Tuesday, May 29, 2012

Ujenzi daraja la Kigamboni wanukia

21st November 2011
Chapa
Maoni
Wakandarasi saba ambao wamefanikiwa kupita katika mchakato wa awali wa kumpata mkandarasi atakayeshinda zabuni ya ujenzi wa daraja la Kigamboni tayari wamefanya ukaguzi katika eneo hilo. 
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martini Ntemo, alisema wakandarasi hao wametembelea eneo hilo mapema wiki hii kwa ajili ya kufanya tathmini ya ujenzi.

Alisema kabla ya mchakato huo wa kuwapata wazabuni walijitokeza wakandarasi 16 walichambuliwa na ndipo walipopatikana hao saba ambao wanashindanishwa.

Ntemo alisema lengo la ziara hiyo ni  kuwapatia maelezo ya kitaalam wakandarasi hao kuhusu maudhui ya mradi husika na changamoto zake kabla ya kuwasilisha makisio yao kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. 

Alisema ujenzi wa daraja hilo unatarajia kuanza mwanzoni mwa mwaka 2012 na kwamba tayari zimeshatengwa bilioni 130 kwa ajili ya zoezi hilo.

Hata hivyo, alisema daraja  hilo ambalo ni la kisasa zaidi kujengwa hapa nchini ambapo litakuwa na barabara tatu kila upande yaani kuwa na uwezo wa kuruhusu magari sita kupita kwa wakati mmoja. 

“Daraja hilo linatarajiwa kuwa na urefu wa mita 600 na litakapokamilika litakuwa ni kiungo muhimu kati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni na pia litachangia kupunguza msongamano wa magari hapa jijini," alisema Ntemo 

Alisema Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF tayari limeshatoa Sh bilioni 100  kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa daraja hilo kwa kushirikiana na Wizara hiyo ambapo watachangia asilimia 40.

Aidha, alisema mchango huo wa NSSF  ni moja ya maagizo ambayo aliyatoa Waziri wa Ujenzi, Dk John  Magufuli  Mwezi Machi mwaka huu ambapo aliwataka kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni unaimarishwa na hivyo kuondoa kero ya usafiri.

 Ntemo alisema NSSF itachangia  asilimia 60 na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itachangia asilimia 40 zilizobakia. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment