China. Maeneo mengi ya nchi ya China hivi sasa hali ya hewa ni joto, katika mji mkuu wa nchi hii, Beijing muda mwingi ni zaidi ya nyuzi joto 31, wakati mwingine hufika hadi 38, wenyeji wanasema kuna wakati linaweza kufika hata nyuzi joto 40.
Waliosoma jiografia wanajua China ni miongoni mwa nchi ambazo kukiwa na joto ni joto kweli na kukiwa na baridi ni baridi kweli, hususan katika baadhi ya maeneo.
Lakini hali ya hewa kwa sasa kwa ujumla ni joto na kutokana na eneo ilipo nchi hii inakuwa na kipindi kifupi cha giza tofauti na ilivyo nyumbani, hivyo kuna muda mwingi wa mwanga kuliko giza.
Julai 26, wenyeji wangu hapa, hususan katika jiji la Beijing ambako ndiko ninaishi muda mwingi waliniambia: “Kesho tutakwenda mahali si mbali sana na hapa, itabidi ubebe koti jepesi na mwavuli”.
Akili yangu ikajua tayari tunaelekea eneo lenye baridi na mvua, hivyo nikajiandaa na safari kama nilivyoelekezwa.
Julai 27 saa mbili asubuhi tunaianza safari, naambiwa tunaelekea katika moja ya vivutio vikubwa duniani, vilivyobeba historia ya nchi ya China na bara la Asia kwa ujumla, nilifurahi sana.
Jiji la Beijing ni kubwa, ukiwa kati kati ya jiji hilo na unatoka kwenda nje ya mji inachukua muda kidogo, hivyo baada ya kitambo kidogo tulifika katika barabara ya kulipia (Express way) kama ile tunayokusudia kujenga kuunganisha Dar es Salaam na Dodoma.
Baada ya kuingia express tukaachana na foleni na karaha za makutano ya barabara.
Baada ya maili 37, sawa na kilomita 60 kutoka jijini Beijing tulifika mwisho wa safari yetu ya gari, hapo tulishuka. Ukiwa hapo ni kama upo bondeni, ukitazama kila upande ni milima tu na utaona kama mstari ulionyooka ambao kila baada ya umbali fulani utaona kama ngome hivi. Wenyeji wangu wakaniambia tunakwenda kwenye ukuta mrefu duniani, maarufu Great Wall.
Tukasogea katika ofisi ya waongoza watalii tukalipia kisha tukapatiwa binti mmoja ambaye umri wake unakadiriwa kuwa si zaidi ya miaka 30, yeye ndiye alitupa maelezo ya kina kuhusiana na eneo hilo la historia, alikuwa akitumia lugha ya Kichina hivyo sikukaa mbali na mkalimani wangu.
Ukipita tu katika lango la kwanza unaanza kushuhudia majengo makubwa imara, lakini ya kale na kila moja lilikuwa na kazi yake wakati huo, mwongoza watalii alituambia kuwa ukuta wa Great Wall ulianza kujengwa kabla ya kuzaliwa kwa Kristo na ulichukua zaidi ya miaka 2,000 kukamilika.
Taarifa za urefu wake hakuna mwenye uhakika nazo, lakini unatajwa kuwa na urefu wa zaidi ya kilomita 20,300 na wengine husema ni zaidi ya 21,000, ukizunguka majimbo 15 ya nchi ya China. Mwaka 1987 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (Unesco), liliutaja ukuta huu miongoni mwa maajabu saba ya dunia.
Ukuta huo ni mfululizo wa kuta na ngome uliojengwa kwa shabaha ya kuimarisha ulinzi wa mataifa na makabila ya kaskazini mwa Asia ambayo yalikuwa yakiivamia nchi hiyo mara kwa mara, huku wakitumia usafiri wa farasi na ngamia.
Kwa nje ukuta unakuwa mrefu ili kuzuia mtu kuupanda au kuuruka kwa urahisi, lakini kwa ndani unakuwa mfupi ili kuwawezesha watu kukimbia au kuokolewa.
