Monday, January 3, 2022

SPIKA NDUGAI AMUOMBA RADHI RAIS, WATANZANIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai alipokuwa akizungumza a Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dodoma kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo na yaliyotokea hivi karibuni hususani kwenye mitandao ya kijamii.

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amemuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan sambamba na Watanzania wote baada ya kuhisiwa kuzungumza maneno ya kuvunja Moyo kuhusu Mikopo wa Serikali.

Akizungumza na Wandishi wa Habari jijini Dodoma mapema leo, Spika Ndugai amesema katika Mkutano alioalikwa na Wana Dodoma, hakukuwa na lolote la kurudisha nyuma juhudi za Serikali wala hakuwa na nia ya kukashifu, kudharau juhudi hizo za Serikali ya Tanzania katika kutimiza azma yake ya Maendeleo.

“Serikali ni Baba yetu, Serikali ni Mama yetu, tunahitaji Serikali na tunaiunga Mkono, katika mazungumzo yetu tulisisitiza kujiimarisha kiuchumi, tulipe Kodi, tulipe ushuru mbalimbali, tulipe Tozo, huo ndio ulikuwa msisitizo wa hotuba yangu na kufanya hivyo tutaisaidia Serikali yetu kujitegemea zaidi na sisi kama Nchi kujitegemea zaidi”, amesema Spika Ndugai.

Amesema, jambo hilo limemuumiza baada ya kusikia kupitia Mitandao ya Kijamii kumnukuu kupinga Mkopo wa Serikali ya Tanzania wa Trilioni 1.3, huku akitolea mfano Jimboni kwake, Kongwa wamepewa Vyumba 112 vya Madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, amesema amefuatilia na kuhakikisha vyumba hizo vimeisha.

Spika Ndugai amesema, “Nimefuatilia suala hilo la utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Jimboni kwangu nimehakikisha tunakamilisha vizuri, kilichobaki ni Madawati tu na tutahakisha Watoto wanaingia kwenye Madarasa mazuri na ya kupundeza, hii yote ni juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan”.

Amesema Makusanyo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ni Shilingi Bilioni 3, akisema wamepata fedha nyingi kwa kiwango cha makusanyo ya ndani hivyo kuweka historia mpya katika Halmashauri hiyo.

Hivi karibuni, Spika Job Ndugai alinukuliwa na Vyombo mbalimbali vya Habari na Mitandao ya Kijamii akidaiwa kuikashifu Serikali ya Tanzania kuhusu Mikopo inayokopa kwa ajili ya Miradi ya Kimaendeleo nchini.

No comments :

Post a Comment