Thursday, May 5, 2022

SHEHENA YA KWANZA YA PARACHICHI KUTOKA TANZANIA YAWASILI NCHINI INDIA

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega (kushoto mwenye miwani myeusi) akikata utepe wakati wa mapokezi rasmi ya Kontena lenye matunda aina ya Parachcihi kutoka Tanzania lililowasili nchini humo tarehe 04 Mei 2022 kupitia Bandari ya Jawalar Nehru ya mjini Mumbai. Kontena hilo la Parachichi limewasili nchini humo kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya IG Fruits ya India na Kampuni ya Avoafri ya Makambako mkoani Iringa.

Balozi Anisa (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa bandari ya Mumbai baada ya kupokea na kufungua Kontena lenye Parachichi kutoka Tanzania

Picha ya pamoja

Balozi Anisa akiwa kwenye mazungumzo na Naibu Mwenyekiti wa Bandari ya Jawaharlal Nehru ya Mumbai, Bw. Unmesh Sharad Wagh baada ya kupokea matunda hayo ya parachichi kutoka Tanzania. Katika mazungumzao yao walikubaliana kushirikiana katika kubadilishana ujuzi kati ya Tanzania na India kwenye masuala ya Bandari
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega leo tarehe 04 Mei 2022 amepokea kwa mara ya kwanza shehena ya matunda aina ya Parachichi (Avocado) kutoka Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za Ubalozi huo za kutafuta masoko ya bidhaa za mazao ya mbogambog ana na matunda nchini India.

Akizungumza na Naibu Mwenyekiti wa Bandari ya Jawalarlal Nehru ya mjini Mumbai, Bw. Unmesh Sharad Wagh mara baada ya kupokea shehena hiyo, Balozi Mbega ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo na kwa pamoja na Bw. Wagh walikubaliana kushirikiana katika sekta ya uchukuzi hususan katika kubadilishana ujuzi kwenye masuala ya Bandari.

Katika maelezo yake Balozi Mbega amesema kuwa, wafanyabiashara wa India wamehamasika kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanywa nchini humo na Ubalozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa hapa nchini na sasa wapo tayari kuanza kuingiza matunda aina ya Nanasi na Embe kutoka Tanzania.

“Huu ni mwendelezo wa juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Serikali na TAHA wa kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa za mazao ya mbogamboga na matunda nchini India. Wafanyabiashara wa India wamehamasika na sasa wanakamilisha taratibu za kuanza kuingiza nanasi na embe za Tanzania nchini India, amesema Balozi Mbega.

Pia, Balozi Mbega amekishukuru Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) kwa ushirikiano wao uliofanikisha shehena hiyo ya Parachihci kuwasili India salama.

Shehena hiyo ya kwanza ya parachichi imewasili nchini India kupitia Bandari yaJawalar Nehru ya mjini Mumbai kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya IG Fruits ya India na Kampuni ya Avoafrica ya Makambako mkoani Iringa.

No comments :

Post a Comment