Ulikuwa na mifumo mingi, ikiwamo ilivyo mipaka mbalimbali hivi sasa au ngome za kijeshi, kuna sehemu ambapo askari huweka kamba kumewekwa mfumo wa maji yaliyokingwa ambayo hufunguliwa pindi wanapogundua adui anasogea na kwa sababu ya hali ya baridi maji hayo huganda, hivyo sio rahisi mtu kupita.
Katika vilele vya miinuko mbalimbali ya eneo lililozungukwa na ukuta utaona vijumba vilivyoinuka kwa juu zaidi, ambavyo vilikuwa vikitumika kama mnara wa mawasiliano.
“Mchana wanatumia kinyesi cha wanyama kufukiza moshi mzito pindi wanapoona adui ili askari wa usaidizi wasogee karibu, usiku watawasha moto, wenzao katika kituo kingine cha mawasiliano wakiona ishara hizo wanajua tayari adui kaonekana mahali, hivyo hujipanga kwenda kutoa usaidizi,” alisema mwongoza watalii.
Aliongeza kuwa fundo moja la moshi liliashiria maadui idadi yao ni chini ya 1,000, mawili yaliashiria chini ya 2,000, yaani kila moshi au moto uliashiria elfu moja.
Baada ya maelezo hayo safari iliendelea tukipita majumba mbalimbali ambayo ni sehemu ya ukuta huo, sehemu ya majengo yana nakshi za utamaduni wa bara la Asia, ikiwemo taswira maarufu ya Buddha na maandishi ya lugha zilizotumiwa wakati huo.
Mbele tukutana na njia ya kushuka chini zaidi ili uweze kupata ukuta huo, ambao katikati yake kuna upenyo ama njia unayoweza kuiita ya watembea kwa miguu ambayo watu hata watano mnaweza kupishana kwa wakati mmoja.
Unahitaji maji ya kutosha, pumzi na uthabiti wa misuli kuweza kupanda ukuta huo, mwanzo mwa safari utakutana na maneno ya Rais wa zamani wa taifa la China, Mao Zedong yakisomeka kwa lugha ya Kichina na tafsiri yake kwa Kiingereza ni kuwa ‘A man who has never been to the Great Wall shall not be considered as a hero’, ama kwa lugha ya Kiswahili ni kwamba yeyote ambaye hajawahi kupanda ukuta mrefu sio shujaa.
Pengine ni kauli ya kuhamasisha watu wengi zaidi kutembelea eneo hilo linalovutia, katika kila ukuta kuna matundu yaliyokuwa yanatumika kama vilengeo vya kurusha mishale na silaha nyingine zilizokuwa zikitumika wakati huo.
Jambo nzuri ni kuwa ukuta huo umehifadhiwa vizuri na mamlaka za nchi hii wanahakikisha historia haipotei, barabara zinazounganisha Beijing na maeneo mengine zinazopita katika aneo hilo ilibidi zipitishwe kwa chini ili juu kusiharibike, reli vilevile.
Wahifadhi wapo muda wote kuhakikisha kila kinachotoka kinarudishwa, hii ndiyo maana halisi ya uhifadhi, kutunza historia na vivutio.
Jambo jingine ukiangalia ukubwa wa ukuta, unene wa mawe na matofali yaliyotumika kujengea unaweza kusema hao wazee walitumia nguvu zao vibaya kwa miaka 2,000 kwa ajili ya ulinzi tu, lakini ni wazi wameacha urithi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Pengine wazee hawakujua kuwa wameacha hazina kubwa yenye thamani, hususan hivi sasa ambapo namna ya ulinzi na vita zimebadilika, lakini namna yao ya ulinzi wakati huo na jitihada zao ni kivutio kikubwa cha utalii, mabilioni ya Shilingi pengine yanapatikana kila mwaka kutoka watalii maana kupanda na kushuka unapishana na watu tu.
No comments :
Post a Comment