Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa akipiga mpira leo Mei 5, 2022 wakati wa uzinduzi wa ziara ya Kombe hilo nchini, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa leo Mei 5, 2022 akiwa katika picha ya pamoja.Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa akiwana mpira leo Mei 5, 2022.
Na John Mapepele
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi kulipokea Kombe la Dunia kwenye ziara yake nchini Mei 31, 2022 kwa niaba ya watanzania wote ikiwa ni mkakati maalum wa kuitangaza Tanzania na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi Juni 1, 2022 Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuliona na kupiga picha.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema haya leo Mei 5, 2022 kwenye uzinduzi wa ziara ya Kombe hilo nchini, jijini Dar es Salaam ambapo amepiga mpira na kufunga penati kwenye goli la mfano na kuashiria ufunguzi rasmi wa ziara ya ujio wa kombe hilo nchini.
Amesema ujio wa kombe hilo unaonyesha jinsi Shirikisho ya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) linavyotambua jitihada kubwa zinazofanywa na Tanzania kwenye michezo katika kipindi hiki.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imefanya mapinduzi makubwa kwenye michezo katika kipindi kifupi kwa kuwa inaamini kuwa michezo ni biashara inayozalisha ajira kubwa na kwamba inachochea uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ameongeza kwamba katika kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa Serikali katika kipindi hiki imeridhia kuratibu na kufadhili Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika utakaofanyika jijini Arusha ambao utahudhuriwa na zaidi ya nchi 54 pamoja na viongozi wakuu wa mashirikisho na vyama vikuu vya michezo akiwemo Rais wa FIFA.
Amesema mkutano huo unafanyika jijini Arusha eneo ambalo ni kitovu cha utalii nchini, jambo ambalo litasaidia kufungua milango ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kwa wageni watakaoshiriki kwenye mkutano huo.
Kwa upande mwingine, amesema Serikali imedhamiria kuandaa miundombinu ya kisasa ya michezo ili kuweza kuratibu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika hapa nchini ambapo ameiomba Kampuni ya Coca Cola kujitokeza kushirikiana na Serikali kujenga viwanja vitakaokidhi mataka ya kufanya mashindano hayo ya kimataifa.
“Natambua mchango wenu katika michezo na kuitangaza Tanzania kwa ujumla nipende kutumia fursa hii kuwaomba Coca Cola kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi huo. Tunahitaji viwanja vitatu ili tuweze kuandaa mashindano haya” amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Amemwagiza Mkurugenzi wa Michezo nchini, Yusufu Singo kuhakikisha Wizara inashirikiana na Coca Cola kutengeneza mfumo wa matangazo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa utakaokuwa ukikodishwa kurusha matangazo kwa makampuni mbalimbali.
Pia ameagiza Idara ya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kuwatafuta wachezaji watanzania wanaocheza katika timu za kubwa duniani ili kuunda timu bora ya taifa itakayoweza kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Coca Cola Kwanza Tanzania, Unguu Sulay, Kampuni ambayo inadhamini ziara ya ujio wa Kombe hilo nchini amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopewa heshima ya kutembelewa na Kombe hilo na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na wizara.
Rais wa TFF, Wallace Karia ameipongeza Serikali kwa juhudi za kufanya maboresho kwenye sekta za michezo nchi huku akifafanua kuwa Wizara imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na wadau kuliko awali hali inayopelekea kuanza kufanya vizuri kwenye michezo.
No comments :
Post a Comment