Friday, May 1, 2015

UCHAGUZI CCM 2015: Anne Semamba Makinda Spika wa Bunge


Anne Semamba Makinda Spika wa Bunge  
Kwa ufupi
Baba yake alikuwa mkuu wa mkoa aliyefanya kazi katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kwa hiyo Makinda alikulia katika malezi ya watu wa daraja la kati au juu tofauti na Watanzania wengi wa wakati huo.

Historia yake
Anne Semamba Makinda alizaliwa Julai 26,1949 mkoani Njombe, zamani sehemu ya Iringa (atafikisha miaka 66, Julai mwaka huu).
Baba yake alikuwa mkuu wa mkoa aliyefanya kazi katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kwa hiyo Makinda alikulia katika malezi ya watu wa daraja la kati au juu tofauti na Watanzania wengi wa wakati huo.
Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi Uwemba iliyoko Njombe na kisha akaenda Shule ya Wasichana Peramiho kwa masomo ya kati “middle school” ambayo yalikuwa ya shule ya msingi. Hii ilikuwa mwaka 1957 - 1964.
Makinda alijiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi iliyoko mkoani Mtwara mwaka 1965 - 1968, kisha kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kilakala mkoani Morogoro mwaka 1969 - 1970. Shule hii wakati huo ikiendeshwa na masista wa kigeni kutoka shirika la Kikatoliki la Salvatory.
Wakati alipokuwa shule ya msingi, alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu na alipokuwa akisoma sekondari wilayani Masasi, alikuwa mwenyekiti wa tawi la vijana la Tanu na pia kiongozi wa wanafunzi kwa ujumla. Makinda amekuwa kiongozi tangu akiwa mtoto. Baada ya masomo yake ya Sekondari, Makinda alijiunga na Taasisi ya Maendeleo na Usimamizi ya Mzumbe (IDM) ambacho siku hiki ni Chuo Kikuu cha Mzumbe ambako alihitimu Stashahada ya juu ya Uhasibu mwaka 1971 – 1975.
Alipohitimu Mzumbe, Makinda aliajiriwa na Shirika la Ukaguzi Tanzania (TAC) na alikuwa kwenye uangalizi kabla ya kupewa mkataba wa muda mrefu ndipo alipoamua kujiunga katika siasa za kitaifa.
Pamoja na kuanza harakati za siasa, Makinda bado alijiunga katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha ya Dar Es Salaam (IFM) na kuchukua kozi ya awali ya CPA mwaka 1975 – 1976 na hadi leo yeye ni mhasibu aliyeidhinishwa na kusajiliwa kisheria.
Mbio za ubunge
Makinda ana rekodi nzito ya kisiasa nchini, huenda kuzidi wanawake wengine wengi tu. Alianza ubunge akiwa na miaka 23 tu, hii ilikuwa mwaka 1975 na alipata fursa hii kupitia kundi la vijana wa CCM na ilikuwa ni lile bunge ambalo pia kina Samwel Sitta waliingia. Makinda ndiye aliyekuwa mbunge mdogo kuliko wote.
Wakati Makinda anajiunga na siasa za kitaifa, ilimpasa kuacha kazi katika Shirika la Ukaguzi Tanzania (TAC). Aliacha mshahara ambao ulikuwa mkubwa mara kadhaa kuliko wa mbunge na kuamua kujiunga na Bunge.
Alikuwa mbunge wa kawaida kwa miaka minane kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa anasimamia masuala ya Sera na Udhibiti wa Majanga mwaka 1983 akiwa na miaka 31.
1 | 2 | 3 | 4 | 5 | 6 Next Page»

No comments :

Post a Comment