SSRA yaanisha changamoto mifuko ya hifadhi ya jamii
8th October 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Muundo
wa kisheria wa mifuko ya hifadhi jamii nchini ni moja changamoto
zinazoikabili Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii nchini (SSRA).
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam
juzi na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, alipozungumza na wahariri
wakuu wa vyombo vya habari kuhusu kazi za Mamlaka hiyo katika kusimamia
mifuko ya jamii nchini.
Alisema hali ilivyo sasa mifuko hiyo
kisheria inaripoti kwa wizara tofauti, akitaja kuwa Mfuko wa Pensheni
Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF)
na GEPF iko chini ya Wizara ya Fedha; Mfuko wa Bima Afya (NHIF) uko
chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) chini ya Wizara ya Kazi na Ajira na Mfuko wa Watumishi wa
Serikali za Mitaa (LAPF) uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na za Serikali Mitaa (Tamisemi).
Kadhalika, Isaka alisema kila mfuko una
sera yake ya uwekezaji, wigo finyu wa hifadhi ya jamii kwa Watanzania
yote kwa pamoja ikiwa imesajili asilimia mbili tu ya Watanzania wote.
Mifuko hiyo ina jumla ya wanachama 853,531 kati ya Watanzania milioni 42.
Mkurugenzi huyo alitaja changamoto
nyingine kuwa ni mfumo ulipo sasa unabana wanachama kwani hauruhusu
kuhamia mfuko mwingine; fofauti kwenye ukokotoaji wa mafao, tofauti
kubwa ya mafao kati ya mifuko; ukosefu wa takwimu sahihi; gharama kubwa
za uendeshaji wa mifuko, uelewa mdogo wa hifadhi ya jamii kwa watunga
sera, waajiri na waajiriwa na umma kwa ujumla.
Isaka alisema ukosefu wa pensheni ya wazee ni changamoto kubwa kwani ni asilimia nne tu ya wazee ndio wanaopata mafao hayo.
Alisema mamlaka hiyo mpya kwa
kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepata mtathmini ambaye
anapitia tathimini zote za mifuko, hali ambayo itawasaidia kujua thamani
halisi ya mifuko yote nchini.
Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi
hilo, SSRA watatoa taarifa na miongozo mbalimbali ili kusimamia vema
sekta ya mifuko ya jamii nchini.
Isaka alisema SSRA inatarajia kuwa na
wiki ya hifadhi ya jamii ambayo itafanyika Novemba mwaka huu ambayo
mifuko yote ya hifadhi ya jamii itapata fursa ya kueleza umma shughuli
wanazofanya ili Watanzania waijue.
CHANZO:
NIPASHE
No comments :
Post a Comment