Wanachama wa NSSF Mwanza wachota bil. 5/-
22nd March 2010
Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF)
Wanachama 2,820 wa Mfuko wa Hifadhi
za Jamii (NSSF) mkoani Mwanza, wamelipwa mafao yao yanayofikia Sh.
bilioni 5.1 katika kipindi cha miezi minane.
Wanachama hao walilipwa kati ya Julai,
mwaka jana na Februari, mwaka huu kufuatia maombi yao waliyotuma kwenye
mfuko huko kwa kipindi hicho.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na
Meneja Mkuu wa (NSSF) mkoa wa Mwanza, Sostenes Nguma, katika
maadhimisho ya Wiki ya NSSF yanayoendelea kote nchini.
Alisema katika kipindi hicho, NSSF mkoa
wa Mwanza ulikusanya zaidi ya Sh. bilioni 11.3 kutoka kwa wanachama
wake ambayo ni sawa ya asilimia 92.6 ya lengo la kukusanya zaidi ya Sh.
bilioni l. 12.2.
Nguma alisema kudorora kwa hali ya uchumi
wa dunia kumechangia Mfuko huo kutofikia malengo waliyojiwekea kwani
makusanyo mengi katika mwaka huu hutokana na sekta ya madini,
wafanyabiashara na wavuvi.
Kuhusu fao la matibabu linalotolewa na
Mfuko huo, Nguma alisema hutolewa bure kwa wanachama waliotimiza
masharti na si kweli kwamba hukatwa mafao yao.
Alisema katika Wiki ya NSSF, mfuko huo
umekuwa ukijihusisha katika masuala ya kijamii ambapo kwa mwaka huu
umepanda miti 1,000 ya matunda, kivuli na maua katika Shule ya Sekondari
Nyamagana.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Nyamagana, Eromena Mallya, aliishukuru NSSF kwa kuchagua shule yake na
kupanda miti hiyo na kuahidi kuitunza kwa hali na mali.
“Tunaushukuru Mfuko kwa kuiona shule
yangu inafaa kuwa mfano kati ya sekondari 36 zilizo wilayani Nyamagana,
watutembelee mara kwa mara na wataona namna tunavyoianza ikiwa ni sehemu
ya utunzaji wa mazingira,” alisema Mallya.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment