Thursday, April 3, 2014

PSPF na upanuzi wigo wa hifadhi ya jamii



M. Adam Mayingu, the incoming Director General of the Public Service Pension Fund (PSPF)

Mkurugenzi mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu
Na christian Gaya, Majira Machi 11 2014
Kufuatia kupitishwa na sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Sheria Na. 8 ya mwaka, 2008 mtu yeyote anaweza kujiunga na PSPF, ili kukidhi matakwa ya watanzania PSPF hivyo imeanzisha mpango wa uchangiaji hiari maarufu unaojulikana kama PSS kwa lengo la kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini. Hii ni kutokana na mabadiliko katika sekta ya hifadhi ya jamii ndiyo yamepelekea kuwepo na mabadiliko ya sheria ya Mfuko wa pensheni wa PSPF. Sheria ya Mfuko kwa sasa inaruhusu kusajili wanachama katika sekta zote za umma na binafsi. “Mfuko sasa una mpango wa uchangiaji wa lazima na mpango wa uchangiaji wa hiari, sasa mtu yeyote awe kwenye sekta binafsi, sekta rasmi na isiyo rasmi anaweza kujiunga na PSPF, pia hata mtanzania akiyepo nje ya nchi anaweza kujiunga na PSPF na wageni wote wanaofanya kazi nchini” Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Adamu Mayingu  anasema


Kulingana na matakwa ya sheria ya msimamizi na mdhibiti wa mifuko ya pensheni ya hifadhi (SSRA) inasistiza ya kuwa kila mtumishi aliye katika ajira rasmi anatakiwa kujiunga na Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii aupendao. Na dira ya mdhibiti na msimamizi wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamiii nchini yaani SSRA ni kuwa na wigo mpana wa hifadhi ya jamii ulio endelevu na wenye huduma bora kwa kila Mtanzania, lakini takwimu zilizotolewa mwaka 2012 zinaonesha ya kuwa ni watu milioni 1.7 tu ndio waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii wakati idadi ya watanzania wote ni milioni 44.9 hii ikiwa ni asilimia 6.5 tu ya nguvu kazi yote ya watu milioni 23.7

Hivyo ni kwamba asilimia 93.5 ya watanzania wote wanaotegemewa kuwa ni milioni 44.9 hawana pensheni ya hifadhi ya jamii. Kwa kweli hata hao ambao wanahudumiwa na hifadhi ya jamii nayo inazidi kupungua kwa sababu ya sera za serikali za kubinaifisha mashirika ya umma kwa watu binafsi na matokeo yake yamekuwa yanakupunguza wafanyakazi badala ya kuongeza kuajiri zaidi na kusababisha kila siku idadi kubwa ya wanachama kutoa michango ya pensheni kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Wakati dhima ya mdhibiti na msimamizi wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamiii nchini ni kuhakikisha huduma bora za Hifadhi ya Jamii zinamfikia kila Mtanzania kupitia usimamizi madhubuti wa sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Hifadhi ya Jamii ni haki ya kila Mtanzania. Haki hii imeanishwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.
Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani hifadhi ya jamii ni mfumo ambao jamii husika imejiwekea kwa lenga ya kujikinga dhidi ya matukio yasiyotarajiwa. Matukio hayo ni kama Maradhi, ulemavu, kupoteza kazi, kuacha kazi kwa sababu ya uzee (kustaafu), aidha kwa hiari au kwa lazima na mengineyo, ikiwamo huduma za matibabu, gharama za msiba ikiwa mwanachama amefariki. Vilevile iwapo mwanachama atafariki kabla ya kustaafu basi mafao yake hulipwa kwa warithi wake kiasi cha kwamba mifuko mingine ya hifadhi ya jamii huweza hata kusaidia kusomesha watoto wa wanachama.
Lengo la hifadhi ya jamii ni kuwezesha mwananchi kuishi maisha yenye staha kwa kuwawezesha kupata huduma za msingi pale wanapokuwa hawana kipato kutokana na sababu mbalimbali zinatokana na uzee, kifo,ugonjwa, uzazi n.k
Dhana ya hifadhi ya jamii inahusisha taratibu za ulinzi dhidi ya majanga ya kiuchumi na ya kijamii yanayosababishwa na kukoma au kupungua kipato kutokana na maradhi, uzazi, kuumia kazini, ukosefu wa ajira, ulemavu, uzee, kifo na kuongezeka kwa gharama za matibabu.

