Sunday, February 27, 2022

JAMII YAASWA KUKABIDHI JUKUMU LA USIMAMIZI WA MIRATHI KWA RITA BADALA YA NDUGU WA MAREHEMU

Waziri wa Katiba na SheriaMhe. George Simbachawene (kulia) akipokea taarifa ya utekelezaji ya Bodi ya Ushauri ya RITA iliyomaliza muda wake kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Hamis Dihenga. Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda.


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA iliyomaliza muda wake Prof. Hamis Dihenga akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa bodi hiyo kwa miaka mitatu kuanzia 2019 hadi 2022 kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene ( hayupo pichani) kabla ya kukabidhi kwake taarifa hiyo.



Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA iliyomaliza muda wake Prof. Hamis Dihenga akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa bodi hiyo kwa miaka mitatu kuanzia 2019 hadi 2022 kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene ( hayupo pichani) kabla ya kukabidhi kwake taarifa hiyo.

Jamii imetakiwa kutokuhangaika kutafuta watu ndani ya familia kusimamia mali za

marehemu kutokana na baadhi yao kutokuwa waadilifu kwa kusababisha migogoro ya kugombania na kufuja mali hizo na badala yake wakabidhi jukumu hilo kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ambapo sheria umeupa mamlaka kisheria kusimamia mirathi kuandika na kuhifadhi wosia.


Hayo yamesemwa hii leo Jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Goerge Simbachawene wakati akipokea taarifa ya Bodi ya Ushauri ya RITA ambayo imemaliza muda wake tangu mwaka 2019 hadi 2022 chini ya Mwenyekiti wake Prof. Hamis Dihenga.

Mhe. Simbachawene amekemea vikali tabia za baadhi ya wanandugu kuanzisha migogoro ya mirathi isiyokwisha katika jamii na kusababisha mali nyingi za marehemu kupotea kwa kuchukuliwa kiholela na watu wanaojifanya ni ndugu wa karibu au wasimamizi wa mirathi huku nia yao ni kupora mali hizo na kuwaacha watoto na wajane wakiwa katika majonzi ya kufiwa na kupokonywa mali na hivyo serikali kuingia katika jukumu la malezi ya familia hizo.

‘’Ni afadhali uamue hivi sasa ukiwa na afya njema kuandika wosia kwani RITA moja ya majukumu yao ni hilo kuandika na kutunza wosia na itasaidia kutoa maelekezo na muelekeo wa namna mali zako zitakavyogaiwa hivyo kupunguza au kuondoa kabisa uwezekano wa kuzuka kwa migogoro ya mirathi katika jamii’’ Alisema.

Waziri Simbachawene alisema usajili wa vizazi na vifo ungekamilika kwa asilimia kubwa kwa nchi nzima zoezi la sensa lingekuwa ni kazi rahisi na kuwezesha kujenga msingi bora wa uchumi wa kisasa kwani uwepo wa taarifa zilizo sahihi za vizazi na vifo husaidia kupanga mipango ya maendeleo kwa nchi.

Pia ameziagiza Bodi za wadhamini wa Taasisi za Kidini, Asasi za Kiraia na Vyama vya Siasa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi ili kuepuka kugogoro na kupelekea kuzorotesha usimamizi wa mali na utoaji wa huduma kwa jamii kama inavyobainishwa majukumu yao kupitia katiba zao zilizowasilishwa wakati wakisajiliwa na kutambulika kisheria kupitia RITA na Wizara ya Mambo ya Ndani.

‘’Bodi za wadhamini zinaposajiliwa zichunguzwe kwa umakini malengo yao kupitia katiba zao ili kuepuka migongano ya kimaslahi baina yao inayopelekea baadhi ya wanachama kukosa haki na kushindwa kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika katiba zao’’. Alisema Mhe Simbachawene.

Wakati huo huo ameipongeza Bodi ya ushauri ya RITA iliyomaliza muda wake kwa kusimamia vizuri majukumu ya wakala na kuwezesha ongezeko la kiwango cha usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoka asilimia 13 (Sensa, 2012) hadi kufikia asilimia 65 Mwaka 2021 sawa na watoto 7,328,985 na kuifanya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi tano kati ya nchi 54 za Afrika, kuwa kinara wa Usajili na kuongoza katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya RITA iliyomaliza muda wake amesema kuwa wakati umefika kwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuamua kwa pamoja kuhusu masuala ya usajili wa vizazi na vifo kulifanya kuwa ni jambo la lazima na kwa kuiwezesha RITA kwenye rasilimali watu na fedha ili kuweza kuyafikia makundi yote yenye sifa za kusajiliwa kwani taarifa zao zitaisaidia serikali katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Bodi ya Usauri na Udhamini ya RITA imetekeleza majukumu mbalumbali ikiwemo Mpango wa Usajili wa Watoto walio na Umri wa Chini ya Miaka Mitano, Mpango wa kuondoa bakaa ya wasiosajiliwa, Usajili wa watoto wa miaka 5-17, Usajili wa makundi mengine, Mpango wa Usajili wa Matukio ya Vifo, Matumizi ya TEHAMA katika shughuli za usajili , Usajili wa vizazi, vifo, ndoa na Bodi za Wadhamini kielektroniki na Mapitio ya Sheria mbalimbali ikiwemo ya usajili wa vizazi na vifo sura ya 108.

Bodi ya Ushauri ya Wakala ilipewa jukumu kisheria la kumshauri Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu utendaji na utekelezaji wa majukumu ya wakala kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo hivi sasa bodi hiyo imemaliza muda wake na kukabidhi rasmi taarifa yake ambayo imeonesha mafanikio makubwa kwa kipindi hicho.

No comments :

Post a Comment