Mwanza/Tarime. Uongozi wa Serikali na CCM Mkoa wa Mara umetangazia kiama wote wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa mawe ya dhahabu kutoka mgodi wa Barrick North Mara ulioko eneo la Nyamongo wilayani Tarime.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Samuel Kiboye maarufu “Namba Tatu” walihusisha mtandao huo na baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho tawala.
“Kuna watu wanajificha kwenye nguo za kijani kwa kujifanya wana CCM kufanya uhalifu, baadhi wanaingia kwenye uongozi wa vijiji kufanikisha malengo yao. Hii haikubaliki. Naviagiza vyombo vya dola kuwasaka wote, hasa wale mapapa wanaofadhili mtandao huu wa wizi,” alisema Hapi alipotembelea mgodi wa Barrick North Mara na kuongeza:
“Huu mtandao lazima umalizwe. Vyombo vya dola fanyeni oparesheni bila kumuonea mtu wala kumuacha mwizi, wakamateni wote, kamateni mapapa wanaoongoza mtandao huu bila kujali nafasi za uongozi kwa sababu mhalifu ni mhalifu tu.”
Akizungumza na Mwananchi kwa simu hivi karibuni kabla ya kuenguliwa kwenye nafasi hiyo, Hapi alisema tayari vyombo vya dola viko kazini kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini wote walioko katika mtandao unaoiba mawe kutoka mgodi huo kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
“Siwezi kueleza wazi hatua iliyofikiwa hadi sasa kuepuka kuharibu uchunguzi, lakini kazi imeanza na tutawanasa wote. Serikali haiwezi kukubali kuona watu wachache wanavuruga mikakati ya kuongeza mapato kupitia sekta ya madini kwa kuiba na kutorosha madini nje ya nchi. Tunataka mapato ya madini yetu yatunufaishe wote kama Taifa,” alisema Hapi, ambaye nafasi yake sasa inachukuliwa na Dk Raphael Chegeni
Kuwekwa kwake kando kumeibua gumzo katika mitandao ya kijamii, kwani baadhi wanaona kumechelewa baada ya Februari mwaka huu, Rais Samia akiwa Mara kueleza kuwa na taarifa za ufujaji mkubwa wa fedha.
Hapi ambaye kabla ya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara alikuwa katika wadhifa kama huo mkoani Iringa, aliingia katika malumbano makubwa ya kisiasa, pale alipowashukia baadhi ya viongozi wakuu wastaafu walioonekana kumkosoa hayati John Magufuli.
CCM yapigilia msumari
Akizungumza na Mwananchi kuhusu madai ya baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM kujihusisha mtandao wa wizi wa mawe ya dhahabu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye alisema chama kitawawajibisha wote ambao tuhuma dhidi yao zitathibitishwa na vyombo vya dola.
“CCM inaunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti uhalifu, ikiwemo wizi wa mawe ya dhahabu kutoka mgodi wa Nyamongo (Barrick North Mara). Wote watakaobainika kuhusika watafikishwa kamati ya maadili. Hatuwezi kuendelea na viongozi wanaokiuka maadili,” alisema Kiboye.
Ingawa Mkuu wa mkoa na Mwenyekiti wa CCM mkoa waligoma kuwataja viongozi wanaodaiwa kuongoza mtandao huo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini katika orodha hiyo wamo viongozi wa CCM Wilaya ya Tarime kuanzia ngazi ya matawi, kata hadi wilaya.
“Kutatokea mtikisiko ndani ya CCM iwapo vyombo vya dola vitafanya uchunguzi wa kina na kuweka wazi majina ya wahusika wote kwa sababu wapo viongozi wakubwa na wenye ushawishi wanaofadhili mtandao huu,” alisema mtoa taarifa wetu kwa sharti la kuhifadhiwa jina.
Huku akionyesha kuufahamu vema mtandao huo, mtoa taarifa wetu alisema: “Madini yanayoibiwa kutoka mgodi wa Nyamongo yanauzwa mji wa (tunahifadhi jina kwa sasa) katika nchi jirani.”
Alisema ni vigumu kudhibiti utoroshaji huo kutokana na mtawanyiko wa mpaka kati ya Wilaya ya Tarime na wilaya za nchi jirani ambako pia wakazi wake wana nasaba na uhusiano wa damu na wenzao upande wa Tanzania.
“Serikali lazima ifanye kazi ya ziada kubaini na kuudhibiti mtandao huu kwa sababu si tu unahusisha wenye fedha, bali pia viongozi wenye ushawishi ndani ya CCM na Serikali,” alisema mtoa taarifa wetu.
Akizungumzia nguvu ya mtandao huo, Hapi alisema; “Serikali ina mikono mirefu, hakuna atakayejihusisha na mtandao huo na kubaki salama.”
Barrick North Mara
Akitoa taarifa wakati wa ziara ya Hapi, Meneja wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko alisema mwaka mmoja uliopita, yameripotiwa matukio 76 ya wizi wa mawe yenye dhahabu yanayoaminika kufanywa na watu kutoka nje kwa ushirikiano wa wafanyakazi wasio waaminifu.
“Wizi huu unafadhiliwa na mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu wanaowapa fedha vijana kutekeleza wizi huo. Ili kuwaondolea woga na hofu, vijana hao hupewa pombe na aina nyingine ya vitu vya kulevya. Tunaiomba Serikali utusaidie kukomesha wizi huu,” alisema Lyambiko.
No comments :
Post a Comment