Hata mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii unaotoa huduma kwa watu ambao wako katika sekta ya kilimo, sekta ya uchumi isiyokuwa rasmi na kwa wale ambao wako sekta rasmi na isiyo rasmi wanaofanya kazi kwa mkataba, na vibarua wengi wao idadi kubwa yao hawajawa wanachama wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii. Pensheni zinatolewa na mifuko iliyopo haitoshelezi mahitaji ya wastaafu kwa sababu ya kutokwenda na hali halisi ya mfumuko wa bei sokoni hivyo kuzidisha ukali wa hali maisha ya kila siku. Hivyo kuna haja watanzania kuelemishwa juu ya kujiunga na mifuko ya pensheni ya ziadi ya kujiunga kwa hiari hata kama ni mwanachama wa mchangiaji mzuri wa mifuko hii ya lazima kisheria, jaribu kuchangua mwenyewe sokoni ni upi unaweza kukusaidia hapo baada ya kustaafu ili kutunisha kikapu cha pensheni yako na familia yako

Katika kusaidia kukuza na kupanua wigo wa hifadhi ya jamii mdhibiti na msimamizi wa mfuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii SSRA sheria inasema kila Mtanzania aliye katika ajira binafsi au anayejiajiri anaweza kuamua kujiunga na Kuchangia Mfuko wa Msingi wa Hifadhi ya Jamii aupendao

Na kwa upande mwingine ni kwamba SSRA inatamka wazi ya kwamba waajiriwa au wanaojiajiri wanayo haki ya kujiunga na Mifuko ya Hiari waipendao.

Kwa kawaida kulingana na utaratibu wa uendeshaji wa hifadhi ya jamii mfuko unatakiwa kutoa namba maalumu na kadi ya uanachama kwa kila mwanachama wa Mfuko.

SSRA unatamka wazi vile vile ya kwamba ni kinyume cha Sheria kwa Mfuko mmoja kumwandikisha kwa mara ya pili, mwanachama ambaye tayari ameandikishwa na Mfuko mwingine wa msingi yaani kwa mfuko wa kujiandikisha kwa lazima kisheria

“Ili kusaidia kukuza na kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini mfuko wa pensheni wa PSPF inatamka wazi ya kwamba waajiriwa au wanaojiajiri wanayo haki ya kujiunga na Mfuko wake wa Hiari yaani PSS. Ili kuwahudumia Watanzania wote walioko ndani na nje ya nchi pamoja na raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini, PSPF imeanzisha Mpango wa Uchangiaji wa Hiari (PSPF Supplimentary Scheme) maarufu kama PSS.” Mayingu anatamka ambaye ndiye mkurugenzi mkuu wa PSPF.

Anasema kujiandikisha ni rahisi sana kwani mwanachama anatakiwa kujaza fomu PSS. FN.1 na kuambatanisha picha moja ya rangi (passport size) pamoja na taarifa muhimu za mwanachama. Mara baada ya kukamilisha usajili, mwanachama hupewa nambari na  kitambulisho cha uanachama. Mkurugenzi mkuu anasema mwanachama wa mpango wa hiari atakuwa kisheria ana haki ya kunufaika na Fao la Elimu, Fao la Ujasiriamali, Fao la Uzeeni, Fao la Kifo,Fao la Ugonjwa ,Fao la Kujitoa, Mkopo wa nyumba kwa atakayekidhi vigezo

“Mwanachama atapaswa kuchangia si chini ya Tshs 10,000 kwa mwezi. Michango inaweza kuwasilishwa kwa siku, wiki, mwezi au awamu. Mwanachama atawekewa gawio la akiba yake kwa kila mwaka mara moja ambayo ni gawio la asilimia sita (6) kwa mwaka. Uanachama ni kwa watanzania wote na wasio watanzania wanaofanya kazi nchini na hata waliopo nje ya nchi. Wanachama waliokwisha kujiunga na Mifuko mingine ya hifadhi ya jamii ikiwemo PSPF wanaweza kujiunga na mpango huu, jiunge sasa ufaidike” Mayingu anatamka bayana. Kiasi cha michango  ni shs 10,000/=  kwa  mwezi, hakuna kiwango cha juu, na mwanachama yuko  huru kuchagua  kuwasilisha michango kwa  wiki, mwezi,  au kwa msimu, na michango inaweza kuwasilishwa kwa kupitia:-Akaunti za Benki na Wakala wa malipo wa M-Pesa na Airtel money
Mpaka kufikia mwezi Juni, 2012 idadi ya wanachama wachangiaji ilikuwa 309,767 ambayo ilivuka lengo la kuwa ikiwa kama ongezeko la asilimia 4 kufikia wakati huo. Wakati mpaka kufikia mwezi Juni mwaka 2013 mfuko ulikuwa na jumla ya wanachama wapatao 367,402. Ambapo kati ya hao wanachama wachangiaji walikuwa 320, 860. Mpaka June mwaka 2012 mfuko ulikuwa na idadi ya waastafu wapatao 36, 535 na mpaka kufikia June mwaka 2913 idadi ya wastaafu iliongezeka mpaka kufikia wastaafu 46,542 ambayo ilikuwa ni sawa na ongezeko la asilimia 27 kwa mwaka.
Mkurugenzi mkuu anasema majukumu ya mfuko huu wa PSPF ni Kusajili wananachama wapya ambapo hadi kufikia mwezi Novemba 2013 Mfuko ulikuwa na jumla ya wanachama wapatao 398,717. Kutunza kumbukumbu za wanachama na wastaafu ambapo hadi Novemba 2013 mfuko ulikuwa na wastaafu 48,206. Kukusanya michango na kutunza taarifa za michango ya wanachama. Kuwekeza michango katika vitega uchumi mbalimbali na salama. Kulipa Mafao na kufanya Tathmini ya Mfuko na kuweka mikakati endelevu ambapo hadi kufikia tarehe 30/06/2013 ambapo Mfuko ulikuwa na thamani ya shs trilioni 1.25 kutoka shs bilioni 36.0 mwaka 2000
Anasema dira ya mfuko ni mtoa huduma bora wa huduma za hifadhi ya jamii nchini kwa dhima ya kutoa huduma zenye ushindani katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa wateja wao kwa kutumia watumishi wenye ari ya kazi  na teknolojia inayofaa. “Maadili Yetu ni kuhakikisha ya kuwa Mfuko unatoa huduma zake kwa wateja, wadau na umma kwa kuzingatia misingi ya Uwajibikaji, Wajibu, Muitikio, Nidhamu, Juhudi. Uwazi na Unyenyekevu kwa wote” anasema
Mkurugenzi anajaribu kutofautisha kati mifuko hii miwili mfuko wa lazima kisheria yaani PSPF na ule wa hiyari yaani PSS anasema kwa upande wa Mwanachama Wa Mfuko wa lazima kisheria Mtu yeyote aliyeajiriwa au kujiajiri katika sekta rasmi au isiyo rasmi anaweza kuwa mwanachama. Mafao yanayotolewa na Mfuko huu Mkuu ni kama vile: Mafao ya Uzeeni (Old Age Benefits), Mafao ya Ulemavu (Invalidity Benefits), Mafao ya Kifo (Death Benefits), Malipo ya“pensheni” ya Wategemezi (Survivors’ Pensions), Rambirambi ya mazishi (Funeral grants) na Mafao  ya Kujitoa (Withdrawal Benefits)
Na kwa upande wa mafao yanayotolewa na Mpango wa Hiari (PSS) ni: Fao la Elimu (Education benefit), Fao la Ujasiriamali (Entrepreneurial Support Benefit), Fao la Uzeeni, Fao la Ugonjwa au Ulemavu (Retirement benefit). Fao la Kifo na (Death gratuity), Fao la Kujitoa (withdraw benefit). Huduma nyinginezo zinazotolewa ni: Mkopo wa kujenga/kununua nyumba kwa wanachama wake waliobakiza miaka mitano kabla ya kufikia umri wa kustaafu kwa lazima ambapo mwanachama huweza kukopeshwa hadi 50% ya mafao yake yanayokokotolewa wakati wa maombi. Nyumba zilizojengwa na Mfuko wa PSPF zinazouzwa kwa wananchi wote na nyumba hizo zipo katika mikoa ya Dar es Salaam- Ilala (Buyuni), Morogoro (Lukobe), Tabora (Usule), Mtwara (Mang’amba) na Shinyanga (Ibadakuli).
Na kwa upande mwingine mkurugenzi mkuu anasema mkopo wa nyumba zilizoko katika mradi wa nyumba wa PSPF, ambapo mwanachama aliyechangia kwa muda usiopungua miaka mitano sawa na miezi 60 anadhaminiwa na Mfuko kupata mkopo wa kununua nyumba hizo kupitia benki za Azania Bank, CRDB Bank, Exim Bank na NMB.

Anasema mpaka sasa nyumba zilizojengwa ni 666. Mikopo kwa wanachama inatolewa kupitia  mabenki yalioingia mikataba maalum na  Mfuko ambapo riba ndogo ambayo ni asilimia 12 hutozwa  kwa marejesho ya hadi miaka 25. Pia nyumba zinauzwa kwa fedha taslimu kwa mwanachama na mwananchi yeyote.

Mpango wa uchangiaji wa hiari ni msaada mkubwa kwa watu wote walio na wasio katika sekta rasmi ambao kwa kujiunga na mpango huo watanufaika na mafao ya elimu, ugonjwa, ujasiliamali, fao la uzeeni, kujitoa na mkopo wa nyumba kwa wale watakaokidhi vigezo.
“PSPF sasa ni kwa watu wote walio kwenye sekta rasmi na wale ambao hawako kwenye sekta rasmi maana lengo letu ni kuwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi kupitia mpango huu wa uchangiaji wa hiari PSS ambao kiwango chake cha chini cha uchangiaji ni sh.10,000 kwa mwezi” anasema Mayingu.

Akizungumzia mwamko wa watu kujiunga na mpango huo wa hiari PSS, mkurugenzi mkuu anasema kumekuwa na mafanikio makubwa kwani tangu kuzinduliwa kwake mapema machi 7 mwaka 2013 tayari wanachama zaidi ya 5,000 wamejiunga na mpango huo. “Makundi zaidi ya 25 yamejiunga na mfuko huu kutokana na ubora wa mafao yake na mikopo inayotolewa kwa wanachama waliojiunga na mfuko huo kwa miaka mitano tofauti na wakati wa nyuma ambapo mikopo ya nyumba ilitolewa kwa wanachama waliobakiza miaka mitano ya kustaafu” anasema .

Mkurugenzi mkuu  anasema ya kwamba uanachama ni wa hiari kwa mtu yeyote aliyeajiriwa au kujiajiri mwenyewe, mwanachama aliye katika mifuko mingine, na kwamba mwanachama wa mpango wa hiari anayo fursa ya kuhamia kwenye mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria ya mfuko wa pensheni wa PSPF

Awali PSPF ilikuwa inahudumia watumishi wa Serikali Kuu na Wakala wa Serikali tu. Kufuatia mabadiliko ya sheria katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii Tanzania; sasa mtu yeyote awe kwenye sekta binafsi, sekta rasmi na isiyo rasmi anaweza kujiunga na PSPF. PSPF ni Taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa Sheria Namba 2 ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma ya mwaka 1999 yaani The Public Service Retirement Benefits Act No.2 of 1999, sura ya 371, hivyo pia Mtanzania aliyepo nje ya nchi anaweza kujiunga na PSPF na wageni wote wanaofanya kazi nchini.

No comments :

Post a Comment