Friday, February 25, 2022

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZUNGUMZA NA VIONGOZI MBALIMBALI BAADA YA MKUTANO WA MPANGO WA AMANI, USALAMA NA USHIRIKIANO NCHINI DRC ,

TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA MATAIFA MENGINE KUDUMISHA AMANI AFRIKA -MAJALIWA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi katika mkutano wa pembeni baada ya kumalizika kwa mkutano wa kumi wa wakuu wa nchi wa Serikali zinazohusika na mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini DRC na kwenye ukanda wa maziwa makuu uliofanyika, jijini Kinshasa, DRC Februari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye baada ya kumalizika kwa mkutano wa kumi wa wakuu wa nchi wa Serikali zinazohusika na mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini DRC na kwenye ukanda wa maziwa makuu uliofanyika, jijini Kinshasa, DRC Februari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa anayeshughulikiwa masuala ya amani Jean-Pierre Lacroix baada ya kumalizika kwa mkutano wa kumi wa wakuu wa nchi wa Serikali zinazohusika na mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini DRC na kwenye ukanda wa maziwa makuu uliofanyika, jijini Kinshasa, DRC Februari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha amani, ushirikiano, ustawi wa kijamii na kiuchumi unaendelea kushamiri katika nchi zote za Bara la Afrika.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere Serikali ya Tanzania imeshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi barani Afrika, kutoa hifadhi kwa wakimbizi pamoja na kushiriki katika kazi ya kulinda amani.

 

Ameyasema hayo  (Alhamisi, Februari 24, 2022) alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano  wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)

 

Amesema katika kuhakikisha inashiriki kwenye ukuzaji wa ustawi wa kiuchumi barani Afrika, Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kutoka uvinza (Tanzania)- Gitega (Burundi) hadi Kindu (DRC).

 

 “Pia tunajenga SGR kutoka Isaka (Tanzania) hadi Kigali (Rwanda)” Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa mradi mwingine unaolenga kukuza uchumi wa Afrika ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanzania).

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amependekeza kuwa katika mikutano mingine ya nchi wanachama wa Makubaliano ya Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC na Ukanda wa Maziwa Makuu Lugha ya Kiswahili iongezwe kama mojawapo ya lugha rasmi ya mikutano hiyo.

 

“Ni heshima kubwa sana kwa lugha yetu ambayo kwa sasa imepata idhini kutumika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”

 

Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Nchi na Serikali umepitisha Taarifa ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na pamoja na  maazimio yake. Mkutano wa Tisa ulifanyika Jijini Kampala, Uganda tarehe 08 Oktoba, 2018.

 

Mkutano huo umeongozwa na Mheshimiwa Rais FĂ©lix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC baada ya kukabidhiwa Uenyekiti na Mwenyekiti wa sasa Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.

 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa mkutano huo, Rais wa DRC, Mheshimiwa Tshisekedi alimshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Mheshimiwa Yoweri Museveni pamoja na viongozi wengine kwa kazi kubwa wanayoifanya.

 

Kadhalika, kiongozi huyo ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na mtangulizi wake kwa faida ya DRC na Afrika kwa ujumla. Amesema viongozi hao wanaisadia nchi ya DRC katika kuimarisha ulinzi na Amani hususani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

 

Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulizinduliwa nchini Ethiopia Februari 24, 2013 baada ya Wakuu wa Nchi 11 kusaini mkataba ulioanzisha mpango huo.

 

Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Angola, Afrika Kusini, Burundi, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kongo, Uganda na Zambia. Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Sudan zilijiunga na mpango huo Januari 31, 2014.

 

Mpango huo unalenga kusitisha mapigano Mashariki mwa DRC na maeneo mengine ya Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na kutoa majukumu kwa DRC kuimarisha usalama, nchi jirani kutoingilia masuala ya ndani ya DRC na kutounga mkono makundi ya waasi nchini humo.

 

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa DRC Mheshimiwa Tshisekedi ambapo pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara.

 

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Tshisekedi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini DRC, pia ametumia fursa hiyo kutoa nafasi kwa Watanzania kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo. “Zaidi ya Majimbo ya DRC wanazungumza Kiswahili.”

 

Viongozi wengine aliofanyanao mazungumzo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya amani Jean-Pierre Lacroix ambapo Waziri Mkuu alimuhakikishia kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kushiriki katika kusimamia upatikanaji wa amani kwenye mataifa mengine. 

 

Pia, Waziri Mkuu alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye ambapo pamoja na mambo mengine walijadiliana namna ya kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha uchumi.

 


No comments :

Post a Comment