Tuesday, May 29, 2012

Mafao chini ya NSSF ni ukombozi wa wengi, wanachama zindukeni

13th December 2009
Maoni ya katuni

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni moja ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ambalo limepania kujenga maisha bora ya wanachama wake sasa na baadaye. Kudhihirisha hilo, shirika limejikita katika kutoa kinga kwa wanachama wake zaidi ya 460,000 hivi sasa kutokana na majanga ya kiuchumi na kijamii ambayo husababishwa na kupungua kwa kipato.
Mwishoni mwa wiki, uongozi wa juu NSSF uliandaa mkutano mjini Zanzibar ambao uliwashirikisha wahariri toka vyombo vikuu vya habari nchini kuwaelimisha pamoja na mambo mengine huduma zitolewazo na mfuko na namna shirika lilivyojipanga kuboresha maisha ya wanachama wake siku za usoni.
Akitoa mada katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu NSSF, Dk.Ramadhan Dau aliwahakikishia wanachama kwamba mfuko uko imara kwa miaka 20 ijayo, hivyo wasiwe na wasiwasi na wale ambao hawajajiunga kufanya hivyo hima.
Alisema kwa sasa NSSF ina vitenga uchumi vyenye thamani ya sh. bil.848.8 kwa mapato ya bil.58.3/- ilipofika Juni mwaka huu, ikilinganishwa na vitega uchumi vya bil.670.3/- kwa pato la bil.43.9/- mwaka uliotangulia. Malengo mwaka 2009/2010 ni kuwekeza vitega uchumi vya tril.1,078.2/- kwa pato la bil.89.7/-
NSSF imeongeza idadi ya mafao toka matano ya awali na kufikia saba hivi sasa. Mafao ya muda mrefu ni pensheni ya uzeeni, mafao ya mkupuo maalum, pensheni ya ulemavu na pensheni ya urithi. Yale ya muda mfupi ni mafao ya matibabu, mafao ya uzazi, mafao ya kuumia kazini na mafao ya mazishi.
Mafao yote haya, hakika, yamelenga kumpa ahueni ya maisha mwanachama pindi atakapokuwa hajiwezi kutokana na majanga ya kiuchumi na kijamii. Pamoja na ukweli huo, kama alivyoeleza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, bado wapo wanaosita kuchangamkia mafao hayo hasa fao la matibabu pamoja na kwamba ni wanachama wakihofia kukatwa pensheni. “Huduma hiyo ni bure hakuna makato”, alisistiza Mkurugenzi wa Matekelezo NSSF, Crescentus Magori katika mada yake.
Pamoja na ukweli kwamba fao la matibabu ni bure lakini ni idadi ndogo sana ya wanachama waliojitokeza kupata huduma hiyo. “Zilitengwa sh. bil.3/- mwaka 2004 lakini hadi sasa ni mil. 100 tu zilizotumika. Watu bado hawaamini…ni wachache sana wamejitokeza kuliko ilivyotegemewa”, alisema Dk.Dau.
Hata sisi tunajiuliza, kwanini walengwa wanasita kutibiwa bure kupitia fao hilo la matibabu? Je, ni elimu haijawafikia vema kuhusu fao hilo au ni kitu gani. Utafiti wa kina yafaa ufanywe kujua tatizo liko wapi.
Lakini hata hivyo, huduma hiyo ni nzuri na muhimu hasa ikizingatiwa kuwa ni ya bure kwa wanachama wa mfuko huo.
Pia NSSF imeonesha mfano wa kuigwa kwa kuongeza kiwango cha pensheni kwa wanachama kuanzia Septemba mwaka huu kutoka sh.33,200/- hadi 52,000. Hii ni katika jitihada zake za kuwajali wanachama wake.
Ni mfuko uliojiwekea malengo hadi miaka 50 ijayo. Lakini ili ufike huko, yapo mambo mengi yamewekewa mkakati ikiwa ni pamoja na kutaka yawepo maboresho ya sheria zinazolinda mifuko ili iweze kuendelea, kuimarika na hatimaye idumu.
Kwa mfano, Dk.Dau anasema, waliojiajiri wenyewe, sheria haiwalazimishi kujiunga na NSSF. Hawa nao mfuko unataka wajiunge. Au mtu akiacha kazi asipewe fedha zake hadi atimize muda wa kustaafu. Kwa sasa mtu anaruhusiwa kuchukua fedha zake kabla ya kustaafu. Utaratibu huu unatishia maisha ya mfuko wa hifadhi.
Wengine wanataka kuchangia lakini wanachagua fao mojawapo. Kisheria ni lazima wanaojiajiri wenyewe wachangie mafao yote saba, jambo ambalo hawalikubali.
Tunaamini kwamba mamlaka husika zimeshafikishiwa mapendekezo hayo kuona uwezekano wa kuyafanyia kazi ili NSSF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wake.
Siyo siri kwamba mafao ya NSSF yanagusa makundi muhimu ndani ya jamii yetu ambayo ni wazee, walemavu, wanawake na watoto, wafanyakazi na kadhalika, hivyo serikali inapaswa kuunga mkono juhudi zake zilizolenga kujenga maisha ya wanachama wake sasa na baadaye.
Ni imani yetu kwamba waajiri na wafanyakazi wote katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, wizara, idara zilizoajiri wafanyakazi ambao wako chini ya mikataba maalum, mashirika ya umma, mtu binafsi aliyejiajiri mwenyewe, watazinduka na kuchangamkia kujiunga na NSSF kunufaika na mafao yatolewayo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment