Saturday, April 9, 2022

Waziri Mkuu wa Burundi aipa kazi CRDB

crdbpic

By Mwandishi Wetu

Benki ya CRDB imeonekana kuwa daraja muhimu la kukuza biashara na mahusiano katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hasa kwa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya

Kongo (DRC) na Burundi.

Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu wa Burundi, Alain Guillaume Bunyoni ambaye ameeleza kufurahishwa kwake na CRDB kufungua kampuni yake tanzu nchini DRC itakayokuwa na makao yake makuu jijini Lubumbashi na kutaka huduma hizo kusogezwa karibu na mpaka wa Burundi na DRC.

"Ninaiomba benki kufungua matawi karibu na mipaka ya Burundi na DRC, katika miji ya Uvira na Bukavu ili kuimarisha biashara," Bunyoni amesema wakati alipotembelewa na ujumbe wa Benki ya CRDB ofisini kwake.

Kwa sasa benki hiyo kwa sasa inatoa huduma katika nchi ya Burundi na inaelezwa kuwa katika robo ya tatu itazindua huduma zake kupitia kampuni tanzu huko Lubumbashi, jiji la pili kwa ukubwa baada ya Kinshasa, nchini DRC.

Kuanzishwa kwa kampuni tanzu hiyo kunaendana vyema na hatua za hivi karibuni ambapo, nchi ya DRC imekubaliwa ombi lake la kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hivyo kufanya jumla ya nchi saba wanachama katika ukanda huu.

Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRDB, Dk Ally Lay na Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Abdulmajid Nsekela waliombatana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Mareko.

Katika mazungumzo, uongozi wa CRDB umemhakikishia Bunyoni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Burundi katika kufadhili miradi ya pamoja ukiwemo ule wa mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Bunyoni kwa upande wake, aliishukuru CRDB kwa kusaidia kukuza uchumi wa Burundi kupitia uwezeshaji wa utoaji mikopo inayogusa makundi mbalimbali ya wateja kuanzia kupitia watu binafsi, kampuni na hata Serikali.

"Niwahakikishie kuwa Serikali yetu inaunga mkono jitihada mnazozifanya katika kuinua uchumi wa Burundi, na tupo tayari kushirikiana nanyi katika utekelezaji miradi mikubwa,” amesema Bunyoni na kuongeza:

"Ni muhimu kutambua kuwa benki hii kupitia programu yake ya mageuzi ya kidijitali imesaidia kurahisha miamala ya kibiashara ya kati ya Burundi na Tanzania kwa kuweka mifumo na miundo mbinu wezeshi.”

Naye Dk Laay amemweleza Bunyoni kuwa benki hiyo imewekeza zaidi katika mifumo ya kidijitali ili kuwawezesha wateja kuokoa muda na kupanua huduma maeneo ambayo hayajafikiwa.

"Hii itasaidia Burundi katika utekelezaji wa ajenda ya kuongeza ujumuishi wa kifedha," Dk Laay amesema na kuongeza:

"Ni katika muktadha huo benki sasa inasambaza huduma za CRDB Wakala maarufu kama ‘Turihose’ hapa Burundi pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma za SimBanking.”

Kwa upande wake, Nsekela amemweleza Bunyoni kuwa kwa sasa benki hiyo inashika nafasi ya tatu kwa utoaji wa mikopo nchini Burundi baada ya miaka 10 ya kufanya kazi na asilimia 20 ya mikopo imesaidia Warundi wengi kuanzisha biashara.

"Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, benki imeendelea kusaidia uchumi wa Burundi kwa kutoa bidhaa na huduma bunifu kwa kampuni, watu binafsi na taasisi kupitia bidhaa za kuweka amana na mikopo," amesema.

No comments :

Post a Comment