Friday, February 25, 2022

TRILIONI 1.66 ZATOLEWA KUIMARISHA SEKTA YA AFYA


Na. Majid Abdulkarim, WAF - DODOMA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema Zaidi ya shilingi Tilioni 1.66 zilizotolewa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu (Global Fund) zitatumika kuongeza kasi ya kuimarisha sekta ya afya kwa kuzingatia maeneo makubwa ya vipaumbele vya sekta ya afya ambavyo vitaweza kuonekana kwa macho kwa watanzania.

Kauli hiyo imebainishwa leo Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund) Bw. Linden Morrison aliyeambatana na wataalam wake waliopo nchini kwa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya afya inayotekelezwa hapa nchini.

Prof. Makubi amesema kuwa vipaumbele hivyo ni Ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika hospitali za mikoa ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi billion 27 zimetumika na zinaendelea kutumika kwa ajili ya kuimarisha hospitali kwa kufanya ujenzi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Prof. Makubi amesema ununuzi wa dawa na vitendanishi vya maabara kwa wagonjwa wa UKIMWI,Kifua Kikuu na Malaria pia ni kipaumbele cha pili ambapo Zaidi ya bilioni 881 zishatumika na zinaendelea kutumika mpaka 2023.

“Eneo la tatu ni usimikaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini hususani katika ngazi ya msingi kuanzia Halmashauri, vituo vya afya mpaka zahanati ambapo husimikaji huu umetumia Zaidi ya bilioni 9”, ameeleza Prof. Makubi.

Vilevile Prof. Makubi emeongeza kuwa mfuko huo umewezesha ununuzi wa Magari 105 ya kubebea wagonjwa ambapo mpaka sasa zimeshaanza kutimika bilioni 8.8

Lakini pia Prof. Makubi amesema kuwa eneo muhimu wakati wa Uviko-19 Global Fund wamesaidia kununua mitambo ya kuzalisha hewa ya Oksijeni katika hospitali za mikoa na baadhi za kanda ambapo bajeti yake imekuwa ni bilioni 14.6.

“Tumeweza kushirikiana nao katika kuimarisha mifumo ya Tehama katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya hasa katika hospitali za mikoa na halmashauri tumetumia bilioni 12.1”, amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameendelea kusema kuwa kupitia Mfuko huo wa Dunia itasaidia kujenga uwezo katika sekta ya afya ambapo wameweza kutoa ajira za muda mfupi za mkataba ili kuimarisha sekta hiyo kwa kupunguza uhaba wa wataalamu wa afya katika miundombinu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa nchini.

“Hivyo ni wahakikishie usimamizi imara katika matumizi ya fedha hizo na fedha hizo zitatumika kulingana na zilivyo lengwa na bila kuchelewa ili kuleta tija kwa watanzania”, amesisitiza Prof. Makubi.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund), Bw. Linden Morrison amesema kuwa wataendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na wao.

“Napenda kusema kuwa nimefurahishwa na ubunifu mlionao wa kutatua changamoto ya uhaba wa watoa huduma za afya kwa kuwapa ajira za mkataba na badae kuajiri katika ajira ya kudumu”, ameeleza Bw. Morrison.

Naye Mratibu wa Mfuko wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua kikuu (Global Fund) kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Renatus Kisendi amesema wanajukumu kubwa la kuhakikisha fedha zinazokuja kusaidia sekta ya afya nchini zinafika kwa watekelezaji ili ziweze kufika kwa wananchi na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.






No comments :

Post a Comment