Tuesday, May 29, 2012

Wastaafu Elimu Kibaha wagomea mafao ya PPF

3rd June 2010
Rais Jakaya Kikwete

Wafanyakazi waliostaafu wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, wamegoma kupokea mafao yao kutoka Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), kwa madai kwamba fedha zilizotolewa na mfuko huo ni kidogo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa wastaafu hao, Ally Gombati, alisema wafanyakazi walioamua kugomea mafao hayo ni wale waliostaafu kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka huu.
Alisema wameyakataa mafao hayo kupinga mfumo unaotumiwa na PPF ya kuwalipa wafanyakazi waliostaafu malipo kidogo tofauti na mifuko mingine ambayo inalipa wanachama wake kiwango ambacho kinamfanya mstaafu kuishi kwa muda mrefu.
"Tumeamua kueleza bayana kuwa hatuwezi kuchukua pesa za mafao hadi hapo PPF watakapofanya marekebisho na kulipa kama ilivyo mifuko mingine," alisema Gombati.
Alisema katika shirika hilo, kuna wafanyakazi wengi waliostaafu lakini baadhi ya wengine waliokuwa wanachama wa mifuko mingine ya jamii ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya (NSSF) ambao walilipwa kiasi kikubwa cha fedha hadi kufikia Sh. milioni 25 lakini wao waliambulia Shilingi milioni tano tu.
"Kitu hiki hakiwezekani kwani hawa wafanyakazi wenzetu tulikuwa na cheo kimoja lakini wamepewa mafao yanayowawezesha kuanza maisha mapya bila kutetereka, iweje sisi tuliojiunga na mfuko huo tuondoke masikini wa kutupwa," alihoji Mwenyekiti huyo.
Pamoja na hayo, Gombati alisema baada ya kuchukua hatua hiyo, walikwenda makao makuu ya mfuko huo kueleza msimamo huo lakini hawakupata ufumbuzi.
Aidha, wastaafu hao, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati mgogoro kati yao na mfuko huo ili hata watu wanaotarajia kustaafu kwa kipindi hiki waweze kulipwa mafao kulingana na muda waliolitumikia taifa.
Hata hivyo, juhudi za kumpata msemaji wa mfuko huo hazikuzaa matunda jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment