Upinzani wahoji mabilioni ya NSSF yaliyokopeshwa Kiwira
17th July 2009
Yasema inawekeza pasipo na tija
Kambi ya Upinzani bungeni, imehoji
mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Sh. Bilioni
8.4 kwa Kampuni ya Makaa ya Mawe na Nguvu ya Umeme – Kiwira utarudishwa
lini, huku wanachama wanaostahili kulipwa mafao yao wakisaga soli za
viatu kufuatilia.
Hoja hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kambi
hiyo, Salim Abdallah Khalfani, kwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya
Vijana, wakati akichangia maoni ya Makadirio ya Matumizi katika wizara
hiyo.
Alisema kambi hiyo ina wasiwasi wa kutokuwepo ushahidi wowote wa dhamana iliyowekwa iwapo mkopaji atashindwa kurejesha.
Ameir alisema mkopo huo ulitarajiwa kulipwa baada ya miezi sita lakini hadi Machi 26, mwaka huu, ulikuwa haujalipwa.
“Isitoshe, Mkataba huo katika kifungu
10.5 unasema kuwa mkopo huo umedhaminiwa na serikali kwa asilimia 100
pamoja na Benki ya CRDB. Hii inashangaza kwani fedha zenyewe ni za
wafanyakazi wa Tanzania, na serirkali yao inadhamini kwa asilimia 100,”
alisema.
Ameir alisema Kambi hiyo inaitaka
serikali kuhakikisha inachukua hatua za haraka za kiutawala ili
kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kama sheria inavyotaka.
Alisema mbali na matatizo hayo ya
udhibiti wa fedha za wanachama pia NSSF imetamkwa kuwa ni miongoni mwa
taasisi zenye utunzaji mbovu wa kumbukumbu za wafanyakazi ambapo
mikataba ya ajira, nakala za vyeti, barua za ajira, taarifa za
kupandishwa vyeo, uhamisho na ongezeko la mishahara wakati wa ukaguzi
havikuwepo.
Aidha, alisema shirika hilo halizingatii
sheria ya ajira ambapo wakati wa ukaguzi iligundulika kuwepo kwa
uvunjwaji wa sheria za ajira kwa kutoa ajira bila kufuata taratibu
zilizowekwa.
Katika hatua nnyingine, Kambi hiyo
ilisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika
ukaguzi wake kwenye Shirika hilo iligundua matumizi ya hovyo hovyo ya
fedha za wanachama.
Alisema NSSF ilikopesha jumla ya Sh.
1,525,368,525 kwa kampuni ya M/S Medtech toka Aprili 2003 na mkopo
ulitakiwa kurejeshwe Desemba 2004, hadi sasa pesa za wanachama
hazijarudishwa.
“Kwa ujumla ripoti imebaini kuwa NSSF imekuwa inawekeza sehemu zisizo na tija kwa wanachama,” alisema.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo inasema kuwa
NSSF ni miongoni mwa taasisi zenye masurufu yanayofikia jumla ya Sh.
22,231,219 ambayo hayajarejeshwa na kwamba imenunua hisa au kuwekeza
katika mashirika kadhaa lakini hakuna gawio inayopata.
Alisema fedha zilizowekezwa na NSSF
kwenye mabano ni Tanzania Oxygen Ltd (sh. 13,200,000), Tanzania Housing
Bank (sh. 495,280,000) na kwamba 1st Adili Bank Corp Litd ilipewa mkopo
wenye utata wa sh 3,152,024,742.
Kampuni zingine ambazo NSSF imewekeza
bila kupata gawio kwa kipindi chote ni CDC Mbeya Cement (sh.
1,152,024,742), Ubungo Plaza (sh. 9,817,038,702), TANR Share
(sh.1,000,000,000), HEPZ Quality Group Share (sh. 47,156,025,113) na
PPL pension Properties (sh. 3,500,00). Jumla ya uwekezaji usio na tija
ni sh. 62,789,093,299.
Alisema mifano hiyo ni michache
inayoashiria udhaifu mkubwa katika upangaji wa miradi na uwekezaji wa
NSSF na kwamba inapaswa suala hilo kuchukuliwa kwa uzito maalumu ili
kunusuru fedha za wanachama.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment