Tuesday, May 29, 2012

Mishahara mipya hailipiki - waajiri

22nd April 2010
  Wasema wafanyakazi wengi watapunguzwa
  Wadai Waziri Juma Kapuya amekurupuka
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.

Waajiri katika sekta binafsi na wanasiasa wameilalamikia serikali kupandisha kima cha chini cha mishahara ya sekta binafsi kwa asilimia 100 na wameonyesha wasiwasi wao kwamba kiasi hicho kitakua vigumu kulipa.
Walitoa malalamiko hayo kufuatia tangazo la juzi la Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya (pichani).
Mjini Arusha, baadhi ya waajiri, wameeleza kushtushwa na hatua ya serikali kupandisha mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi kwa asilimia 100 wakidai kuwa hatua hiyo itawafanya wapunguze wafanyakazi kwa kuwa hawatakubali kupata hasara.
Wamesema hatua hiyo itawafanya washindwe kumudu kulipa mishahara kwa idadi kubwa ya wafanyakazi walionao kwani hakuna ambaye anapenda kupata hasara.
“Ongezeko hili la mishahara litaenda sambamba na ongezeko la mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), hali ambayo itawafanya waajiri walio wengi waingie gharama mara mbili,” alisema Wilson Leguna kutoka kampuni ya Insignia Ltd iliyopo mtaa wa viwanda mjini hapa.
Alisema mwajiri yeyote anataka kupata faida zaidi kwa kupunguza matumizi, hivyo, nyongeza ya mishahara itawapa wakati mgumu.
“Kuongeza mishahara ni kuongeza matumizi, hivyo hali hiyo itawafanya waajiri wengi katika sekta ya biashara kupandisha bei ya bidhaa zao ili kufidia matumizi katika malipo ya mishahara,” alisema.
Hata hivyo, alisema waajiri kama hao hawawezi kupandisha ghafla bei ya bidhaa zao hasa ikizingatiwa kwamba wakati huu ni wa ushindani wa kibiashara. Meneja Mkuu wa kiwanda cha magodoro, TanFoam, Riaz Somji, alisema ameshtushwa na habari ya kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 100. Hata hivyo, Somji anayemiliki kiwanda hicho chenye wafanyakazi wapatao 120 alikataa kutoa maoni kuhusu nyongeza, kwa maelezo kuwa anayepaswa kufanya hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wake, Bala Subiramania, ambaye yupo safarini.
Alisema menejimenti ya kiwanda hicho itakaa hivi karibuni kutafakari suala hilo. Mwajiri mwingine, mwenye asili ya Kiasia, alisema hakuwa na taarifa yoyote ya nia ya serikali kupandisha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.
Jijini Tanga, baadhi ya waajiri walisema serikali ilipaswa kutafuta mbinu mbadala ili kupata suluhu ya kutatua matatizo ya wafanyakazi badala ya kuwakomoa waajiri wa sekta binafsi.
Baadhi ya waajiri kutoka makampuni ya ulinzi, viwandani, hospitali binafsi na waajiri wa majumbani, wakiongea kwa sharti la kutotaka kutajwa majina yao kwa madai yataleta uchonganishi na watumishi wao, walisema kuwa Serikali ilipaswa kupandisha kwanza kima cha mishahara kwa watumishi wake.
Walisema serikali ilipaswa kutafuta maoni kwanza kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi kabla ya kuamua kutoa tangazo hilo kwani litaleta uchochezi na chuki baina ya watumishi wa sekta binafsi na waajiri wao.
Jijini Dar es Salaam, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mshahara huo ni ‘kiini macho’ na kwamba serikali haina dhamira ya dhati kuhusu ilichosema.
Chadema imesema kama serikali ingekuwa na dhamira ya kweli ingeanza yenyewe kutangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake kabla ya ile ya sekta binafsi.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mnyika, alisema jana kuwa tamko hilo la serikali ni la kisiasa tu kujaribu kuzima mgomo kwa kuwa bado haijatangaza viwango vya mishahara kwa watumishi wake.
Alisema Waziri Kapuya amekurupuka kutoa tamko kuzima shinikizo la kumtaka ajiuzulu, kama alivyoshauriwa na wadau mbalimbali.
Alisema serikali bado pia haijatoa notisi kwenye gazeti la serikali kwa kuwa notisi namba 223 ya mwaka 2007 ilivurugwa, kwa hiyo hata watumishi wa sekta binafsi wasichekelee kwa kuwa kuna dalili zote kuwa tamko hilo ni mchanga wa macho.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ashura Mustafa, alisema serikali bado haijatatua matatizo ya wafanyakazi na badala yake imeingiza siasa katika mgogoro huo mkubwa.
Alisema kumekuwa na utendaji mbovu katika idara nyingi za serikali na chanzo kikubwa ni kwa serikali kutowajali wafanyakazi wake ipasavyo.
Alisema watumishi wengi wa umma wanashindwa kuhudumia wananchi hadi watoe rushwa kutokana na uduni wa mishahara.
Alishauri kima cha chini kiwe sawa kwa sekta zote na kwamba hali hiyo inaweza kusaidia ufanisi kuonekana sehemu za kazi.
Mwenyekiti wa PPT Maendeleo, Peter Mziray, alisema kama ni suala la kuongeza mshahara serikali ndiyo inayopaswa kuanza na sekta binafsi inafuata.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samweli Ruhuza, alionyesha wasiwasi kwamba watumishi wa umma watabaki kwenye hali ngumu na hivyo wanaweza kupungua kwa asilimia kubwa kwa kutimkia sekta binafsi.
Ruhuzu alisema sekta binafsi inajiendesha kulingana na uwekezaji, hivyo mwajiri wake atakapofanya vizuri katika kuzalisha kipato ndipo hupatiwa mshahara mzuri.
Alisema kuwa serikali inatakiwa kuangalia suala hilo kwa kina zaidi kwani mtumishi wa umma hulipwa kulingana na cheo chake tofauti na sekta binafsi.
Alisema kuwa suala hilo litasababisha wataalamu wa utumishi wa umma kuondoka serikalini na kuelekea sekta binafsi kwa ajili ya kufuata maslahi.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alisema suala la serikali kutangaza ongezeko la mshahara katika sekta binafsi bado limekuwa ni kitendawili kutokana na kwamba jambo hilo halijatolewa ufafanuzi wa kutosha.
Mrema alisema alipokuwa akitizama taarifa ya habari kuhusiana na tangazo la serikali, alishangaa kumuona Profesa Kapuya akisita kutaja kiasi cha fedha kilichoongezeka.
Alisema Kapuya alitakiwa kutoa ufafanuzi wa kina kwa mfano, kueleza mtumishi wa ndani atalipwa kiasi gani na kadhalika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Agrey Mlinuka, alisema chama chake kitatoa tamko kuhusu ongezeko hilo ambalo limetangazwa na serikali kitakapopata taarifa rasmi ya serikali.
Imeandikwa na John Ngunge, Arusha, Lulu George, Tanga, Joseph Mwendapole na Beatrice Shayo, Dar.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment