Wednesday, September 1, 2021

DKT. NCHEMBA AZIAGIZA HALMASHAURI KUWALIPA WAZABUNI NA WATOA HUDUMA

Waziri Wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu ambayo imepunguzwa kwa asilimia 30, jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Khatib Kazungu na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja.



Waziri Wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja.



Waziri Wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Khatib Kazungu, wakati akihitimisha mkutano wa Waziri na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.



Kamisha na Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Balandya Elikana na Afisa Sheria Mwandamizi wa wizara Bi. Mwantum Sultan wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayumo pichani), na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.



Mwandishi wa Habari Juma Kapalatu (ITV) akiuliza swali wakati wa mkutano wa Waziri Wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WFM)

******************************

Na. Regina Frank, Sandra Charles na Rahma Taratibu, (SJMC), Dodoma.

Halmashauri zote nchini zimeagizwa kuhakikisha zinalipa madeni yote ya watoa huduma ndani ya miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 mwezi Septemba mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu marekebisho ya tozo ya Miamala ya simu baada ya kusaini marekebisho ya Kanuni hizo jana.

“Mheshimiwa Rais anaguswa sana na madeni ya watoa huduma hasa watoa huduma wadogo, fedha zao kukaa Serikalini kwa muda mrefu, wengine walikopa kwenye mabenki na wengine wameshapata misukosuko, Mheshimiwa Rais ameagiza walipwe haraka”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema watoa huduma hao walipwe haraka ili fedha hizo ziingie kwenye mzunguko kwakuwa kutokuwalipa ni sawa na kuwatia umasikini kitu ambacho si lengo la Serikali.

Kuhusu Tozo za Miamala ya Simu, Mhe. Dkt. Nchemba alisema mpaka tarehe 31 Agosti 2021 Serikali imekusanya jumla ya Sh. bilioni 63 ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya 220 katika Tarafa zote 220 ambazo hazijawahi kuwa na huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru.

Alisema fedha zitakazokusanywa kutoka katika tozo hizo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kununua madawati ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

“Januari mwakani tutaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuongezeka mara mbili ya mwaka uliopita, si vema tukarudi kule tulikotoka kwa wanafunzi kufaulu 50 halafu anachaguliwa mmoja kutokana na ukosefu wa madarasa”, alifafanua Dkt. Nchemba.

Mhe. Nchemba alisema kwa ruhusa aliyopewa na Waziri wa Nchi TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu, amewaagiza Madiwani kutoa taarifa rasmi ya mahitaji ya Madarasa kwa kila Kata kwa ajili ya Wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Amesema taarifa hizo zitaiwezesha Serikali kugawa fedha kutokana na mahitaji ili kuhakikisha azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inayotaka wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa darasa la saba watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanadahiliwa.

No comments :

Post a Comment