Tuesday, May 29, 2012

Benki kupiga mnada Mgodi wa Kiwira

12th March 2011

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja

Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira ambao uligeuzwa kuwa kitega uchumi cha kujipatia fedha za kukopa kutoka taasisi mbalimbali za fedha nchini hivi sasa madeni hayo yameanza kuutokea puani ambapo Benki ya CRDB imeandika barua kwa serikali ikielezea kusudio lake la kutaka kuupiga mnada mgodi huo.
Mgodi huo ambao hadi sasa upo chini ya mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL) licha ya serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja, kutoa taarifa kuwa umerejeshwa serikalini, hadi sasa unadaiwa madeni na taasisi mbalimbali za fedha zaidi ya Sh.28,869,938,996.
Taasisi za fedha ambazo zinaudai mgodi huo ambazo zilikopwa na mwekezaji ni pamoja na CRDB deni lote pamoja na riba ni Sh.bilioni 4.077, Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Sh.bilioni 9.497 na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh. bilioni 15.294.
Madeni hayo kwa mgodi huo yalibainika wakati Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF, Yakubu Kidula, alipokuwa akitoa taarifa juu ya pendekezo la NSSF la kuchukua kampuni ya Kiwira Coal and POWER Limited kwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAOC).
Alisema kutokana na hali hiyo, Benki ya CRDB imechukua hatua ya kuiandikia barua serikali ikielezea kusudio la kutaka kuupiga mnada mgodi huo kwa kushindwa kulipa deni hilo ambalo mwekezaji huyo alikopa Dola milioni saba kwa lengo zitumike kuzalisha umeme megawati 50.
Kidula alisema hata hivyo, NSSF wameiomba Benki ya CRDB isitishe uamuzi wake wa kutaka kuupiga mnada mgodi huo kwasababu NSSF inakusudia kuwa mwekezaji mpya wa mgodi ambapo itachukua jukumu la kulipa madeni yote yanayodaiwa na taasisi zote zinazoudai mgodi huo.
Kwamujibu wa barua ya CRDB yenye kumbu Na. 3390/654316/4113 ya 28 Julai 2009 ambayo NIPASHE imepata nakala, aliandikiwa Ngeleja, ikitaka serikali kulipa deni hilo lililokopwa na mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Project (KCPL) kwa ndiye mdhamini mkuu wa mkopo huo.
Hata hivyo Septemba 5 , 2009 Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, katika barua yake yenye kumbu Na.CDA 48/171/01 aliijibu Benki ya CRDB kwa kueleza kuwa wizara yake ingefanya kazi kwa kushirikiana na wakopeshaji ili kuhakikisha kuwa suala hilo linatatuliwa mapema iwezekanavyo.
Februa mwaka jana, CRDB ilimkumbusha Waziri wa Nishati na Madini kuhusiana na kushindwa kwa kampuni ya KCPL kulipa deni lake na kueleza kuwa hatua iliyobaki ni kwa wakopeshaji kuuza mgodi wa KCPL kwa mnunuzi yeyote ili kurudisha fedha walizoikopesha KPCL.
Pamoja na mfululizo wa barua zilizoandikwa na CRDB, wizara iliendelea kukaa kimya ambapo Disemba mwaka jana (2010) Benki ya CRDB iliandika barua ngingine kwa Waziri yenye kumbu Na. 3390/654316/4113 ikimtaarifu kwamba wakopeshaji hawana njia nyingine zaidi ya kuuza Mgodi wa Kiwira.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment