi waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya
wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na
wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?
Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu
Julius Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi
akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi
miwili baadaye akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa
uzito malalamiko ya wanafunzi hao.
Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo
(sasa marehemu) na wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile
walichokiita haki zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu
Mwalimu Nyerere kwa maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni
kuliko utawala wa Mwalimu”.
Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo
wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani
mwao”. Miezi kumi baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira
kutulia akaamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo;
Sitta na wenzake 7 walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni.
Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu
aliliwe zaidi na kuandikiwa barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na.
C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio
hicho na kuwaruhusu vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale
watukutu wawili (Sitta na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu
Nyerere” mwenyewe. Hii ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM
na kuendelea na masomo kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.
Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa
mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967
– 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la
Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala.
Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza
kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha
IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976.
Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta amekuwa
kiongozi wa juu wa CCM na serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na waziri
katika nyakati tofauti na ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo
wa vyama vingi.
Sitta amemuoa Margareth Simwanza Sitta na wana familia imara.
No comments :
Post a Comment