Mkataba wa ujenzi daraja la Kigamboni wasainiwa
10th January 2012
B-pepe
Chapa
Maoni
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF), Ramadhani Dau, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Shi Yuan
kutoka kampuni ya ujenzi ya China Railways Constructin Engineering
Group, kwa pamoja wakiweka saini ya mkataba wa ujenzi wa daraja la
Kigamboni na maungio yake jijini Dar es Salaam jana. Kazi hiyo ya ujenzi
inatarajiwa kuchukua miezi 36.(PICHA: OMAR FUNGO)
Ujenzi
huo utatekelezwa na kampuni ya China Railway Construction Engineering
Group Co. Ltd kwa kushirikiana na China Major Bridge Co. Ltd na
utagharimu Sh. 214,639,445,523.80 kwa kipindi cha miaka mitatu.
MAGUFULI: TUFANYE KAZI, TUACHE SIASA
Akizungumza
baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John
Magufuli, alimtaka mkandarasi kukamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo
hata kabla ya muda uliowekwa, lakini azingatie ubora wa kazi.
“Sioni
sababu ya kusubiri muda huo kwa sababu pesa zipo; nataka mradi huu
ukamilike kabla ya muda uliopangwa ili Rais Jakaya Kikwete auzindue
kabla hajamaliza muda wake,” alisema.
Dk.
Mgufuli, aliwaasa viongozi na wananchi kwa ujumla kuacha siasa kwenye
masuala yanayohusu maendeleo kwa kuwa siasa inakwamisha mipango
mbalimbali.
“Watanzania
sasa wamechoka na maneno wanataka utekelezaji, tufanyekazi tuache
siasa, zitatupotezea muda na zitatupeleka pabaya,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza: “Ifike mahali tuache kusimamia siasa tupambane kuwaletea Watanzania maendeleo.”
Kuhusu
miradi mingine, alisema serikali inatekeleza miradi mingi ya ujenzi wa
barabara na madaraja na kwamba makandarasi wamekuwa wakituma maombi kila
siku.
Alisema
serikali imejipanga kupanua barabara ya Morogoro kutoka Dar es Salaam
hadi Chalinze na ya kutoka Arusha-Himo, mkoani Kilimanjaro; pamoja na
ile ya mabasi ya mwendokasi kutoka Kimara hadi Kivukoni, jijini Dar es
Salaam.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, alisema daraja hilo litakuwa
la njia sita za lami za magari na njia za waenda kwa miguu.
Aliishukuru
serikali kwa kukubali kuchangia asilimia 40 ya gharama za ujenzi na
kuahidi kwamba shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali katika
kutekeleza miradi mbalimbali yenye manufaa kwa taifa.
AJIRA 2,000 KUZALISHWA
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema mradi huo
utazalisha ajira za muda mfupi zaidi ya 2,000 na kuwataka wananchi
hususani vijana kuzichangamkia na kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii na
uadilifu.
Hata
hivyo, aliwaonya watu wenye tabia za wizi kutothubutu kwenda kwenye
mradi huo kwa kuwa ataimarisha ulinzi kwenye eneo hilo: “Hata
ikiwezekana tutaweka kituo cha polisi pale, vijana wa Dar es Salaam
changamkieni ajira hizi, lakini msiwe wazembe au wadokozi.”
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, ambaye
ni Mwenyekiti wa kamati ya wataalam wanaosimamia ujenzi huo, alisema
kamati yake itafanyakazi kwa uadilifu ili kuhakikisha kuwa daraja hilo
linajengwa kwa ubora wa kimataifa.
Hafla
ya kusaini makubaliano hayo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, ambaye alisema mradi huo
utazalisha pia ajira za kudumu takribani 1,000.
Wengine
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Hubert Mrango, Wenyeviti wa
Bodi mbalimbali ikiwemo ya makandarasi, wahandisi, wabunifu majengo na
wakadiriaji majenzi na maofisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya
Ujenzi na NSSF.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment