NSSF wajitoa kuzalisha umeme
3rd February 2011
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema umeanza mchakato wa kuzalisha
megwati 300 za umeme na kuziingiza katika grid ya taifa ifikapo Desemba
mwaka huu, ili kusaidia kuondoa matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa
sasa.
Mpango huo ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, jijini Arusha.
Dk. Dau
bila kutoa ufafanuzi kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa, alisema
tayari mfuko wake umeshateua mtaalamu mshauri kwa ajili ya kutekelezwa
kwa mradi huo, ambao pia hakutaja gharama zake.
Hatua
hiyo imekuja wakati nchi ikikabiliwa na matatizo ya umeme na
kulilazimisha Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza
mgawo mara kwa mara.
Dk. Dau
alikuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa NSSF unaofanyika jijini
hapa na kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa mifuko ya hifadhi ya jamii
kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi.
Aidha,
Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba
la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza.
“Madhumuni
ni kusambaza gesi inayozalishwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali ya
nchi yetu,” alisema Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na
mradi huo.
Kuhusu
wanachama wa mfuko huo, Dk. Dau alisema katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, wameongezeka kutoka 380,000 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka
2009/10 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 33.
Alisema ifikapo Juni mwaka huu wanachama wanategemewa kufikia 518,410.
Kwa
upande wa makusanyo, alisema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126.96 hadi
Sh. bilioni 315.31 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 148.
“Mategemeo yetu ni kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu,” alisema.
Akizungumzia
uwekezaji, Dk. Dau alisema shirika limeendelea kuwekeza raslimali
katika miradi ya muda mfupi na mrefu. Kutoka mwaka 2005/6 hadi 2009/10
uwekezaji wa Mfuko uliongezeka kutoka Sh. 424.89 bilioni hadi Sh.
trilioni 1.03.
Alisema uwekezaji huu umesaidia kuongeza ajira na kuboresha thamani ya shirika.
Kuhusu
ulipaji wa mafao, alsema Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha pensheni
kwa asilimia 52 ambapo kutokana na mabadiliko hayo kiwango cha chini cha
pensheni kwa wastaafu kimeongezeka kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 80,000
kwa mwezi.
Katika
hatua nyingine, Dk. Dau alisema tathmini inayoishia Juni 2009,
imeonyesha kuwa NSSF inaweza kujiendesha, hata kama shirika litaacha
kukusanya michango na bila kupata mapato yo yote kutoka katika vitega
uchumi vyake, bado linaweza kuendelea kutoa mafao yote saba na kukidhi
gharama za uendeshaji kwa muda wa miaka saba.
Akifungua
mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kazi na
Ajira, Gaudensia Kabaka, aliipongeza NSSF kwa kujizatiti kuanza ujenzi
wa daraja la Kigamboni na mipango ya kuzalisha megawati 300 za umeme na
kuziweka katika gridi ya taifa pamoja na kusafirisha gesi asilia.
“Hii ni
mipango mizuri na ni endelevu kwa ustawi na maendeleo ya taifa. Ujenzi
wa daraja la Kigamboni ambao kwa muda mrefu wananchi walitarajia kuwa
litajengwa sasa watapata faraja kusikia kuwa utaanza wakati wowote,”
alisema.
“Kuhusu
ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme ni jambo la muhimu zaidi na ni
muafaka kwa uchumi wa taifa kwani upungufu wa umeme/kukatika mara kwa
mara kwa umeme kunaathiri sana mitambo ya uzalishaji wa bidhaa
viwandani, tija na ufanisi katika maofisi kupungua na hivyo kuleta
athari kwa taifa,” alisema.
“Lakini
athari kubwa zaidi ni ile ya kukimbiza vitega uchumi kwa wawekezaji
wanaotaka kuwekeza wa ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha ajira
kwa wananchi kukosekana,” alisema, na kuongeza:
“Jitihada hizi zinazofanyika na NSSF zitapunguza sana kama si kuondoa kabisa kero hizi.”
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Abubakar Rajabu, aliiomba serikali kutoa
uamuzi wa kuukubalia mfuko huo kujenga majengo ya ofisi za ubalozi wa
Tanzania nje ya nchi ili kuokoa fedha za serikali kwa kupanga ofisi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment