NA MWANDISHI WETU, MNAZI MMOJA, DAR
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) umewatahadharisha Wanachama na Wastaafu kuwa makini wanapopigiwa simu na watu wasiowafahamu wakiwaelekeza kuwasaidia kupata malipo ya Mafao
Tahadhari hiyo imetolewa jana na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF Bw. James Mlowe wakati akitoa elimu kwa wanachama wanaofika kwenye banda la PSSSF kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Lengo la Wiki hiyo ni kuwapa fursa wananchi wa kada mbalimbali kukutana na taasisi za fedha za Umma na Binafsi ili kupata elimu ya huduma za fedha na hivyo kutambua fursa zilizopo ili kufaidika nazo na hivyo kuboresha maisha yao na hatimaye kujenga uchumi wa nchi.
Alisema kumekuwepo na matukio ya Wastaafu kutapeliwa na wahalifu wanaotumia teknolojia ya mtandao vibaya, wakiwapigia simu Wanachama na Wastaafu wa PSSSF wakijitambulisha kuwa ni maafisa kutoka Mfuko, Wizara ya Fedha au Ofisi mbalimbali za Umma na kuwapa maelekezo mbalimbali yanayopelekea kutapeliwa fedha za Mafao.
“PSSSF ina utaratibu wake mahsusi wa ulipaji wa Mafao, na malipo yetu tunayafanya moja kwa moja kwenye akaunti zao baada ya kupokea fomu zao za madai ya Mafao. hakuna utaratibu wa kuwalipa Mafao kupitia simu zao za mkononi au application mbalimbali za benki.” Alisema Bw. Mlowe na kufafanua….
Tunawaomba sana Wastaafu wanapopigiwa simu za aina hiyo wasifanye jambo lolote na badala yake wawasiliane na Mfuko kwa ufafanuzi zaidi…………………matukio haya yamekuwa yakitokea sehemu mbalimbali za nchi, mtandao wa wahalifu hawa ni mkubwa, tunawaomba mnapopigiwa simu zinazohusu kuhamisha fedha au kupokea malipo kwa kutumia njia ambazo PSSSF haizitumii kulipa Mafao msifanye hivyo na badala yake toeni taarifa.
Alisema utaratibu wa Mfuko kuhusu malipo, huanzia hatua ya mwanachama kujaza fomu kupitia kwa Mwajiri wake na mwajiri anapoifikisha kwenye Mfuko fomu hizo hufanyiwa kazi na malipo yanalipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mwanachama ambayo ameijaza kwenye fomu.
“Na hata kama kuna mapunjo ya malipo (under payment) mwanachama anatakiwa kuandika barua ya kuomba mapunjo na sisi kama Mfuko tunashirikiana na mwajiri ili kujua sababu zilizosababisha hayo mapunjo na mwajiri anaporekebisha tunafanya utaratibu ule ule kwa kulipa moja kwa moja kwenye akaunti ya mwanachama na si vinginevyo.” Alifafanua Mlowe.
Hata leo hii tumepokea malalamiko kutoka kwa mwanachama wetu aliyekuwa Mtumishi wa Umma huko Mtwara naye alipigiwa simu na watu waliojitambulisha kuwa wako Hazina wakimueleza kwamba kuna mapunjo (underpayment) anayodai kwenye Mfuko na wakamuelekeza aingie kwenye application ya simu yake anayotumiaya SIM BANKING kwenye benki anayotumia wakamuelekeza kuwa watamsomea contral number ili wamfanyie malipo.
“Kumbe ile control number ni akaunti yao hao matapeli, kwa hiyo walikuwa wanampa maelekezo kwenye simu nay eye anayafuata na mwisho wasiku akawa amehamisha fedha kiasi cha shilingi milioni 5 (5,000,000) kutoka kwenye akaunti yake ya benki kwenda kwenye akaunti ya hao matapeli.” Alisema.
Aidha mwanachama mmoja wa PSSSF Bi. Hamida Mushi aliyefika kwenye banda la Mfuko huo ili kupata taarifa za michango yake, amewashauri wanachama wenzake kujiepusha na taarifa za mtaani ambazo sio rasmi na badala yake wafike kwenye ofisi za PSSSF ili kupata taarifa sahihi.
“Mimi ninafanya kazi Maktaba Kuu ya Taifa hapa Dar es Salaam, nilivyosikia kuna Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa hapa Mnazo Mmoja na kwamba taasisi za Umma zitashiriki, nikaona nikitoka tu kazini nifike hapa ili kuuliza masuala mbalimbali ya michango yangu maana nakaribia kustaafu.” Alisema Mwanachama huyo na kuongeza……………..Nimefurahi kweli kweli maana nimepokelewa vizuri na nimepatiwa maelezo yaliyoniridhisha na hata nilipowaambia wanipatie taarifa yangu ya michango, wameni printia na nkunipatia, nimefurahi sana na ninawahimiza wenzangu wafike hapa Mnazi Mmoja kwenye banda la PSSSF wapate taarifa sahihi.” Alisema Bi.Hamida Mushi.
No comments :
Post a Comment