Tuesday, May 29, 2012

NSSF, Dowans, Muhimbili na Tanesco, zanyooshewa kidole

29th April 2009
Shirika la Umeme (Tanesco).

Mashirika kadhaa ya umma na taasisi nyeti za serikali yamepuuza mapendekezo ya ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yaliyotakiwa kufanyiwa kazi, kwani kasoro zilizogundulika na kutakiwa kurekebishwa zimeendelea kuwepo mwaka mmoja baadaye.
Kasoro hizo ni uvunjaji wa kanuni za matumizi ya fedha za walipa kodi ambazo katika kipindi cha ukaguzi kilichopita zilitakiwa kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2007/08 iliyowasilishwa bungeni juzi, baadhi ya taasisi hizo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Taifa (NSSF), Shirika la Umeme (Tanesco), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na taasisi nyingine nyeti za serikali.
Kwa hospitali ya Muhimbili, kwa mfano, ripoti inaonyesha kwamba kuna jengo binafsi lililojengwa katika eneo la hospitali ambalo mkataba unaonyesha kwamba lilitakiwa kuwa mali ya hospitali kuanzia mwaka 1992, lakini limeendelea kuwa mali ya mtu huyo, H.A Kiluvia.
Imeelezwa kuwa jengo hilo kwa sasa kuna benki ya National Microfinance Bank (NMB) na duka la dawa.
“Mkataba umeshamalizika lakini jengo bado liko kwenye himaya ya H. A. Kiluvia kinyume na makubaliano ya mkataba (licha ya mapendekezo yetu ya mwaka 2006/07),” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza, katika ripoti yake iliyopita, kusitishwa kwa mkataba wa Kampuni ya Kuhudumia Makontena Bandarini (TICTS) kutokana na kuongezewa kipindi kingine cha miaka 15 kinyume cha sheria, lakini mkataba bado haujavunjwa hadi ripoti hiyo inaandikwa.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG ilipofuatilia mapendekezo hayo yaliyotolewa mwaka 22 06/07, haikupata majibu, hali inayoonekana kwamba hakuna utekelezaji kwa upande wa serikali.
Kadhalika, CAG anasema katika ripoti yake kwamba Tanesco ilishauriwa kuidai kampuni ya M/s Dowans Holdings tozo (liquidated damage) kutokana na kampuni hiyo kukiuka mkataba kwa kushindwa kuzalisha umeme wote wa megawati 100 kama mkataba unavyoonyesha.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG haikupata majibu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo hayo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza kwa Hazina kukusanya madeni yatokanayo na mauzo na ubinafsishaji wa mashirika ya umma kutoka kwa wawekezaji.
Ilipendekeza pia kwamba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wawekezaji walioshindwa kutekeleza majukumu yao ya mikataba ya uwekezaji.
Pia ilipendekeza kwamba mashirika na taasisi za umma ambazo bado zinajiendesha kwa hasara zichukuliwe na serikali au kuuzwa tena.
Hata hivyo, ripoti inasema kwamba mapendekezo hayo hayajafanyiwa kazi hadi ripoti mpya ilipokuwa ikiandaliwa.
Kuhusu NSSF, ofisi ya CAG ilipendekeza isiendelee kukopesha na kwamba kiasi cha mikopo kilichoripotiwa ni kikubwa kuliko inavyotakiwa.
Hata hivyo ripoti inaonyesha kwamba ushauri haukuzingatiwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment