Friday, May 1, 2015

UCHAGUZI CCM 2015: Fredrick Sumaye Waziri Mkuu mstaafu

Fredrick Tluway Sumaye  
Kwa ufupi
Sumaye alifaulu vizuri na alichaguliwa kwa masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Ilboru alikosoma kidato cha I – IV kati ya mwaka 1966 – 1969. Baada ya kuhitimu kidato cha nne, alikwenda nchini Kenya kwenye Chuo cha Kilimo cha Egerton kusomea stashahada ya Uhandisi wa Kilimo (Agricultural Engineering) mwaka 1970– 1972.


Historia yake
Fredrick Tluway Sumaye alizaliwa Mei 29, 1950 wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara. Sumaye alianza darasa la kwanza mwaka 1958 katika shule ya Msingi Gidas iliyoko Hanang; alifika darasa la nne mwaka 1961 kisha akajiunga na Shule ya Kati “Single Middle School” mwaka 1962 hadi alipohitimu darasa la nane mwaka 1965.
Sumaye alifaulu vizuri na alichaguliwa kwa masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Ilboru alikosoma kidato cha I – IV kati ya mwaka 1966 – 1969. Baada ya kuhitimu kidato cha nne, alikwenda nchini Kenya kwenye Chuo cha Kilimo cha Egerton kusomea stashahada ya Uhandisi wa Kilimo (Agricultural Engineering) mwaka 1970– 1972.
Baada ya kuhitimu stashahada yake, alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadaye akaenda kufundisha katika Chuo cha Kilimo Nyegezi jijini Mwanza. Aliifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 1973 hadi 1976.
Mwaka 1976 – 1980 alifanya kazi katika kiwanda cha Sukari Kilombero kama mhandisi na meneja wa kitengo. Mwaka 1980 hadi 1982 alifanya kazi katika Shirika la Nishati Vijijini la CAMARTEC mkoani Arusha na wakati huohuo alijishikiza katika mradi wa “Arusha Appropriate Tech” kama mratibu wa mradi.
Katika kipindi chote hicho, Sumaye alikuwa mwana CCM kindakindaki akiendelea kujishughulisha na harakati za chama chake kokote kule ambako alikuwa.
Mwaka 2006, wakati akiwa amestaafu uwaziri mkuu, Sumaye alikwenda Marekani na kujiunga Chuo Kikuu cha Havard katika Shule ya Uongozi ya John F. Kennedy na kuhitimu shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma (Public Administration). Sumaye ameoa na ana watoto.
Mbio za ubunge
Sumaye alianza mbio za ubunge katika jimbo la Hanang mwaka 1983. Alipitishwa na CCM kugombea chini ya chama kimoja akawa mbunge. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1985, Rais Ali Hassan Mwinyi alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Ushirika wadhifa alioushika hadi mwaka 1994 alipoteuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo hadi 1995.
Siasa za vyama vingi zilipoanza mwaka 1992, Sumaye ni kati ya vigogo wa CCM walioonja “joto ya jiwe” kutokana na upinzani mkali pale Hanang, hususani kutoka NCCR-Mageuzi. Wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 1995 alikumbana na Siringi Mangi Nathael wa NCCR na Nicholaus Maro Mgare wa TLP. Nathael ndiye alisumbua sana japo alipata asilimia 21.2 (kura 6,358) huku Sumaye akipata ushindi wa asilimia 77.3 (kura 23,212).
Kwa kuwa tayari alikuwa mtu muhimu ndani ya CCM wakati huo, akitoka kuongoza wizara ya kilimo kwa mafanikio walau ya kuridhisha, Novemba 28, 1995, Rais Benjamin William Mkapa alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akivaa viatu vilivyowahi kuvaliwa na Mwalimu Julius Nyerere, Rashid Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, John Malecela na Joseph Sinde Warioba.
Sumaye alihudumu katika wadhifa huo, kwa miaka yote 10 ya uongozi wa Mkapa. Kwanza ni kuanzia 1995 – 2000 na aliposhinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 pale Hanang, aliteuliwa tena katika wadhifa huo hadi alipostaafu 2005.
1 | 2 | 3 | 4 | 5 Next Page»

No comments :

Post a Comment