Waziri
wa nchi ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mheshimiwa Mudrik Soraga
Na Christian Gaya-HakiPensheni, Zanzibar.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar Mheshimiwa Mudrik Ramadhani Soraga aliwakumbusha waajiri juu ya wajibu wao wa kujisajili na Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) pamoja na wafanyakazi wao kuwa wanachama wakati wa mkutano mkuu wa sita wa wadau wa Mfuko huo uliofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Michezani jijini Zanzibar.
“Waajiri wa sekta binafsi
walitekeleze hilo na kuwasilisha michango kwa wakati ili walengwa wasipate
usumbufu unapofika wakati wa kustaafu. Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA)
ambao nao ni wadau wakubwa wa mkutano huu hawana budi kuwakumbusha waajiri juu
ya jukumu hili la kisheria ili kujenga mstakbala mzuri baina ya waajiriwa, ZSSF
na waajiri,”Waziri Soraga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alisema.
Waziri Soraga pia alitoa
shukurani zake za dhati kwa uongozi wa Mfuko wa ZSSF kuweza kuendelea na mikutano
hii ya wadau ukiwa mkutano wa wa sita uliyowajumuisha
wadau wa Mfuko huo kutoka taasisi za Serikali na za kampuni binafsi.
“Ni jambo lilowazi kwamba
fursa kama hizi za kukutana na kujadili kwa pamoja zikitumiwa ipasavyo
hutarajiwa kuleta matunda yasiyo mithilika katika Taasisi zetu,” Waziri Soraga
alitamka.
Pia aliwakumbusha waajiri
kujisajili na kuwasilisha michango kwa wakati ili walengwa wasipate usumbufu
unapofika wakati wa kustaafu.
“Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) ambao
nao ni wadau wakubwa wa mkutano huu hawana budi kuwakumbusha waajiri juu ya
jukumu hili la kisheria ili kujenga mstakbala mzuri baina ya waajiriwa, ZSSF na
waajiri.” Waziri alisisitiza.
Alisema hifadhi ya jamii ni
haki ya msingi ya kila mwananchi awe mtu mzima ama mtoto mdogo popote awapo
katika ulimwengu huu. Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 linasisitiza
hayo. Utekelezaji wa agizo hilo ulitokana na Azimio la Shirika la Kazi Duniani
nambari 102 la Hifadhi ya Jamii la mwaka 1952.
“Hifadhi ya jamii inaweza
kutafsiriwa kwa ujumla kama ni maandalizi au kinga ya kiuchumi na kijamii dhidi
ya dhiki inayosababishwa na kupoteza uwezo wa kipato kutokana na umri, maradhi,
kuumia kazini au kufariki dunia. Kutokana na athari kubwa ambazo mwanachama
anaweza kuzipata kwa kupoteza kipato, uendeshaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
ni jukumu la Serikali zote duniani,”Waziri Soraga alifafanua.
Alisema sekta ya hifadhi ya
jamii kwa Zanzibar inayo historia ndefu sana. Sekta hii ilikuwepo kabla ya
Mapinduzi mwaka 1964 lakini walionufaika wakati huo walikuwa ni wachache tu
wale ambao waliobahatika kufanya kazi za ukarani katika Serikali ya Kikoloni na
pia kulikuwa na hifadhi ya jamii za kikabila au madhehebu.
“Tangu 1964 Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imefanya jitihada kubwa katika kuendeleza hifadhi ya jamii kwa
wananchi kupitia mfuko mkuu wa Serikali. Mfumo huu ulikuwa ndiyo njia kuu ya
hifadhi ya jamii Zanzibar mpaka mwanzo 1990 wakati Serikali ilipoanza kupambana
na hali ngumu ya uchumi. Pia ilichangiwa na ongezeko maradufu la watu kutoka
300,000 mwaka 1967 hadi 750,000 mwaka 1997,”alifafanua zaidi.
Alisema mfuko wa ZSSF ulianzishwa
kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1998 ambayo ulirekebishwa na Sheria Na 9 ya mwaka
2000, pia ulirekebishwa kwa notisi ya Serikali ya 2004 na kuanzishwa upya kwa
Sheria Na 2 ya mwaka 2005 baada ya kufanyiwa mapitio. Mkutano huu ni fursa
adhimu kwenu kupata wasaa wa kukutana na uongozi wa Mfuko, ili kuweza kuona
jinsi ya mambo yanavyoendeshwa ndani ya Mfuko wa ZSSF. Lakini pia mtapata fursa
ya kutoa maoni yenu ambayo ninaamini yatakuwa chachu ya maendeleo ya Mfuko huu.
“Naomba kutumia fursa hii
kukumbushana machache yanayohusu Mfuko huu na jinsi tunavyoweza kuutumia na
kufaidika nao. Yapo maeneo ambayo tayari yamekwisha elezwa vizuri na wasemaji
waliopita. Madhumuni makuu ya mkutano huu ni kuzidisha mashirikiano baina ya
Mfuko na wadau wake sambamba na kuondoa changamoto zinazoukabili. Hivyo naomba
muitumie fursa hii kwa kuona utendaji ulivyofikiwa na kutoa mawazo chanya na
kuamini kuwa Mfuko huu ni wetu sote,” Waziri Soraga alisisitiza.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni, mipango ya kustaafu na elimu ya kuwekeza pensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni website: Simu 0655 13 13 41

No comments :
Post a Comment