Friday, May 6, 2022

MKURUGENZI MKUU COSTECH DK.AMOS NUNGU AZINDUA PROGRAMU PesaTech INAYOLENGA KUKUZA MAWAZO YA KIBUNIFU



MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amezindua programu ya PesaTech Accelerator inayolenga kukuza mawazo ya kibunifu kwa ajili ya mifumo ya Sekta ya Fedha nchini.


Halfa ya uzinduzi huo imefanyika katika ukumbi wa ZO Space (mkabala na Millenium Tower), barabara ya Bagamoyo, jijini Dar es Salaam.



"Serikali kupitia COSTECH, tunajivunia kwa kuwa  tumeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu hapa nchini, program tuliyoizindua hii leo itawasaidia wabunifu nchini kuongeza maarifa, kujenga mtandao, na kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza bunifu zao" alisema Dkt. Nungu.

"Mh. Rais katika mahojiano na ndg. Mhando wa Azam TV, alisema jinsi ubunifu unavyowezesha vijana kujiajili na kutoa ajira kwa wenzao ambapo aliitaja Magilla na Maxcom wakiwa ni mfano wa wanufaika wa kumbi za bunifu kupitia COSTECH" aliongeza Dkt. Nungu.

Dkt. Nungu aliwataka wabunifu wa mifumo ya kifedha nchini kujitokeza kwa wingi katika kushiriki katika hiyo program ya PesaTech Accelerator ili wapate fursa ya kujengwa na kuunganishwa na wafadhili mbalimbali – kujenga kampuni changa nyingine mfano wa Nala inayoongozwa na Benjamini Fernandes ambaye amepata uwekezaji wa Fedha za kimarekani milioni kumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike alieleza kuwa
“Tutafanya kazi hii kwa karibu kabisa na COSTECH, tuko hapa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Nungu vileivile tunashirikiana na wadau muhimu kama UNCDF  lengo likiwa ni kutambua vijana wenye mawazo ya kibunifu kwa  kuwapatia msaada wa kifedha, kiufundi, nyenzo pamoja na msaada wa kibiashara ikiwemo kupatiwa mitaji ili mawazo yao yaingie sokoni na kuleta tija katika jamii” alisema

Bi. Anneth Kasebele amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Mitaji - UNCDF kwa kushirikiana na Serikali  na makampuni binafsi wataendelea kusaidia miradi ambayo imejikita kwenye mifumo  ya kifedha na bunifu za mageuzi ya kidigitali kupitia sekta za kifedha. Aliongeza kuwa dira yao ni kusaidia kuchochea jitihada zilizopo na kupanua wigo wa huduma ndani na nje ya nchi.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Utafiti toka Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Alfred Mkombo alisema kupitia uzinduzi huo wabunifu katika sekta ya fedha nchini wataweza kusaidiwa kwa kuendeleza mawazo yao eneo la fedha, masoko na mitaji na kwa kuendelea kutoa miongozo itakayosaidia kutoa mawazo mapya  yatakayoleta maendeleo hapa nchini.


Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau  wa ubunifu nchini wawezeshaji kwa maana ya UNCDF na Ubalozi wa  Swedish; washirika wa mradi: Sahara Ventures, Enea Advisors, Hindsight Ventures ;  pamoja na wadau wa Sekta za Kifedha zikiwemo Taasisi ya  Flutterwave, CRDB, Mwalimu bank  na Wabunifu wa  Tunzaa, Tausi, na Bizzyn.

No comments :

Post a Comment