Majambazi yavamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu NSSF
18th April 2010
Kiasi kikubwa cha fedha chaibwa
Dk. Ramadhan Dau
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi,
jana walivamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Dk. Ramadhan Dau na kuiba kiasi kikubwa cha fedha.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia
jana maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo watu hao walibomoa
ukuta unaozunguka nyumba hiyo na kuingia ndani.
Akizungumza na Nipashe Jumapili, Kamanda
wa Polisi wa Kinondoni, Elias Kalinga alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kusema hata hivyo, watu hao hawakumjeruhi mtu na hawakuchukua
kitu chochote zaidi ya fedha ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye
masanduku maalum ya kuhifadhia fedha.
"Ni kweli tukio hilo limetokea majira ya
saa 9 (juzi) usiku ambapo majambazi hao ambao bado hatujajua idadi yao,
waliingia ndani baada ya kubomoa ukuta wa nyumba hiyo," alisema
Kalinga.
Aidha, Kamanda huyo wa Polisi alisema
baada ya kuingia ndani waliwakamata walinzi wawili wa nyumba hiyo
waliokuwa na silaha aina ya shotgun na kuwafunga kamba kabla ya kuingia
chumbani na kuiba fedha hizo ambazo kiasi bado hakijajulikana.
Alisema baada ya kuwafunga kamba walinzi
hao waliingia chumbani kwa mwenye nyumba (Dk. Dau) na kubomoa sanduku la
kuifadhia fedha na kuondoka na fedha hizo.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, Dk. Dau hakuwepo nyumbani hapo pamoja na familia yake na walibaki walinzi hao.
Aidha, Kamanda Kalinga alisema kutokana
na mazingira ya tukio hilo kuwa ya kutatanisha, Jeshi la Polisi
linawashikilia walinzi wa nyumba hiyo, Deus Mtatilo (52) pamoja na
Yusuph Bakari (59) waliokuwepo siku ya tukio hilo.
Alisema mazingira ya tukio hilo
yanonyesha kuwa na ulakini kutokana na ukweli kuwa walinzi hao walikuwa
na silaha za moto ambazo hawakuzitumia wakati wa tukio na pia hakukuwepo
kwa milio yoyote ya risasi. Alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment