Thursday, February 24, 2022

WIZARA YA AFYA YAPOKEA MSAADA KUTOKA WHO

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui(kushoto) akipokea msaada wa dawa na  vifaa Tiba  vyenye thamani  ya  bilioni 1.3 za Kitanzania kutoka Shirika la Afya duniani (WHO) hafla iliyofanyika Bohari kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar.
Mwakilishi mkaazi Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania Dk.Tigest Ketsele akizungumza machache wakati wa makabidhiano ya dawa baina yao na Wizara ya Afya  huko Bohari kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akizungumza wakati wa makabidhiano ya dawa na Vifaa baina ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Bohari kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar.
Mkurugenzi Bohari kuu Zahran Ali akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya  makabidhiano ya  msaada wa dawa na vifaa tiba baina ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani WHO,huko Bohari kuu  Maruhubi Zanzibar. Picha na Fauzia Mussa-Maelezo Zanzibar

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR.

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea msaada wa Madawa na Vifaa Tiba vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 za kitanzania kutoka Shirika la Afya duniani WHO. Vifaa hivyo vitatumika kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kiafya nchini ikiwemo maradhi ya Uviko 19.



Akipokea msaada huo Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui amesema msaada huo umekuja muda muafaka kutokana na Zanzibar kukabiliwa na uhaba wa baadhi ya dawa.

Amesema Shirika la WHO limekuwa bega kwa bega na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha linasaidia kuimarisha afya za wananchi. Ameishukuru WHO kuendeleza mashirikiano yake kwa Zanzibar hasa katika mripuko wa Janga la Korona uliotokea nchini.

Waziri Mazrui ameahidi kutoa kila aina ya ushirikiano ili shirika hilo lifanye kazi zake kwa ufanisi. Ameahidi msaada huo kutumika ipasavyo kama Shirika hilo lilivyoagiza ili kutimiza malengo yaliyokusudia.

 Akielezea hali halisi ya Ugonjwa wa Uviko 19 Waziri Mazrui amesema kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyebainika na maambukizi ya maradhi hayo.Hata hivyo amesema juhudi mbalimbali zinapaswa kuchukuliwa ili Zanzibar iendelee kuwa salama dhidi ya maradhi mbali mbali ikiwemo ya Uviko 19.
 
Kwa upande wake Mwakilishi mkaazi wa WHO Tanzania Dkt. Tigest Ketsele ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata nchini.

Akielezea kuhusu msaada walioutoa Dkt. Tigest amesema msaada huo ni mchango kutoka Nchi tofauti duniani ikiwemo Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya. Awali Mkurugenzi wa Bohari kuu ya Dawa Zahran Ali alisema Zanzibar kama ilivyo nchi nyingine zinahitaji Dawa na Vifaa tiba mbalimbali ili kukabiliana na maradhi.

 Aidha ameishukuru WHO kwa kazi yao nzuri wanayoifanya ikiwemo misaada mbali mbali ya Dawa na mafunzo kwa wataalam wa afya nchini.

 Mapema Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alifungua Mkutano wa pamoja kati ya Shirika la Afya ulimwenguni WHO na Wizara ya Afya kuhusu masuala ya sekta ya Afya. Alisema utoaji wa huduma zenye ubora zinakwenda sambamba na kupanga mipango na mahitaji mapema katika sekta ya Afya.


No comments :

Post a Comment