Tuesday, May 29, 2012

Serikali yakiri mafao ya wastaafu hayatoshi

16th February 2011
Chapa
Maoni

Serikali imekiri kuwa mafao yanayotolewa hivi sasa na mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii nchini bado ni madogo kulinganisha na hali ya maisha.
Vile vile, imesema imejipanga kuifanyia marekebisho makubwa mifuko hiyo ili iweze kutoa mafao makubwa zaidi kwa wanachama wake tofauti na mafao wanayoyapata sasa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano baina ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Kamishna Msaidizi wa Kazi (Hifadhi ya Jamii), Daudi Kaali, alisema mafao yanayotolewa sasa ni duni mahitaji halisi ya wakati huu hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho.
Alisema ingawa hali iko hivyo, baadhi ya mifuko imekuwa ikijitahidi kuongeza mafao kila inapoona inafaa na alitoa mfano wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambao hivi karibuni uliongeza mafano kwa wanachama wake kutoka shilingi 52,000 kwa mwezi hadi 80,000.
Alisema baadhi ya mifuko mingine nayo imeongeza mafao hayo kutoka shilingi 21,000 hadi 40,000.
Kaali alisema mamlaka ya SSRA kusimamia mabadiliko ya mifuko hiyo ili iweze kutoa mafao manono yatakayowawezesha wastaafu kuishi maisha mazuri zaidi.
Alisema vile vile mifuko ya hifadhi ya jamii inawajibu wa kusaidia watu wa makundi yasiyojiweza kama wanavyochangia katika maeneo mengine.
Naye Mkurugenzi wa Mipangop na Utafiti wa SSRA, Ansgar Mushi alisema mafao yanayotolewa yanapaswa kulingana na thamani ya pesa ya wakati uliopo.
Alisema mifuko ya hifadhi ya jamii iwekeze kokote inakotaka lakini inatakiwa mafao inayotoa yawe na maana kubwa kwa maisha ya wanachama wao.
Alisema hivi sasa asilimia 3.5 tu ya watanzania ndio wako katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba SSRA imejipanga angalau kuongeza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 20 kwa muda mfupi ujao.
Tunapaswa kutoka hapo tulipo kwenda hadi asilimia 20, twende 50 hadi asilimia 100 maana hifadhi ya jamii ni haki ya msingi na inahusu haki za binadamu, kwa kuwa kuishi ni haki ya binadamu lazima vyombo vya umma kama SSRA imwezeshe mtu kuishi maisha mazuri,” alisema.
Alisema utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani miaka michache iliyopita unaonyesha kuwa asilimia 35 ya watu wanaofanyakazi hapa nchini ni maskini na wanapostaafu wanaishi maisha ya shida.
Alisema mifuko ya hifadhi ya jamii iboreshwe ili iweze kutoa mafao ya kuwanufaisha wastaafu.
SSRA inawajibu wa kuhakikisha mfumo huu unawajumisha watanzania wengi na hata mafao yanayotolewa yawe ya viwango vya kimataifa na watu wapate huduma zinazolingana hivi sasa tofauti ya mafao ni kubwa sana baina ya makundi katika jamii,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya SSRA, Siraju kaboyonga alisema tatizo la ucheleweshaji wa mafao katika mifuko ya jamii inasababishwa na ukosefu wa utunzaji mzuri wa kumbukumbu.
Alisema kuna wakati wanachama wamekuwa wakiulizwa barua za ajira zao kabla ya kupata mafao yao jambo linalowawea gumu kwani wengi wao waliajiriwa miaka mingi iliyopita.
Mimi niliajiriwa Benki Ku ya Tanzania (BoT), mwaka 1974 leo hii ukiniambia nilete barua ya mwajiri wangu ndipo unipe mafao yangu utakuwa unanitesa maana sina, utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kubwa katika utoaji wa mafao ya wanachama,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment