Monday, January 3, 2022

Rais Samia Atuıma Salamu Za Rambirambi Kufuatia Vifo Vya Watu 14.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti kufuatia vifo vya watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 02 Januari, 2022, saa 2:15 usiku katika Kijiji cha Lidumbe, Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara ACP Mark Njera amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika barabara ya ‘Uchumi’ Mtwara-Tandahimba-Newala-Masasi ni mwendokasi wa dereva wa gari aina ya Scania wakati aliposhindwa kulimudu na kwenda kuwagonga watu hao hali iliyopelekea vifo hivyo na kujeruhi watu wengine 22.

Mhe. Rais Samia amemtaka Mkuu Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Gaguti kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mhe. Rais Samia pia amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za   marehemu wote mahali pema peponi, Amina.

Aidha, Mhe. Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka, na pia amewaasa madereva kufuata na kuzingatia Sheria za usalama barabarani.

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

No comments :

Post a Comment