Sawa NSSF, wengine waige
4th February 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Maoni ya katuni
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), umetangaza kwamba umeanza mchakato wa kuzalisha megawati 300 za
umeme ifikapo Desemba, mwaka huu. Hatua ya mfuko huo ina lengo la
kusaidia kukabiliana na matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa sasa na
kulilazimisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugawa nishati hiyo
kwa mgawo.
Mpango huo ulitangazwa jijini Arusha juzi
na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, ingawa hakutoa ufafanuzi
kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa na gharama za mradi huo.
Aidha, Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake
unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi
Dar es Salaam na Mwanza.
Hatua ya mfumo huo kubuni mradi wa kufua
umeme huo imekuja wakati nchi ikiwa katika matatizo makubwa ya ukosefu
wa umeme wa uhakika.
Tatizo la umeme nchini ni la muda mrefu
kiasi cha kuilazimisha tanesco kuingia katika mikataba na kampuni nyingi
za kigeni za kufua umeme wa dharura ikiwemo Independent Power Tanzania
Limited (IPTL), Aggreko na Richmond/Dowans kwa kutaja baadhi.
Hata hivyo, baadhi ya mikataba hiyo hadi
sasa inalalamikiwa kwamba imegharimu fedha nyingi za walipakodi na
kwamba imewanufaisha vigogo na watu wachache.
Kwa mfano, mchakato wa kuipatia mkataba
wa Richmond ulibainika kuwa ulitawaliwa na mazingira ya rushwa kutokana
na kampuni hiyo kupewa tenda ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100
bila kuwa na uwezo, na baadaye kuirithisha mkataba huo kampuni ya Dowans
Tanzania Limited kinyemela.
Dowans licha ya kurithi mkataba wa
Richmond bila kupitia utaratibu wa kisheria, iliishitaki Tanesco katika
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) kwa
kusitisha mkataba wake baada ya Bunge kuazimia usitishwe.
Mkataba wa Richmond uliitikisa nchi baada
ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wawili Dk.
Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kulazimika kujiuzulu Februari mwaka
2008, baada ya kuhusishwa na kashfa hiyo.
Licha ya migongano ambayo imekuwa
ikijitokeza kati ya serikali na makampuni ya kigeni ya kufua umeme, nchi
inakabiliwa na utatizo la kutokuwa na umeme wa uhakika.
Nchi inahitaji angalao megawati 1,000,
lakini imekuwa ikishindikana kutokana na sababu mbalimbali hususan
kukauka mara kwa mara kwa mabwawa ya kuzalisha umeme kutokana na ukame.
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa
yakichangia kukosekana kwa mvua za uhakika na hivyo kuchangia uhaba wa
maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Tunaipongeza NSSF kwa kuliona tatizo hilo ambalo ni janga la kitaifa na kuamua kujitosa katika mchakato wa kuzalisha umeme.
Kwa kuwa NSSF ina mtaji wa kutosha, bila
shaka itafanikiwa kuutekeleza mchakato huo na kuzalisha umeme huo
ifikapo Desemba mwaka jana.
Mfuko huo umetangaza kuutekeleza mradi
huo wakati hali imeanza kuwa mbaya kwa uchumi wanchi. Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, jana alisema kuwa mgawo wa
umeme unaoendelea utaathiri uchumi katika robo ya mwisho wa mwaka huu
wa fedja .
Itakumbukwa kwamba Tanesco ilipandisha
gharama za umeme kwa asilimia 18.5 Desemba mwaka jana, hatua ambayo
imelalamikiwa na wananchi wengi kwamba itawaumiza kutokana na gharama za
maisha kupanda maradufu.
Hatua hiyo pia imelalamikiwa na vyama vya wafanyabiashara kwamba itawaathiri wao na wawekezaji.
Ni vizuri NSSF ikajipanga kwa ajili ya
kufanikiwa lengo hilo katika muda uliopangwa kwa kutilia maanani kwamba
mfuko huo unaendesha miradi mingi nchini.
Hatua hiyo hainabudi kuwa changamoto kwa
mashirika mengine nchini yenye mitaji ya kutosha kuangalia uwezekano wa
kuwekeza katika miradi ya kufua umeme badala ya kusubiri Tanesco kufanya
hivyo.
Huu ndio wakati kwa serikali kujipanga upya kubuni namna ya kupata vyanzo vingine vya nishati ya uhakika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment