NSSF kuanza ujenzi wa Kigamboni mwaka huu
23rd March 2011
Shirika
la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limesisitiza kuwa ujenzi wa daraja la
Kigamboni jijini Dar es Salaam unatarajia kuanza muda wowote mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani
Dau, alitoa kauli hiyo jana kwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC), inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Dk. Dau aliwaambia wajumbe wa Kamati hiyo
kuwa NSSF ina fedha za kutosha kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa
unafikia Dola za Marekani milioni 120.
Kwa upande wa utalii Kamati ya Hesabu za
Serikali PAC, wajumbe wake walichachamaa na kutaka maelezo ni kwa nini
wawekezaji katika mahoteli wanajenga kwa kutumia makuti.Wabunge wa
Kamati hiyo walisema kitendo cha wawekezaji hao kujenga kwa kutumia
makuti ni dalili ya wizi na hujuma kwa Serikali.
Walisema vifaa vingi vya wawekezaji
vinasamehewa kodi hivyo hawana sababu ya kutumia makuti ambayo ni ya bei
nafuu lakini sio ya kudumu na hatari kwa wateja kwa kuwa yanaweza
kuungua muda wowote.Wabunge hao walitaka kupatiwa maelezo ni kwa nini
baadhi ya mahoteli ya Kitalii yanajibadilisha majina baada ya kumaliza
mkataba wa kufanya biashara kwa kuwa wanalenga kukwepa kulipa kodi.
Kamati hiyo pia ilimhoji Mhasibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na kushuka kwa mapato ya serikali
ambayo yeye anahusika kuyakusanya.
Akijibu hojahizo za Wabunge hao, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, alikiri kuwepo
tatizo hilo, lakini akasema tatizo halipo kwa wizara yake pekee bali
kuna wadau wengi wanaohusika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment