Friday, December 3, 2021

MADAKTARI WALIOPATIWA MAFUNZO NA WCF WAONGEZEKA NA KUFIKIA 1,322 NCHI NZIMA: DKT. OMAR

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akifuatilia majadiliano ya vikundi mwisho mwa mafunzo hayo.

Majadiliano ya vikundi.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendahi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dkt.Godlove Mbwanji (wapili kushoto) akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo hayo, Dkt. Marther Chacha huku Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Juma Mabrouk (kushoto) akishuhudia.
Baadhi ya washiriki.
Dkt. Adolph Daudi kutoka Hospitali ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake.
Afisa Tathmini za madai, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Matilda Rusibamayila, akijibu maswali mbalimbali ya washiriki kuhusu Mafao yatolewayo na Mfuko
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, (MZRH) Dkt. Godlove Mbwanji akizungumza na washiriki.
Afisa Tathmini za madai, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Matilda Rusibamayila (wakwanza kulia waliosimama) akifuatilia majadiliano ya vikundi.

 NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mbeya.

IDADI ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi imepanda na kufikia 1,322 nchi nzima, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar amesema.

Dr. Omar ameyasema hayo Desemba 3, 2021 wakati wa kufunga

mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na WCF ili kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya jinsi yakufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kutoka mikoa saba ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa.

“Tukiwa tunaelekea mwaka wa saba tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu yake, ninyi ambao mmepatiwa mafunzo hapa, mnafanya idadi ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,322 kwenye mikoa yote Tanzania Bara.” Alisema.

Madaktari hao walijifunza sheria ya fedia, jinsi ya kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao, kusajili waajiri na namna wanavyoweza kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa njia ya mtandao, namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi na Mafao yatolewayo na Mfuko,

Kwa upande wao, washiriki hao waliupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wameeleza yamekuwa na manufaa makubwa kwao.

 “Nimejifunza mambo mengi ambayo nilikuwa siyafahamu,mfano sasa nimejua ya kwamba mtu anapokuwa amepata ajali itakayompelekea kupata ulemavu atastahili kufanyiwa tathmini pale tu atakapofikia kiwango cha juu cha kupona yaani maximum medical improvement.”. Dkt. Adolph Daudi Ntilagana, Hosptali ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi alisema.

Mshiriki mwingine Dkt.Pronent Mtei kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya alisema mafunzo hayo yamembadilisha kwani hivi sasa ameelewa kwamba Mfuko unaweza kumpatia matibabu au fidia mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.

“Nimejifunza na kuelewa tofauti ya magonjwa yatokanayo na kazi na yale ambayo hayatokani na kazi, hivyo itakuwa rahisi kwangu mteja anapokuja kwa changamoto ya maradhi kuweza kumtambua kama tatizo lake lina vigezo au la kwa mujibu wa mwongozo wa WCF.” Alisema Dkt. Mtei

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, (MZRH) Dkt. Godlove Mbwanji ambaye ndiye aliyafunga mafunzo hayo aliwaasa madaktari na watoa huduma za afya kuzingatia yale waliyojifunza wakati watakaporejea kwenye vituo vyao vya kazi.

“Mafunzo haya yatatusaidia sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini kuweza kufanya tathmini sahihi ambayo itauwezesha Mfuko kutoa tathmini sahihi na kwa wakati.” Alisisitiza.

No comments :

Post a Comment