Tuesday, May 29, 2012

JK atoa changamoto kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii

24th March 2011
Chapa
Maoni
Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA), kuyaangalia kwa makini malalamiko ya wafanyakazi kuhusu tofauti kubwa ya utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni, iliyopo kati ya mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii na mwingine.
Mifuko hiyo, ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GEPF), Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni nchini (PPF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya SSRA pamoja na nembo ya mamlaka hiyo, inayosimamia mifuko hiyo.
Alisema kutokana na tofauti hizo, wafanyakazi wenye viwango sawa vya mishahara na muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata mafao hadi mara tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine, na kusema: “Hili ni jambo la kuliangalia kwa makini sana.”
Hata hivyo, aliipongeza SSRA kwa uamuzi wake wa kuajiri Mshauri Mwelekezi anayeshughulikia suala hilo ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuwapo kwa uwiano mzuri wa mafao kati ya mfuko na mfuko, na kushauri uamuzi utakaofikiwa, uzingatie afya ya mifuko na pia tathmini ihakikishe serikali inapunguziwa mzigo.
Pia aliitaka SSRA kuangalia malalamiko ya wastaafu kwamba, mafao ya pensheni hayazingatii mfumuko wa bei, viwango vya riba katika masoko na ukuaji wa uchumi, hali ambayo alisema inasababisha wengi wao kupata pensheni isiyokidhi maisha yao ya kawaida.
Alisema uanzishwaji wa mfuko wa pensheni ya wazee, ni jambo lisiloepukika hivi sasa nchini kwani inasikitisha kusikia kuwa ni asilimia nne tu ya wazee ndiyo wanaopata pensheni.
Aliitaka SSRA kwa kushirikiana na wadau, kuandaa mkakati wa kutekeleza jambo hilo akisema kuanzisha pensheni ya wazee, serikali itafanikiwa kupunguza kiwango cha umaskini kwa zaidi ya asilimia 10.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SSRA, Siraju Kaboyonga, alisema wafanyakazi wengi nchini, bado hawajatambua ipasavyo umuhimu wa hifadhi ya jamii, hali ambayo alisema inachangia kuwakatisha tamaa baadhi ya wanachama watarajiwa kuhiari kujiunga katika mifuko hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment