Sunday, November 14, 2021

Profesa Mkumbo Ataka Wahitimu CBE Waache Tabia Ya Kutafuta Ajira

 Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, akimpa cheti mmoja wa wanafunzi bra wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kwenye mahafali ya 57 ya Chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, na viongozi wa CBE wakiwa wamesimama kwaajili ya wimbo wa taifa kwenye mahafali ya 57 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), mwishoni  mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza kwenye mahafali ya 56 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), mwishoni  mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),  akizungumza kwenye mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni  mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.
Wahitimu wa fani mbalimbali wakiwa kwenye mahafali hayo ya 56 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo.

Na Mwandishi Wetu

WAHITIMU wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), wametakiwa kuacha tabia ya kuhangaika kutafuta ajira mara baada ya kuhitimu chuo na badala yake watumie elimu waliyoipata kutengeneza nafasi za ajira.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo ambapo wahitimu 800 wametunukiwa shahada za fani mbalimbali.

Amesema wanaohitimu kwa mwaka mzima wanafikia 800,000 hivyo ajira haziwezi kutosheleza wahitimu wote na suluhisho pekee ni kwao kutafuta cha kufanya kwa kutumia elimu waliyoipata chuoni hapo.

“Nafasi za ajira serikalini ni chache mno na mnaohitimu kwa mwaka mzima ni kama laki nane sasa cha msingi mkihitimu leo hii msianze kutafuta ajira tafuteni kazi, kazi zipo ila ajira ndiyo hazipatikani. Kazi ni kile kitu ambacho wewe mhitimu unataka kufanya ambacho kitakuingizia kipato bila kuajiriwa popote,” amesema Profesa Mkumbo.

Vile vile, Profesa Mkumbo amesema serikali inatambua na kupongeza mafanikio ya chuo hicho lakini inatambua changamoto za miundombinu ambazo chuo hicho bado kinakabiliana nazo.

Aidha ameutaka uongozi wa chuo hicho kuweka msisitizo katika mafunzo ya biashara kwa wanachuo na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wasiokuwa wanachuo na kufanya tafiti zinazolenga kutafua changamoto na matatizo katika sekta ya biashara na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Amesema serikali inatambua umuhimu wa elimu ya biashara katika maendeleo ya nchi pamoja na kwamba nchi zinazokua kiuchumi kwa kasi kubwa kama Brazil, Urusi,, India, China na Afrika ya Kusini zimewekeza sana katika teknolojia na kuipa umuhimu elimu ya biashara.

Amesema elimu ya ujasiriamali inahitaji wanachuo kuwa wabunifu na kushirikiana na watu wengine ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Amesema nchini Tanzania elimu ya ujasirimali inahitajika sana ili kuzitumia kwa ufanisi fursa na rasilimali zilizopo kama vile maziwa, mito, bahari, mabwawa, madini, vivutio vya utalii na mazao ya misitu.

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema amesema pamoja na kuongeza kozi chuo kimeendelea kujiimarisha katika suala zima la udhamini wa wahadhiri katika masomo ya shahada za uzamivu.

Amesema hilo linafanyika ili kuhakikisha chuo kinatoa elimu bora kulingana na uhitaji wa soko na kwamba mpaka sasa chuo kimeendelea kuwasomesha wanataaluma wake kufikia kiwango cha shahada za uzamivu (PhD) kwa kutumia fedha za ndani.

Profesa Mjema amesema kwa sasa chuo kina wanataaluma wahadhiri 35 wenye shahada za uzamivu kati ya wahadhiri 192 na bado chuo kinafanya mipango mbalimbali kuhakikisha kinawaendeleza wahadhiri ambapo kwa sasa kinawasomesha wahadhiri 43 ngazi ya uzamivu na wahadhiri wengine 11 katika ngazi ya uzamili.

Ameiomba serikali iendelee kuwapa ufadhili wahadhiri wa chuo hicho ili waweze kujiendeleza kitaaluma katika ngazi za ashahada za Uzamivu ambazo ni muhimu kwa taasisi ya elimu ya juu.

Profesa Mejama amesema chuo bado kinakubwa na uhaba wa fedha za kufanya tafiti lakini aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwalipa mishahara wafanyakazi wote wa chuo hicho.

“Huu ni mchango mkubwa sana kwa CBE ambao unahakikisha kuwa chuo hiki kama taasisi inajiendesha vizuri na kazi kubwa kwetu hapa ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu na jukumu la kufundisha linafanyika vizuri,” amesema

No comments :

Post a Comment